Na
Mary Gwera, Mahakama
Rais wa Taasisi ya
Kimataifa inayoshughulikia mabaki ya shughuli za Mahakama za Makosa ya Jinai ‘International
Residual Mechanism for Criminal Tribunals-IRMCT’, Mhe. Jaji. Carmel Agius amekutana
na Mhe. Jaji Mkuu wa Tanzania kwa lengo la kujitambulisha.
Rais huyo wa IRMCT,
Mhe. Jaji Argius aliteuliwa rasmi kushika wadhifa huo na Katibu Mkuu wa
Umoja wa Mataifa (UN) Januari 19 mwaka huu.
Katika mazungumzo yao
yaliyofanyika Machi 07, kwenye Ofisi ya Mhe. Jaji Mkuu, Mahakama ya Rufani
jijini Dar es Salaam, Rais huyo alimshukuru Mhe. Jaji Mkuu kwa kwa kukubali
ombi la yeye kukutana nae na vilevile alimpongeza kwa kazi kubwa ya kuondoa
mlundikano wa mashauri katika Mahakama ya Tanzania.
Jaji. Agius alimuelezea
Mhe. Jaji Mkuu jinsi Taasisi hiyo inayojishughulisha na Makosa ya jinai
inavyofanya kazi, ambapo ameishukuru Tanzania kwa ushirikiano ambao inaipatia
taasisi hiyo.
Kwa upande wake, Jaji
Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma alimueleza Rais huyo na ujumbe ulioambatana
nae juu ya ngazi za Mahakama ya Tanzania ambazo ni tano (5) na jinsi zinavyofanya
kazi.
“Mahakama ya Tanzania
imegawanyika katika ngazi mbalimbali, kuna Mahakama za Mwanzo zilizopo takribani
900, katika ngazi hii mashauri mengi hufunguliwa, aidha idadi ya Mahakama
zilizopo katika ngazi hii bado haitoshelezi hali inayoleta changamoto kwa
wananchi waliopo baadhi ya maeneo yasiyokuwa na Mahakama hizo, lengo ni kila
kata kuwa na Mahakama ya Mwanzo,” alieleza Mhe. Jaji Mkuu.
Mhe. Prof. Juma
aliendelea kuueleza ujumbe huo kuwa Mahakama imejiwekea muda maalum wa kesi
kusikilizwa hadi kumalizika katika kila ngazi ya Mahakama, ambapo Mahakama ya
Mwanzo kesi husikilizwa kwa muda wa miezi sita (6), Mahakama ya Wilaya na
Mkoa/Hakimu Mkazi mwaka mmoja (1), Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufani miaka
miwili (2).
Aidha; Mhe. Jaji Mkuu alizungumzia
mikakati iliyowekwa na Mahakama katika kushughulikia mlundikano wa mashauri mojawapo
ikiwa ni kukasimisha mamlaka ya nyongeza kwa baadhi ya Mahakimu ‘Magistrates
with extended jurisdiction’ inayowawezesha kusikiliza mashauri ya Mahakama Kuu ambayo
kwa kawaida husikilizwa na Majaji wa Mahakama Kuu.
Taasisi ya IRMCT yenye
Ofisi zake ‘The Hague’ nchini Uholanzi ina tawi pia Arusha nchini Tanzania
ambalo hushughulikia mabaki ya shughuli za iliyokuwa Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji
ya Kimbari ya Rwanda ‘ICTR’.
Jaji Mkuu wa Tanzania
Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akiwa na wageni wake kutoka Taasisi ya Kimataifa
inayoshughulikia Mabaki ya shughuli za Mahakama za Makosa ya Jinai
(International Residual Mechanism for Criminal Tribunals- IRMCT) Mhe. Jaji Carmel
Agius (kushoto) walipomtembelea ofisini kwake leo jijini Dar es Salaam.
Rais
wa Taasisi ya Kimataifa inayoshughulikia Mabaki ya shughuli za Mahakama za
Makosa ya Jinai (International Residual Mechanism for Criminal Tribunals-
IRMCT) Mhe. Jaji Carmel Agius akisoma kitabu cha Mpango Mkakati wa Miaka Mitano
wa Mahakama ya Tanzania alichokabidhiwa na Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof.
Ibrahim Hamis Juma.
Jaji
Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akiwa katika picha ya pamoja na
Rais wa Taasisi ya Kimataifa inayoshughulikia Mabaki ya shughuli za Mahakama za
Makosa ya Jinai (International Residual Mechanism for Criminal Tribunals- IRMCT)
Mhe. Jaji Carmel Agius (kushoto) alipofika ofisini kwa Jaji Mkuu kumtembelea
leo jijini Dar es salaam. Kulia ni Msajili wa Taasisi hiyo Mhe. Olufemi Elias.
(Picha na Lydia Churi, Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni