Jumatano, 13 Machi 2019

WATUMISHI WA MAHAKAMA KUU KANDA YA IRINGA WAANZISHA UTARATIBU WA KUFANYA MAZOEZI


Na Lusako  Mwang’onda- Mahakama Kuu-IRINGA

Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Iringa, Mhe.Panterine Kente amewasisitiza watumishi wa Mahakama hiyo kuwa na utaratibu wa kufanya mazoezi kwa ajili ya kuziweka sawa afya zao.

Amewataka watumishi hao wa Mahakama kuwa mazoezi ni muhimu  kufanya mazoezi ili kuuweka mwili sawa na kujenga kinga ya mwili dhidi ya magonjwa mbalimbali madogomadogo na hata makubwa.

Watumishi wa Mahakama kanda ya Iringa tangu mwezi uliopita wametenga siku tatu kwa juma (Jumatatu, Jumatano na Ijumaa) kwa ajili ya kufanya mazoezi.

Mazoezi hayo hufanyika jioni kuanzia saa 9:30 baada ya muda wa kazi kwa siku hizo tatu nilizozitaja. Kwasasa mazoezi yanayofanywa ni yale ya kutembea na kukimbia huku juhudi za makusudi zikiwa zinafanywa ili kutenga ukumbi maalumu kwa ajili ya mazoezi mengine ya viungo.

Akizungumza na watumishi wa Mahakama mwishoni mwa wiki iliyopita kwenye viwanja vya Mahakama Kuu Kanda ya Iringa wakati wakiwa wanajiandaa kuingia barabarani kufanya zoezi la kukimbia, Mhe. Kente aliainisha faida za mazoezi kwa binadamu. Jaji Kente alisema ili kujenga mwili na afya njema inahitajika kutumia angalau dakika 150 kwa wiki kufanya mzoezi mepesi yajulikanayo kitaalamu kama “Aecrobics” ili kujiimarisha kiafya.

Jaji Kente amezitaja faida  nyingine za mazoezi kuwa ni pamoja na; kupunguza hatari ya kupata magonjwa yasiyoambukiza ikiwamo magonjwa ya moyo, kiharusi, saratani na kisukari. Pia ameongeza kuwa mazoezi yanadhibiti unene uliokithiri ambao ni kihatarishi cha kupata magonjwa mbalimbali. Pia Kente amesema mazoezi yanachangia kupata usingizi mnono.

Mhe. Kente alisema “au kuna yeyote kati yetu asiyejua faida za usingizi? Usingizi una faida nyingi mwilini ikiwa ni pamoja na kusahihisha hitilafu za mwili na kuujenga mwili ili kuwa katika ubora unaotakiwa”.

Utaratibu huu wa mazoezi kwa watumishi wa Mahakama Kanda ya Iringa ni endelevu, na utakuwa unafanyika baada ya muda wa kazi watumishi hujumuika pamoja kufanya mazoezi.
Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Iringa Mhe.Panterine Kente akiwa tayari kwa ajili ya mazoezi. 
Baadhi ya mahakimu wakiwa tayari kwa ajili ya mazoezi.
Baadhi ya watumishi wa Mahakama Kuu Kanda ya Iringa wakiwa katika mazoezi.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni