Ijumaa, 12 Aprili 2019

WATUMISHI WA MAHAKAMA KANDA YA IRINGA WAPATIWA MAFUNZO YA NAMNA YA KUHUDUMIA WATEJA


Na Lusako P. Mwang’onda, Mahakama Kuu Iringa

Watumishi wa Mahakama Kuu Kanda ya Iringa wameshiriki mafunzo ya namna ya kuhudumia wateja yaliyoratibiwa na Taasisi ya habari Kusini mwa Jangwa la Sahara Afrika Tawi la Tanzania (MISA –TAN) kwa kushirikiana na Mahakama ya Tanzania.

Mafunzo hayo yaliyofanyika katika Hoteli ya ‘Gentle-hills’ yalianza rasmi  Aprili 08, 2019 na kuhitimishwa Aprili 11, 2019 yalifungwa  na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Iringa,  Mhe. Jaji Panterine Kente ambapo aliwashukuru waratibu na wawezeshaji wa mafunzo hayo kwa kutoa mafunzo kwa watumishi wa Kanda hiyo.

“Kwa niaba ya Mahakama Kuu Kanda ya Iringa na labda niongeze kuwa na kwa niaba ya Mahakama ya Tanzania kwa ujumla wake, ninawashukuru sana waratibu wa mafunzo haya kwa kuona umuhimu wa kuwakumbusha watumishi wetu kuhusu masuala mbalimbali mliyofundisha na hasa kwenye hili la namna ya kuwahudumia wateja wetu, tunawashukuru sana” alisema Mhe. Jaji Kente.

Naye Mwenyekiti wa MISA-TAN Bi. Salome Kitomari aliwashukuru watumishi wa mahakama kwa kuyapokea mafunzo hayo kwa sura chanya, na kuahidi kuyaendeleza mafunzo hayo .kama tutaweza tena kupata rasilimali za kuweza kuyaendeleza basi tutafanya hivyo”.

“Tunaushuru sana uongozi wa Mahakama ya Tanzania kwa kuukubali mpango wa mafunzo hayo, na kama rasilimali zitaruhusu basi mafunzo hayo yatakuwa endelevu,” alisema Mwenyekiti huyo.

Nao washiriki wa mafunzo hayo wamesema wanashukuru kwa mafunzo waliyoyapata na kuahidi kwenda kuyatumia katika maeneo yao ya kazi.
Akizungumza kwa niaba ya washiriki wenzake, Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo ya Kalenga, Mhe. Magdalena Malaba alisema “tunawashukuru wawezeshaji wa mafunzo haya kwa kutukumbusha wajibu wetu wa kuwahudumia vizuri wateja wetu, na tunawaahidi kuwa haya tuliyojifunza kwa siku tatu tunakwenda kuyaishi vituoni kwetu”.

Mafunzo haya yameshirikisha watumishi wa kada mbalimbali kutoka  Mahakama Kanda ya Iringa.
Pamoja na maboresho mbalimbali yanayoendelea ndani ya Mahakama ya Tanzania, Mafunzo kwa watumishi ni moja ya vipaumbele vya Taasisi ili kufikiwa kwa malengo yaliyokusudiwa. 
 Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Iringa,  Mhe. Jaji Panterine Kente akizungumza wakati wa kufunga mafunzo ya utoaji wa huduma kwa mteja ‘Customer care’.
 Sehemu ya Washiriki wa mafunzo wakimsikiliza kwa makini Mhe. Jaji Kente akizungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo.
Mhe. Jaji Mfawidhi (Katikati) katika picha ya pamoja na Washiriki wa Mafunzo na Waratibu wa Mafunzo hayo kutoka MISA-TAN (walioketi pamoja na Mhe. Jaji Kente). Kulia ni Mwenyekiti wa MISA-TAN, Bi. Salome Kitomari na kushoto ni  Bw. Balile, Afisa kutoka MISA-TAN.



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni