Na
Mary Gwera, Mahakama –Mbeya
Jaji Kiongozi, Mahakama
Kuu ya Tanzania, Mhe. Jaji Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi amehitimisha ziara yake
ya kikazi katika Mahakama Kanda ya Mbeya huku akitoa wito kwa Uongozi wa Kanda
hiyo kutoruhusu mlundikano wa mashauri.
Akizungumza na Viongozi
na baadhi ya Maafisa wa Mahakama katika kikao chake cha majumuisho ya ziara
yake kilichofanyika Aprili 10, 2019 katika Ukumbi wa mikutano wa Mahakama
Kuu-Mbeya, Mhe. Jaji Dkt. Feleshi aliwaelekeza Viongozi hao kuainisha mashauri
yote yenye umri wa miaka mine (4) lengo likiwa ni kutoruhusu mashauri hayo
kuvuka miaka mitano (5).
“Nimeridhika na suala
la usikilizwaji na umalizwaji wa mashauri katika Kanda hii kupitia taarifa
mbalimbali zilizotolewa, hivyo ni rai yangu kuwa mashauri yote yaliyo na umri
kuanzia miaka mitatu na minne (4) yaainishwe na kufanyiwa kazi kabla
hayajafikia umri wa miaka mitano (5) Mahakamani,” alieleza Mhe. Jaji Kiongozi.
Mhe. Jaji Kiongozi
alisema kuwa lengo la Mahakama ya Tanzania ni kutokuwa na mashauri yanayokaa
kwa muda mrefu kuanzia miaka mitano (5) na kuendelea huku akisema kuwa nia
iliyopo mashauri yasikae zaidi ya miaka miwili (2) Mahakamani kabla ya
kumalizika.
Mbali na agizo hilo,
Mhe. Jaji Kiongozi aliwasisitiza Wahe. Majaji, Wasajili, pamoja na Mahakimu
kuheshimu nyaraka mbalimbali zinazotolewa na Viongozi wa Mhimili huo kwa ustawi
bora wa uondoshwaji wa mashauri.
Aidha; Mhe. Jaji
Kiongozi alionyesha kufurahishwa kwake na juhudi za Majaji na Mahakimu
wanaochapa nakala zao za hukumu na kuwapatia Wadaawa kwa wakati.
“Katika Kanda hii nimefurahishwa
na jitihada za baadhi ya Mahakimu wanaochapa nakala zao za hukumu, hivyo nitoe
wito kwa Majaji na Mahakimu ambao hawajaanza kuiga mfano huu ili kutopelekea
ucheleweshaji wa upatikanaji wa nakala za hukumu na mienendo ya mashauri,”
alieleza Mhe. Jaji Kiongozi.
Kwa upande mwingine, Mhe. Jaji
Dkt. Feleshi aliagiza Mahakama katika Kanda hiyo kuhamasisha wanafunzi katika
shule za Sekondari kusoma masomo ya sheria ili kuwajengea upendo wa fani ya
uanasheria/uhakimu.
Kabla ya kuhitimisha
rasmi ziara yake katika Kanda hiyo, Mhe. Jaji Kiongozi alitembelea na kupata
taarifa za utendaji za Mahakama ya Watoto, Mahakama ya Mwanzo Uyole, Mahakama
ya Hakimu Mkazi na Wilaya Mbeya ambapo sehemu zote Mhe. Jaji Kiongozi
alionyesha kuridhishwa na kasi ya uondoshaji wa mashauri na kusisitiza
kuendelea na kasi hiyo.
Mhe. Jaji Kiongozi
amefanya ziara ya kikazi katika Mahakama Kanda ya Iringa na Mbeya lengo likiwa
ni kujua hali ya maendeleo ya
utekelezaji wa maboresho ya huduma mbalimbali za Mahakama na vilevile kuwakumbusha Watumishi
wa Mhimili huu kuendelea kutekeleza jukumu la msingi la utoaji haki nchini kwa
ubora wa hali ya juu kwa manufaa ya wananchi.
Jaji Kiongozi, Mahakama
Kuu ya Tanzania, Mhe. Jaji Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi (aliyesimama) akizungumza
na Wahe. Majaji wa Mahakama Kanda ya Mbeya (pichani) pamoja na baadhi ya
Viongozi na Maafisa wa Kanda hiyo (hawapo pichani) alipokuwa katika kikao cha
Majumuisho ya ziara yake katika Kanda hiyo. Wa tatu kushoto ni Jaji Mfawidhi,
Mahakama Kuu-Kanda ya Mbeya, Mhe. Jaji Robert Makaramba, wa kwanza kushoto ni
Jaji wa Mahakama Kuu, Kanda ya Mbeya, Mhe. Jaji Dunstan Ndunguru na wa pili
kushoto ni Jaji wa Mahakama Kuu, Kanda ya Mbeya, Mhe. Jaji Dkt. Lilian Mihayo
Mongella.
Mazungumzo yakiendelea.
Jaji Kiongozi, Mahakama
Kuu ya Tanzania, Mhe. Jaji Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi (wa tano kushoto) akiwa
katika picha ya pamoja na Wahe. Majaji pamoja na Maafisa wa Mahakama Kanda ya
Mbeya na baadhi ya Maafisa alioambatana nao katika ziara yake ya kikazi.
Mhe. Jaji Kiongozi
akitoa maelekezo alipokagua masjala katika jengo la Mahakama Kuu-Mbeya.
Ukaguzi wa rejesta ya
Mahakama.
Wateja waliofika kupata
huduma ya Mahakama Kanda ya Mbeya wakimsikiliza Mhe. Jaji Kiongozi (hayupo pichani)
alipokuwa akizungumza nao, amewasihi wananchi kuendelea kuwa na imani na
Mahakama kwani ipo kwa ajili ya kuhudumia wananchi.
Mhe. Jaji Dkt. Feleshi
(katikati) akizungumza na wateja wa Mahakama (hawapo pichani), kulia ni Jaji
Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Mbeya, Mhe. Jaji Robert Makaramba na kushoto
ni Mtendaji wa Mahakama Kuu, Kanda ya Mbeya, Bw. Moses Mwidete.
Mhe. Jaji Kiongozi (katikati)
akiwa katika picha ya pamoja na sehemu ya Watumishi wa Mahakama ya Watoto
iliyopo mkoani Mbeya na Maafisa wengine wa Mahakama Makao Makuu na Mahakama Kuu
Kanda ya Mbeya, wa tatu kulia ni Kaimu Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama hiyo,
Mhe. Zawadi Laiser.
Hakimu Mkazi Mfawidhi,
Mahakama ya Mwanzo Uyole, Mhe. Zawald Nyekelela akimkabidhi Mhe. Jaji Kiongozi
taarifa ya hali ya Utendaji wa Mahakama hiyo pindi Mhe. Jaji Dkt. Feleshi
alipotembelea katika Mahakama hiyo.
(Picha na Mary Gwera,
Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni