Jumatano, 10 Aprili 2019

VIONGOZI WA MAHAKAMA WATAKIWA KUIBUA WATUMISHI WANAOFANYA VIZURI


Na Mary Gwera na Rajabu Singana, Mahakama-Mbeya

Viongozi wa Mahakama, Kanda ya Mbeya wametakiwa  kuwatambua watumishi wanaofanya kazi kwa kujituma na kwa weledi na kutoa taarifa kwa mamlaka za juu za Mahakama ili watumishi hao waweze kuteuliwa katika nafasi za juu kwa ustawi wa Mahakama.

Akizungumza na Watumishi wa Mahakama Kanda ya Mbeya kwa nyakati tofauti, Aprili 09, 2019 Jaji Kiongozi, Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Jaji Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi aliyepo ziarani katika Kanda hiyo alisema jukumu la Watendaji ni pamoja na kuwaibua Watumishi wanaofanya vizuri.

Mhe. Jaji Kiongozi alisema kuwa jukumu la viongozi ni kuibua Watendaji wazuri katika kila eneo na endapo mtumishi anabainika kutekeleza majukumu yake kwa weledi ni vyema uongozi ukatambua na kutoa taarifa ili kuteuliwa katika nafasi za juu.

“Endapo mtumishi anabainika kutekeleza majukumu yake kwa weledi ni vyema uongozi ukatambua na kutoa taarifa ili kuteuliwa katika nafasi za juu, hivyo nawasihi Watumishi kila mmoja kwa nafasi yake kutimiza majukumu yake kwa weledi bila chuki, fitina na majungu,” alieleza Mhe. Jaji Dkt. Feleshi.

Aidha Mhe. Jaji Kiongozi aliwataka watumishi kuwa wabunifu, kujipa thamani, kujitambua wao wenyewe na kutambua umuhimu wao kwa Mahakama ya Tanzania.
 
Hata hivyo;  Mhe. Jaji Kiongozi amewapongeza watumishi wa Mahakama Kanda ya Mbeya kwa kazi kubwa wanayoifanya na kuwataka kuendelea kufanya kazi kwa bidii.

Sambamba na hilo, Mhe. Jaji Kiongozi aliwasisitiza kushirikiana katika utendaji kazi ili kuboresha huduma zitolewazo na Mahakama na kusaidiana katika kutatua changamoto mbalimbali za kiutumishi kwa manufaa ya wananchi. 

“Mfano ushirikiano unavyoweza kuwa ni pale inapotokea kituo kimoja kimezidiwa mashauri hivyo kuhitaji nguvu kutoka kituo kingine kwenda kupunguza na hata kumaliza mzigo wa kazi katika kituo husika,” alisisitiza Mhe. Jaji Kiongozi. 

Kwa upande mwingine, Mhe. Jaji Dkt. Feleshi aliwataka Mahakimu wenye uwezo wa kutumia kompyuta watumie ujuzi huo kuchapa mienendo na hukumu ili kuweza kuongeza kasi ya utoaji wa nakala za hukumu badala ya kutegemea Makarani ambao idadi yao haitoshelezi.

Akiwa katika jengo la Mahakama Kuu Mbeya Mhe. Feleshi aliwataka viongozi pamoja na watumishi kuendelea kuitunza miundombinu ya kisasa iliyofungwa katika jengo hilo. 

Awali akiwasilisha taarifa ya utendaji kazi wa Mahakama Kanda ya Mbeya, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda hiyo,  Mhe. Jaji Robert Makaramba alisema kuwa amefanikiwa kufanya ukaguzi wa Mahakama zote katika Kanda hiyo isipokuwa moja na inaendelea kufanya vizuri katika suala la uondoshaji wa mashauri. 

Katika kudumisha ushirikiano kati ya Mahakama na Serikali, katika siku ya kwanza ya ziara yake mkoani humo, kwa nyakati tofauti Mhe. Jaji Kiongozi alitembelea Ofisi ya Mkuu wa Mkoa Mbeya pamoja na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Rungwe na kuwataka Viongozi hao kwa nafasi zao kuendeleza ushirikiano.

Katika mazungumzo na Viongozi hao wa mkoani Mbeya, Mhe. Jaji Kiongozi aliwataka pia kuendelea kuwaelimisha Wananchi juu ya mipaka ya kiutendaji kazi kati ya Serikali na Mahakama ili wanapokuwa na jambo linalotakiwa kutatuliwa na Mahakama waweze kufika mahakamani bila kuchelewa.

“Naomba pia muwahimize Wapelelezi kukamilisha kwa haraka upelelezi wa kesi mbalimbali ili Mahakama iweze kuondosha mashauri kwa wakati, nakumbusha pia kutumia Kamati za Maadili ya Mahakimu za Mkoa na Wilaya ili kupata taarifa za Mahakimu wanaojihusisha na Vitendo vya utovu wa maadili ili hatua stahiki zichukuliwe na Mahakama,” alieleza Mhe. Jaji Dkt. Feleshi.

Katika siku ya kwanza ya ziara yake katika Kanda hiyo mbali na kuzungumza na Watumishi Mhe. Jaji Kiongozi alifanya pia ukaguzi katika miradi ya ujenzi wa Mahakama ya Wilaya Rungwe pamoja na Mahakama ya Mwanzo Uyole ambayo miradi yote inatarajiwa kukamilika ndani ya mwaka huu.
 Jaji Mfawidhi, Mahakama Kuu-Kanda ya Mbeya, Mhe. Jaji Robert Makaramba akiwasilisha taarifa ya hali utendaji kazi wa Mahakama katika Kanda hiyo mbele ya Mhe. Jaji Kiongozi aliyepo ziarani katika Kanda hiyo.
Wahe. Majaji wa Mahakama Kuu Mbeya, Maafisa wa Mahakama Kuu Mbeya pamoja na Maafisa walioambatana na Mhe. Jaji Kiongozi wakimsikiliza Mhe. Jaji Mfawidhi alipokuwa akiwasilisha taarifa yake kwa Mhe. Jaji Kiongozi.
 Mhe. Jaji Mfawidhi (kushoto) akimuonesha  Mhe. Jaji Kiongozi (wa pili kushoto) sehemu ya jengo la Mahakama Kuu Mbeya alipowasili katika jengo hilo la kisasa.
 Jaji Kiongozi, Mahakama Kuu ya Tanzania pamoja na viongozi aliombatana nao akisalimiana na Watumishi wa Mahakama ya Wilaya Rungwe alipowasili katika Mahakama hiyo.
 Mhe. Jaji Kiongozi (wa tatu kulia) akikagua mradi wa ujenzi wa  jengo la Mahakama ya Wilaya Rungwe lililopo katika hatua za mwisho za uwekaji wa msingi, kwa mujibu wa Mkandarasi jengo hilo linatarajiwa kukamilika mwezi Julai, 2019.
 Jaji Mfawidhi, Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya, Mhe. Jaji Robert Makaramba (wa tatu kulia) akimueleza jambo Mhe. Jaji Kiongozi alipokuwa akikagua mradi wa ujenzi wa Mahakama ya Wilaya Rungwe. Mwenye suti ya kijivu ni Mkuu wa Wilaya ya Rungwe, Mhe. Julius Chalya.

Mhe. Jaji Kiongozi akiwa katika picha ya pamoja na Mahakimu na Watumishi wengine wa Mahakama ya Wilaya Rungwe.
 Ukaguzi wa jengo la Mahakama ya Mwanzo Uyole, kwa mujibu wa Mkandarasi mradi huo upo katika hatua za mwisho na unatarajiwa kumalizika mwisho wa mwezi Aprili taratibu zilizobaki zikienda sawa.

Sehemu ya muonekano wa jengo la Mahakama ya Mwanzo Uyole lililopo katika hatua za mwisho za ujenzi.
 Watumishi wa Mahakama Kanda ya Mbeya wakimsikiliza Mhe. Jaji Kiongozi (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza nao.
 Mhe. Jaji Kiongozi akizungumza na Watumishi. Walioketi kushoto kwa Mhe. Jaji Kiongozi ni Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya, Mhe. Jaji Robert Makaramba, anayefuatia ni Jaji wa Mahakama Kuu, Mhe. Jaji Dunstan Ndunguru, anayefuata ni Jaji wa Mahakama Kuu, Kanda ya Mbeya, Mhe. Jaji Dkt. Lilian Mihayo Mongella, aliyeketi kushoto ni Naibu Msajili Mwandamizi, Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Messeka Chaba, walioketi upande wa kulia, kulia ni Msajili, Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya, Mhe. George Herbert, kushoto ni Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya, Bw. Moses Mwidete.
 Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Mhe. Albert Chalamila (kushoto) akiwa na Mhe. Jaji Dkt. Feleshi pindi Mhe. Jaji Kiongozi alipotembelea Ofisi ya Mkuu huyo wa Mkoa. Walioambatana na Mhe. Jaji Kiongozi ( nyuma kushoto) ni Jaji Mfawidhi, Mahakama Kuu, Kanda ya Mbeya, Mhe. Jaji Robert Makaramba na kulia ni Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Mbeya, Bw. Moses Mwidete.

(Na Mary Gwera, Mahakama-Mbeya)




 



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni