Jumanne, 5 Machi 2019

MAHAKAMA YA HAKIMU MKAZI PWANI YAPATA MTENDAJI MPYA


Na Rashid Omar, Mahakama ya Hakimu Mkazi Pwani
Mahakama ya Hakimu Mkazi Pwani imepata Mtendaji mpya baada ya aliyekuwa Mtendaji wa Mahakama hiyo kuhamishiwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na hivyo nafasi yake kuchukuliwa na Bw. Moses Minga ambaye amehamia kituoni hapo akitokea mkoani Mwanza.

Akizungumza katika hafla fupi ya kumuaga aliyekuwa Mtendaji wa Mahakama  hiyo na kumkaribisha Mtendaji mpya iliyofanyika mwishoni mwa wiki katika Ukumbi wa Kiteshe mjini Kibaha, Bw. Minga alishukuru kwa kupewa mapokezi mazuri katika Mahakama hiyo ikiwa ni ishara nzuri ya ushirikiano mkubwa anaotarajia kupatiwa katika  utendaji kazi wake.

“Ninashukuru kwa kupewa mapokezi mazuri, jengo ni zuri, kitu kimoja cha msingi ni kuhakikisha tunatoa huduma bora kwa wananchi ” Alisema Bw. Minga.
Naye, aliyekuwa Mtendaji wa Mahakama hiyo, Bi. Athanasia Kabuyanja aliwasihi Watumishi wa Mahakama hiyo kumpa ushirikiano Mtendaji huyo mpya katika utekelezaji wa majukumu yake.

“Nawasihi pia mumpe ushirikiano mkubwa mtendaji mpya , lengo ni kulipeleka mbele gurudumu la Mahakama na hasa ikizingatiwa kuwa, Kibaha ndipo mpango mkakati wa maboresho ya huduma za Mahakama ulipozinduliwa ”  Alisisitiza Bi.Kabuyanja. 

Kwa upande wake, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Mhe. Joyce  Mkhoi alimpongeza Mtendaji anaeondoka kwa kuishi vyema na watumishi huku akimkaribisha Mtendaji mpya. 

 “Tunakushukuru sana Bi Kabuyanja kwa kuishi nawe vyema, umejitoa sana katika kuhakikisha shughuli za kimahakama zinakwenda mbele.  Mimi binafsi kuna mambo mengi mazuri nimejifunza kwako ” Aliongeza Mhe. Mkhoi.
 Mtendaji mpya wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Pwani, Bw. Moses Minga akizungumza katika hafla hiyo.
Nyuso za furaha: Pichani ni Mtendaji mpya wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Pwani, Bw. Minga, kushoto ni aliyekuwa Mtendaji wa Mahakama ya Hakimu Mkazi, Bi. Athanasia Kabuyanja.


Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Mhe. Joyce  Mkhoi akizungumza katika hafla hiyo.
 Wakifurahi kwa pamoja na baadhi ya waalikwa walioshiriki katika hafla hiyo.



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni