Ijumaa, 15 Machi 2019

MAJAJI WASTAAFU WATANO WA MAHAKAMA KUU YA TANZANIA WAAGWA KITAALUMA


Na Mary Gwera & Dennis Buyekwa

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi, amesema Mahakama itaendelea kuwatumia Majaji wastaafu katika shughuli mbalimbali za Mahakama nchini.

Akizungumza na Vyombo vya habari mara baada ya hafla ya kuwaaga rasmi kitaaluma jumla ya Majaji watano wa Mahakama Kuu ya Tanzania iliyofanyika Machi 15 Mahakama Kuu Dar es Salaam, Mhe.Jaji Kiongozi alisema kuwa Mahakama inafanya kazi kwa karibu na Majaji wastaafu kwa kuwashirikisha katika  shughuli mbali mbali za mahakama ikiwa ni pamoja na  eneo la Mafunzo.

“Mahakama inafanya kazi kwa karibu na Majaji Wastaafu, tunashirikiana na katika masuala mbalimbali ikiwa ni pamoja na eneo la Mafunzo ambapo tunawatumia katika kutoa mada kutokana na uzoefu walio nao,” alieleza Mhe. Jaji Kiongozi. 

Katika hatua nyingine, Mhe. Jaji, Dkt. Feleshi alisema  kuwa mpaka sasa kuna jumla Majaji wastaafu sabini (70) , hivyo kwa kushirikiana na Majaji waliopo kazini, Mahakama inaendelea kuwatumia katika shughuli kadhaa kupitia Chama cha Majaji Wastaafu.

 Akizungumzia umuhimu wa hafla hiyo, Mhe.Jaji kiongozi amesema kuwa lengo kubwa la hafla hizi ni kuwakumbusha Wahe. Majaji waliobaki umuhimu wa wao kufanya kazi zao kwa uadilifu na ufanisi ili waweze kumaliza vizuri vipindi vyao vya uongozi kwa muda wote wa utumishi wao.

Majaji Wastaafu walioagwa katika hafla hiyo ni Mhe. Jaji Fredrica William Mgaya, Mhe. Jaji Aisha Charles Nyerere, Mhe. Jaji Rose Aggrey Temba, Mhe. Jaji Crecensia Makuru na Mhe. Jaji Salima Chikoyo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Majaji hao Wastaafu wamewaasa Watumishi wa Mahakama waliobaki kufanya kazi kwa uadilifu na kutimiza wajibu wao kwa mujibu wa sheria na taratibu zilizopo.

Naye, Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Bi. Fatma Karume aliishukuru Serikali kwa kutambua mchango wa wanawake katika sekta ya sheria huku akionesha furaha yake kwa Majaji hao wastaafu ambao wote ni wanawake.

“Nilipoanza kufanya kazi za Uwakili, miaka takribani 30 iliyopita, Sekta ya sheria ilikuwa inaendeshwa na idadi kubwa ya wanaume ukilinganisha na miaka ya hivi karibuni ambapo wanawake wamepewa nafasi katika sekta hii,” alisisitiza Bi. Karume.
Kabla ya kustaafu kwake Mhe. Jaji Mgaya alikuwa Jaji wa Mahakama Kuu Divisheni ya Ardhi, naye Mhe. Jaji Nyerere alikuwa Jaji Mfawidhi, Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi.

Mhe. Jaji Teemba alikuwa Jaji Mfawidhi, Mahakama Kuu, Kitengo cha Usuluhishi, Mhe. Jaji Makuru alikuwa Jaji wa Mahakama Kuu, Divisheni ya Ardhi naye Mhe. Jaji Chikoyo alikuwa Jaji wa Mahakama, Kitengo cha Usuluhishi.

Majaji wote wastaafu waliitumikia Mahakama na Taifa kwa ujumla katika nafasi mbalimbali za Kiutumishi.
 Pichani ni Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Jaji Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi akiwa katika hafla ya kuwaaga kitaaluma jumla ya Majaji watano wastaafu wa Mahakama hiyo, wa pili kushoto ni Jaji Mstaafu wa Mahakama Kuu-Divisheni ya Ardhi, Mhe. Fredrica Mgaya, wa kwanza kushoto ni Jaji Mstaafu wa Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi, Mhe. Aisha Nyerere na wa kwanza kulia ni Jaji Mstaafu wa Mahakama Kuu-Divisheni ya Kazi.

Jaji Mstaafu wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Jaji Aisha Nyerere akitoa hotuba yake katika hafla ya kuagwa rasmi kitaaluma, kulia ni Mhe. Jaji Mstaafu Fredrica Mgaya.


Pichani ni baadhi ya Majaji wastaafu wa Mahakama Kuu walioagwa kitaaluma, kushoto ni Mhe. Jaji Teemba na kulia ni Mhe. Jaji Mstaafu, Crencensia Makuru.

Jaji Mstaafu wa Mahakama Kuu, Kitengo cha Usuluhishi, Mhe. Salima Chikoyo (kushoto) akitoa hotuba yake katika hafla ya kuagwa kitaaluma jumla ya Majaji watano wa Mahakama Kuu ya Tanzania.
 Baadhi ya Viongozi na baadhi ya Watumishi Mahakama walioshiriki wakifuatilia hafla hiyo.
Baadhi ya Maafisa wa Mahakama pamoja na wageni waalikwa waliohudhuria katika hafla hiyo.
Wasajili wa Mahakama wakiwa katika hafla hiyo. 


Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Bi. Fatma Karume akizungumza wakati wa hafla hiyo.
Jaji Kiongozi, Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Wahe. Majaji Wastaafu walioagwa kitaaluma mapema Machi 15. Wa nne kushoto ni Jaji Mstaafu, Mhe. Fredrica Mgaya, wa tatu kushoto ni Jaji Mstaafu, Mhe. Jaji Aisha Nyerere, wa nne kulia ni Jaji Mstaafu, Mhe. Jaji Rose Teemba, wa tatu kulia ni Jaji Mstaafu, Mhe. Jaji Crencensia Makuru na wa pili kushoto ni Jaji Mstaafu, Mhe. Jaji Salima Chikoyo, wa kwanza kulia ni Jaji wa Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Jaji Dkt. Ngwalla na wa kwanza kushoto ni Kaimu Jaji Mfawidhi, Mahakama Kuu Divisheni ya Ardhi, Mhe. Joaquine De Mello na waliosimama ni baadhi ya Wahe. Majaji wa Mahakama Kuu walioshiriki katika hafla hiyo.
 Picha ya pamoja na Jaji Mstaafu wa Mahakama Kuu, Kanda ya Iringa, Mhe. Jaji Mary Shangali (aliyesimama) akiwa na Msajili Mkuu, Mahakama ya Tanzania, Mhe. Katarina Revocati.

Jaji Kiongozi, Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi (katikati) katika picha ya na Wahe. Majaji wastaafu pamoja na Manaibu Wasajili na Wakurugenzi wa Mahakama walioshiriki katika hafla hiyo.
 Baadhi ya Majaji na Manaibu Wasajili, Wanachama wa Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania wakiwapongeza wanachama wenzao mara baada ya kustaafu.
 Picha ya pamoja na baadhi ya Watumishi wa Mahakama ya Ardhi na Kazi.
(Picha na Mary Gwera, Mahakama)


 

 


 



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni