Alhamisi, 14 Machi 2019

WATUMISHI WA MAHAKAMA KUU KANDA YA MOSHI WAPATIWA MAFUNZO YA HUDUMA KWA WATEJA 'CUSTOMER CARE'

Na Paul Mushi, Mahakama Kuu-Moshi

Jumla ya watumishi wa Mahakama 36 kutoka katika wilaya ya Rombo, Hai, Siha, Mwanga, Same na Moshi wanapatiwa Mafunzo ya huduma kwa wateja, upatikanaji wa taarifa na maadili.

Mafunzo hayo ya siku tatu (3) yamefunguliwa rasmi leo Machi 14, 2019 na yamejumuisha kada mbalimbali ambao Mahakimu, Wasaidizi wa Kumbukumbu, Maafisa Utumishi/Tawala, Madereva, Walinzi, Wasaidizi wa Ofisi.

Akifungua mafunzo hayo, Kaimu Jaji Mfawidhi, Mahakama Kuu-Kanda ya Moshi, Mhe.Jaji Patricia Fikirini aliwahimiza washiriki wote kushiriki kikamilifu katika mafunzo hayo ili kupata matokeo chanya. 

“Nahimiza mshiriki ipasavyo mafunzo haya kikamilifu natazamia kupata na kuona mabadiliko haswa kupungua kwa malalamiko baada yamafunzo haya” alisema Mhe. Jaji Fikirini.

Aidha Mhe. Jaji Fikirini waliwashukuru Waandaaji wa mafunzo hayo ambao ni MISA TANZANIA, kwa ufadhili wa FES MEDIA AFRICA.

 “Napenda kuwashukuru waandaaji wa mafunzo haya kwani yamekuja kwa wakati muhafaka katika kipindi hichi muhimu  ambacho mahakama inapambana kuboresha huduma zetu,niseme asante sana na karibuni sana” alieleza.

Nae Mkurugenzi wa Taasisi ya habari kusini mwa jangwa la Sahara Afrika Tawi la Tanzania (MISA TANZANIA) ambaye pia ni mwezeshaji katika mafunzo hayo, Bw. Gasirigwa Sengiyumva alieleza kuwa katika kipindi hicho cha siku tatu (3) washiriki wataelimishwa  juu ya njia bora ya mawasiliano baina ya watumishi na wateja, umuhimu wa kupata taarifa na mtazamo wa kisheria (sheria ya habari ya mwaka 2016).

Aliongeza kuwa washiriki hao watafundishwa pia jinsi ya kutoa taarifa na kuomba taarifa, ujuzi na msingi wa kushughulikia malalamiko pamoja na kanuni za maadili kwa watumishi wa umma.

Lengo la Mafunzo kwa Watumishi wa Mahakama ni kuwawezesha kuwa sehemu ya maboresho ya huduma za Mahakama kwa kuwahudumia wateja ipasavyo.

Mafunzo hayo yanatolewa kwa ushirikiano wa Mahakama ya Tanzania na MISA TANZANIA Kwa ufadhili wa Shirika la Ujerumani ‘FRIEDISH EBERT STIFTUNG’ ( FES MEDIA AFRICA.

Awamu ya kwanza ya mafunzo haya yanayotazamiwa kukamilika Machi 16 yanafanyika katika Kanda ya Moshi na Kanda ya Iringa. 
 Kaimu Jaji Mfawidhi, Mahakama Kuu kanda ya Moshi, Mhe. Jaji Patricia Fikirini akifungua mafunzo hayo kwa Watumishi wa Mahakama Kanda ya Moshi.
 Baadhi ya washiriki katika mafunzo ya huduma kwa wateja wakiwa katika mafunzoni.
 Baadhi ya washiriki wakiwa katika majadiliano katika mafunzo hayo.
Kaimu Jaji Mfawidhi, Mahakama Kuu-Kanda ya Moshi, Mhe. Jaji Patricia Fikirini (aliyeketi katikati) akiwa katika picha ya pamoja Maafisa wa Mahakama ,wawezeshaji na washiriki katika mafunzo hayo.
 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni