Jumapili, 17 Machi 2019

SERIKALI YASHAURIWA KUTENGA MAENEO YA MAHAKAMA INAPOANZISHA MAENEO MAPYA YA KIUTAWALA


Na Lydia Churi- Mahakama- ARUSHA
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Arusha Mhe. Moses Mzuna ameishauri Serikali kutenga maeneo kwa ajili ya ujenzi wa majengo ya Mahakama pale inapoanzisha maeneo mapya ya kiutawala ikiwemo wilaya na mikoa mipya kama ilivyo kwa ofisi za serikali.  

Akizungumza na Wajumbe ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria wanaoendelea na ziara ya kukagua ujenzi wa majengo ya Mahakama unaoendelea katika maeneo mengi nchini, Jaji Mzuna alisema Mahakama katika baadhi ya maeneo nchini imekuwa ikijitafutia viwanja kwa ajili ya ujenzi wa majengo ya yake ambapo alisema endapo serikali itakuwa ikitenga maeneo hayo itaurahisishia Mhimili huo kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi.

Jaji Mzuna pia ameiomba kamati hiyo kushauri ili Mahakama iwe ikipatiwa mgao wa fedha za matumizi ya kawaida (OC) kila miezi mitatu badala ya kila mwezi ili kurahisisha upangaji wa vikao vya kusikiliza mashauri (Session) ikiwa ni pamoja na kuwajulisha mashahidi mapema na maandalizi mengineyo, hatua itakayosaidia umalizikaji wa mashauri kwa wakati na kupunguza mlundikano wa mashauri Mahakamani. 

Jaji Mzuna pia “Vikao vya kusikiliza mashauri yaani Session haviwezi kufanyika ipasavyo ikiwa mgao wa fedha za OC utakuwa ukitolewa kila mwezi”, alisisitiza Jaji huyo.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Arusha pia ameishukuru Serikali kwa kutatua changamoto za Mahakama ya Tanzania pamoja na Bunge la Tanzania kwa kuitetea Mahakama Bungeni.  

Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria wanaendelea na  ziara ya kukagua miradi ya ujenzi wa majengo ya Mahakama ya Tanzania ambapo jana wajumbe hao walitembelea mradi wa ujenzi wa jengo la Mahakama ya wilaya ya Longido mkoani Arusha.

Katika ziara hiyo, wajumbe hao walifurahishwa na kuipongeza Mahakama ya Tanza nia kwa hatua iliyofikiwa ya ujenzi wa Mahakama hiyo ambayo iko katika hatua ya umaliziwaji na kuishauri Mahakama kushirikiana karibu kamati hiyo katika ujenzi wa majengo ya Mahakama hasa pale wanapokutana na changamoto ambazo kamati hiyo ina uwezo wa kuzitatua.

Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria pia wanatarajia kutembelea na kukagua ujenzi wa jengo la Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoa wa Manyara ambayo inayoendelea kujengwa na sasa iko kwenye hatua ya umaliziwaji.
 Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Arusha Mhe. Moses Mzuna (katikati) akizungumza na wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria Ofisini kwake jana jijini Arusha. Kamati hiyo inaendelea na ziara ya kukagua ujenzi wa majengo ya Mahakama katika mikoa ya Mbeya, na Arusha na Manyara.



 Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Arusha Mhe. Moses Mzuna (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria walipomtembelea ofisini kwake jana jijini Arusha.
 Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Augustine Mahiga (wa pili kulia) akisikiliza jambo wakati wakati  wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria walipotembelea mradi wa ujenzi wa jengo la Mahakama ya wilaya ya Longido mkoani Arusha jana. Wa kwanza kulia ni Mwenyekiti wa  Kamati hiyo na Mbunge wa Rufiji Mhe. Mohamed Mchengelwa. 
 Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria Mhe. Amoni Mpanju (katikati)  akisikiliza jambo wakati wa ziara ya wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria katika Mradi wa Ujenzi wa jengo la Mahakama ya wilaya ya Longido mkoani Arusha jana.
 Mtendaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania Bwn. Solanus Nyimbi akifafanua jambo kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria walipotembelea Mradi wa Ujenzi wa jengo la Mahakama ya wilaya ya Longido mkoani Arusha jana.
 Mkuu wa Kitengo cha Usimamizi wa Majengo cha Mahakama ya Tanzania (HEM) Mhandisi Mohamed Kitunzi akifafanua jambo  kuhusu ujenzi kwa wajumbe wa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria walipotembelea Mradi wa Ujenzi wa jengo la Mahakama ya wilaya ya Longido mkoani Arusha jana.
 Jengo la Mahakama ya wilaya ya Longido mkoani Arusha likiwa katika hatua ya umaliziwaji.
 Jengo la Mahakama ya wilaya ya Longido mkoani Arusha likiwa katika hatua ya umaliziwaji.
  Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt. Augustine Mahiga (wa nne kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria walipotembelea mradi wa ujenzi wa jengo la Mahakama ya wilaya ya Longido mkoani Arusha jana. Wa nne kulia ni Naibu Katibu Mkuu wa wizara ya Katiba na Sheria Mhe. Amon Mpanju na wa tano kushoto ni Mwenyekiti wa  Kamati hiyo na Mbunge wa Rufiji Mhe. Mohamed Mchengelwa. 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni