Jumatatu, 4 Machi 2019

RAIS MAGUFULI AMWAPISHA WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA


Na Lydia Churi-Mahakama
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amewaapisha mawaziri wapya wa Wizara ya Katiba na Sheria, Balozi Dkt. Augustine Mahiga na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba Kabudi na kuwataka kutekeleza wajibu wao mpya kwa kuzingatia viapo vya Maadili walivyoapa.

Rais Magufuli pia aliwaapisha Makamishna watano wa Jeshi la Polisi nchini pamoja na Balozi wa Tanzania nchini Zambia Mhe. Yahaya Simba ambao aliwateua hivi karibuni.

Akizungumza baada ya kuwaapisha Mawaziri hao pamoja na viongozi wengine, Rais Magufuli amewataka viongozi hao kufanya kazi kwa bidii, uadilifu na kwa ushirikiano ili kuijenga Tanzania.

Aidha, Rais Magufuli amewataka Makamishna walioapishwa leo na Makamishna wengine kurekebisha kasoro ndogo zilizopo kwenye jeshi hilo ikiwemo watumishi wachache wanaokiuka maadili ya kazi kwa kujihusisha na uhalifu ili kujenga taswira chanya ya jeshi hilo kwa watanzania.

“Ninalithamini jeshi la polisi nchini kwa kuwa linafanya kazi nzuri, jirekebisheni”, alisema. 

Rais Magufuli pia amewataka viongozi wa jeshi hilo kutowakatisha tamaa kwa kutowaunga mkono askri wa wanapotekeleza majukumu yao kwa usahihi kwani kwa kufanya hivyo watakuwa wakiwadhalilisha na kuwavunja moyo katika kazi yao.
Aidha, amewataka Majaji, Mawaziri, Makamishna wa Polisi, Makatibu wakuu pamoja na viongozi wengine wa serikali kutenda haki kwa watanzania na kuwataka viongozi hao kutanguliza mbele maslahi ya taifa  na kuhimiza umoja baina ya wananchi ili nchi ifanikiwe. 

Akizungumza kwenye hafla hiyo iliyofanyika leo Ikulu jijini Dar es salaam, Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe Prof. Ibrahimu Hamis Juma amewapongeza Mawaziri wa Katiba na Sheria na Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na kumwelezea Prof. Kabudi kuwa ni kiongozi aliyeifahamu vizuri Mahakama ya Tanzania na dhana yake ya kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi.

Jaji Mkuu aliitaja baadhi ya mikakati ya Mahakama ya Tanzania ya kusogeza huduma karibu zaidi na wananachi kuwa ni ujenzi wa majengo ya Mahakama katika ngazi zote, uanzishwaji wa Mahakama inayotembea (Mobile Court) pamoja na matumizi ya Tehama katika kurahisisha upatikanaji wa haki.

Prof. Juma ameahidi kushirikiana na Waziri Mahiga katika kutekeleza jukumu la msingi la Mahakama la kuhakikisha wananchi wanapata haki kwa wakati kwa kuwa atakuwa ni kiungo kati ya wananchi na mhimili wa Mahakama.
 Pichani ni Wahe. Mawaziri, Balozi pamoja na Makamishna wa Jeshi la Polisi walioteuliwa wakisubiri kuapishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli. Aliyeketi wa kwanza kulia ni Waziri mpya wa Wizara ya Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga, katikati ni Waziri mpya wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, kushoto ni Balozi mteule wa Tanzania nchini Zambia, Mhe. Balozi Yahya Simba na walioketi nyumba na baadhi ya Makamishna wa Polisi walioteuliwa.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akimuapisha Mhe. Dkt. Augustine Mahiga kuwa Waziri wa Katiba na Sheria, kabla ya uteuzi wake, Mhe. Dkt. Mahiga alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.


Mkono wa pongezi.
 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akimuapisha Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, kabla ya uteuzi huu, Mhe. Prof. Kabudi alikuwa Waziri wa Katiba na Sheria.
 Baadhi wa Viongozi walioshiriki katika hafla ya kuapishwa Wateule wapya, wa kwanza kulia ni Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Majaliwa Kassim Majaliwa, wa pili kushoto ni Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, wa pili kulia ni Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Job Ndugai na wa kwanza kushoto ni Katibu Mkuu Kiongozi, Mhe. Eng. John Kijazi.
 Rais wa Jamhuri  ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akimuapisha Mhe. Balozi Yahya Simba kuwa Balozi wa Tanzania nchini Zambia.

 Sehemu ya wageni mbalimbali walioshiriki katika hafla ya kuapishwa kwa Mawaziri, Balozi na Makamishna wa Polisi wateule. Sherehe ya kuapishwa imefanyika mapema Machi 04 katika Viwanja vya Ikulu jijini Dar es Salaam.

 Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Simon Sirro akimtunuku wadhifa mpya moja ya Makamishna wapya walioteuliwa na Mhe. Rais.
Kiapo cha maadili ya Utumishi wa umma.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akizungumza wakati wa hafla hiyo, ameahidi kutoa ushirikiano kwa Waziri mpya wa Katiba na Sheria katika utendaji kazi.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli  (katikati), Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (wa kwanza kushoto), Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Majaliwa Kassim Majaliwa (wa pili kushoto), Spika wa Bunge la Tanzania, Mhe. Job Ndugai (wa pili kulia) pamoja na Katibu Mkuu Kiongozi, Eng. John Kijazi wakiwa katika picha ya pamoja na Wahe. Mawaziri, Balozi na Makamishna wa Jeshi la Polisi walioapishwa mapema Machi 04, 2019.
 Mhe. Rais akiwa katika picha ya pamoja na Waziri wa Katiba na Sheria pamoja na baadhi ya Viongozi wa Sekta ya Sheria.
 Mhe. Rais akiwa katika picha ya pamoja na Wateule pamoja na baadhi ya Wahe. Majaji wa Mahakama ya Rufani na Mahakama Kuu ya Tanzania waliohudhuria katika hafla hiyo.

Kwa upande mwingine, naye Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi amemuapisha Kamishna wa Utawala na Menejimenti ya Rasilimali watu wa Jeshi la Polisi Tanzania, Kamishna Benedict Michael Wakulyamba kuwa Mjumbe wa Tume ya Utumishi wa Polisi, Uhamiaji na Magereza. Kamishna Wakulyamba anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Kamishna Albert Nyamuhanga ambaye ameteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Idara ya kuhudumia Wakimbizi.
 Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi akimuapisha Kamishna Benedict Michael Wakulyamba kuwa Mjumbe wa Tume ya Utumishi wa Polisi, Uhamiaji na Magereza.
 Kamishna  Wakulyamba akisaini hati ya kiapo mara baada ya kuapishwa rasmi. Kamishna huyo ameahidi kufanya kazi kwa weledi na kwa manufaa ya Watumishi wa Jeshi la Polisi na umma kwa ujumla.
Mhe. Jaji Kiongozi akisaini hati ya kiapo mara baada ya kumuapisha Kamishna Wakulyamba.
(Picha na Mary Gwera, Mahakama)

 
 


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni