Na
Francisca Swai, Mahakama ya Hakimu Mkazi Musoma
Katika kutekeleza agizo
la Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan la
kuhifadhi mazingira, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya Musoma, Mhe. John
Kahyoza, pamoja na Viongozi wa Serikali- mkoani Mara wameshiriki kupanda jumla
ya miche 564 ya miti katika eneo la Mahakama Kuu Musoma.
Viongozi hao wamepanda
miti ikiwa ni uzinduzi wa kampeni ya upandaji miti katika wilaya ya Musoma
inayosimamaiwa na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Ofisi ya Mkurugenzi pamoja
na Ofisi ya Idara ya Misitu.
Akizungumza na viongozi
mbalimbali walioshiriki katika zoezi hilo Aprili 12, 2019, Mhe. Jaji Kahyoza
alisema kuna umuhimu mkubwa na faida nyingi katika utunzaji wa mazingira hasa
kwa kupanda miti mfano kupata hewa safi, mvua za kutosha, kivuli, kutumika kama
mipaka n.k.
Mhe. Jaji Mfawidhi huyo
aliwaasa washiriki kujali mazingira ya sehemu wanazofanyia kazi na kuahidi kuwa
miti hiyo iliyopandwa itatunzwa na
kulindwa ipasavyo kwa kushirikiana na uongozi na wananchi wa eneo la Bweri
ambako ndiko Mahakama ilipo.
Kwa upande wake Mkuu wa
wilaya ya Musoma, Bw. Vicent Naano alimshukuru Mh. Jaji Kahyoza kwa kukubali
kuhudhuria uzinduzi huo katika eneo lake la Mahakama na kuongeza kuwa miti
ipo mingi na inagawiwa bure na hii ni awamu ya pili ya upandaji miti, ambapo
awamu ya kwanza miche 500,000 ilipandwa.
“Natoa wito kwa mamlaka
zote pamoja na watendaji wote wa Kata, Wenyeviti wa mitaa kuhakikisha miti inapandwa
angalau kwa kila kaya mbele ya nyumba zao, katika kampeni hii kauli mbiu ni “Misitu
ni mali, ni uhai, panda miti kwa maendeleo yetu” alisema Mkuu huyo wa Wilaya.
Naye Katibu Tawala wa
Wilaya ya Musoma, Bw. Justine Manko alisema zoezi la upandaji miti ni agizo la Mhe.
Makamu wa Rais, na wao kama Wilaya wanakusudia kupanda miti mingi katika
manispaa ya Musoma na wilaya kwa ujumla kwani licha ya kuwa ni agizo pia ni
faida kwa kwa vizazi vijavyo.
Afisa Misitu, Bw. Anderson
Mbaga alisema hadi sasa kuna miche 10,000,000 ambayo inatazamiwa kupandwa
maeneo mbalimbali lakini hasa katika Taasisi, mabonde, barabara, n.k na kuwa
hadi ifikapo 2025 maeneo yote katika mji wa Musoma yawe kijani.
Jaji Mfawidhi, Mahakama
Kuu-Kanda ya Musoma, Mhe. John Kahyoza akimwagilia mti alioupanda katika
uzinduzi wa kampeni ya upandaji miti uliofanyika katika eneo la Mahakama kuu
Musoma.
Mkuu wa wilaya ya
Musoma, Bw. Vicent Naano akipanda mti.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni