Na
Ibrahim Mdachi, Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof.
Ibrahim Hamis Juma amefungua rasmi Mafunzo elekezi ya kwanza kufanyika kwa
Wahe. Majaji wapya wa Mahakama ya Rufani walioteuliwa na kuapishwa na Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli hivi karibuni.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo
elekezi ya wiki moja kwa Wahe. Majaji hao, Machi 11,mwaka huu Mhe. Jaji Mkuu alisema
kuwa, mafunzo endelevu kwa Majaji yana umuhimu wa kipekee na ni moja ya kigezo
cha msingi katika kuboresha utoaji wa haki.
Akinukuu maneno ya Marehemu Jaji J.K
Mathur aliyehudumu katika Mahakama Kuu ya Huko Calcutta chini India katika
andiko lake lenye kichwa cha habari kisemacho “Judicial Training: Some
Inceptive Considerations,” Mhe. Jaji Prof. Juma alisema kuwa, andiko hilo
huwakumbusha mambo makuu matatu katika mafunzo ya Maafisa wa Mahakama nayo ni
Maarifa, Ujuzi na Mtazamo.
“Mambo hayo yanatakiwa kuzingatiwa
katika utendaji kazi wa Majaji na Majaji wa Mahakama ya Rufani,” alieleza Mhe.
Jaji Mkuu.
Akinukuu maneno ya Jaji Mstaafu wa
Mahakama ya Rufani aliye hudumu katika Mahakama ya Rufaa ya Albert mwenye
uzoefu wa takribani miaka 27 katika Mahakama tatu tofauti nchini Canada Mhe. J.E.
Cote alisema kuwa “Jaji Mbaya si yule asiyefahamu Sheria bali ni yule asiye mdadisi wa mambo. Jaji wa
mahakama ya Rufaa hapaswi kuwa mdadisi pekee bali anapaswa pia kufahamu namna
ya kupitia kesi mbalimbali.”
Mkuu wa Chuo na Mratibu wa Mafunzo hayo
Mhe. Jaji. Dkt Paul F. Kihwelo akitoa maelezo ya utangulizi alisema kuwa, kama
Chuo wamefarijika kuona kuwa Majaji hao walioteuliwa na kuapishwa kuwa Majaji
wa Mahakama ya Rufaa, sita kati yao waliwahi kupata mafunzo elekezi hapa Chuoni
miaka kadhaa iliyopita.
Aliongeza jambo la kufurahisha zaidi ni kwamba aliyekuwa
Mkuu wa Chuo ambaye pia wakati huo alikuwa ndiye Mratibu wa Mafunzo hayo Mhe.
Jaji Fredinand Wambali ni miongoni mwa
washiriki wa mafunzo haya elekezi kama Jaji wa Mahakama ya Rufaa.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mafunzo
hayo Mhe. Jaji Mstaafu Harold Nsekela, akitoa neno la ukaribisho kwa washiriki
aliiasa Mahakama kuendelea kuendesha mafunzo
elekezi na endelevu ya Kimahakama kwa Majaji kama fursa ya kuendesha mijadala
na kujiimarisha zaidi katika taaluma ya Sheria, ubadilishanaji wa uzoefu na
kuboresha ufahamu kuhusu elimu ya sheria nchini.
Naye Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi wa Chuo Mhe. Jaji Dkt. Gerald Ndika akitoa neno la shukrani kwa hadhara hiyo, Mhe. Jaji Ndika alimshukuru Jaji Mkuu kwa busara zake na kukiamini Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto kuwa kina uwezo wa kuandaa, kufanya na kutoa mafunzo yenye ubora unahitajika kwa Majaji wa Mahakama ya Rufaa nchini. “Sina shaka kwamba hotuba hiyo imetutia hamasa na imetuweka katika hatu nzuri ya kuandaa na kuendesha mafunzo elekezi”
Pia aliishukuru zaidi Menejimenti ya Chuo kwa kufikiria kwa mapana zaidi “out of the box” kwa kuandaa programu ya siku tatu kwa Madereva kumi na watano waliombatana na Majaji wa Mahakama ya Rufaa. Programu hii kwa upande mwingine ubunifu wa shughuli zitakazoweza kuisaidia Mahakama kutumia vyema rasilimali watu na rasilimali fedha zinazotengwa kwa Mafunzo elekezi
Ikumbukwe kuwa Mafunzo haya elekezi kwa
Majaji wa Mahakama ya Rufaa yanafanyika kwa mara ya kwanza na Mahakama ya Tanzania
kwa kushirikiana na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto. Sambamba na Jaji Mkuu
kuwa Mgeni rasmi wa ufunguzi wa Mafunzo hayo vilevile alikuwa ni miongoni mwa
wawezeshaji wa mafunzo hayo.
Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto
kinawatakia kila lakheri Majaji hawa wanapoanza safari hii ya kihistoria ya
kazi yako kama Majaji wa mahakama ya Rufaa. Nchi inatarajia utendaji kazi wa
mfano wa kuigwa kutoka kwao.
Jaji Mkuu wa
Tanzania,Mhe. Profesa Ibrahim Juma akitoa hotuba ya kufungua mafunzo elekezi
kwa majaji wapya wa Mahakama ya Rufaa
yaliyofanyika katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto(IJA).
|
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni