Na
Lydia Churi na Dennis Buyekwa-Mahakama
Jaji
Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amesema kuwa uelewa wa sheria,
ujuzi na tabia ni mambo matatu muhimu wanayotakiwa kuwa nayo Majaji wa Mahakama
ya Rufani ili yaweze kuwasaidia katika kutoa maamuzi kwenye mashauri.
Akifungua
Mkutano wa mwaka wa Majaji wa Mahakama ya Rufani wa kutathmini utendaji kazi wa
Mahakama hiyo wa mwaka 2018 na kuweka mikakati ya kazi kwa mwaka 2019, Jaji
Mkuu alisema Majaji kuwa na uelewa wa sheria na ujuzi haitoshi
pasipo kujenga tabia ya kufanya kazi kwa kasi na kwa weledi.
“Uvivu,
uchonganishi, kulalamika pamoja na ubishi usio na mwelekeo ni tabia za kibinadamu
zinazoweza kuathiri utendaji kazi kwa kuchelewesha upatikanaji wa haki”,
alisema Jaji Mkuu.
Alisema
Majaji wanao umuhimu wa kipekee katika jamii hivyo hawana budi kutoa haki kwa
kufuata sheria ili wananchi waweze kuwa na imani na mfumo wa utoaji haki pamoja
na utawala wa sheria.
“Kupitia
mkutano huu mtapata fursa ya kubadilishana uzoefu wa namna ya kumaliza mashauri
kwa kasi kwani utoaji haki uko katika utamaduni ambao haujaandikwa popote hivyo
naamini mtaibua tamaduni zitakazorahisha utoaji wa haki”.
Akizungumzia
ongezeko la idadi ya Majaji wa Mahakama ya Rufani, Jaji Mkuu alisema kuongezeka
kwa Majaji hao kutasaidia Mahakama kupunguza changamoto ya mlundikano wa
mashauri ya muda mrefu yaliyopo Mahakamani. Hivi sasa kuna Majaji 21 wa
Mahakama ya Rufani ambapo awali kulikuwa na Majaji 15.
Kuhusu
changamoto, Jaji Mkuu alisema Mahakama inakabiliwa na upungufu wa bajeti kwa
ajili ya vikao vya kusikiliza mashauri. Alisema endapo kungekuwa na bajeti ya
kutosha vikao vingi Zaidi vya mashauri vingefanyika na kumaliza mlundikano wa
mashauri ya muda mrefu.
Alisema
sheria imerekebishwa na kuwapa mamlaka Mahakimu na Manaibu Wasajili kusikiliza mashauri
ya Mahakama Kuu hususan yale yanayohusu migogoro ya Ardhi ambapo hatua hii
itasaidia kupunguza mashauri mahakamani. Aliongeza kuwa ili Mahakama iweze
kuwatumia inahitaji kuongezewa bajeti Zaidi ya iliyopo sasa.
Mkutano
wa Mwaka huu wa Majaji wa Mahakama ya Rufani pia umewashirikisha Manaibu
Wasajili, wasaidizi wa kisheria wa Majaji, Makarani na watunza kumbukumbu ili waweze
kusaidiana na Majaji kupanga mikakati ya kumaliza mashauri kwa wakati.
Jaji
Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akifungua Mkutano wa Majaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania wa kutathmini utendaji kazi wa Mahakama hiyo katika mwaka 2018 na kupanga mikakati ya kazi ya mwaka 2019 unaofanyika katika ukumbi wa Mwalim Julius Nyerere jijini Dar es salaam
Majaji
wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania wakiwa kwenye Mkutano wao wa kutathmini Utendaji Kazi wa
Mahakama hiyo katika mwaka 2018 na kupanga mikakati ya kazi ya mwaka
2019 unaofanyika katika ukumbi wa Mwalim Julius Nyerere jijini Dar es
salaam. Kulia ni Mhe. Jaji Shaaban Lila na kushoto ni Mhe. Jaji Rehema Mkuye.
Jaji
Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akiwa katika picha ya pamoja na Majaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania mara baada ya kufungua mkutano wao wa kutathmini utendaji kazi wa
Mahakama hiyo katika mwaka 2018 na kupanga mikakati ya kazi ya mwaka
2019 unaofanyika katika ukumbi wa Mwalim Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.
Jaji
Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma pamoja na Majaji wastaafu wakiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa Mahakama ya Tanzania wakiwemo Manaibu wasajili. Wa kwanza kushoto waliosimama ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) Mhe. Jaji Dkt. Paul Kihwelo na wa nne kutoka kushoto ni Mtendaji wa Mahakama ya Rufani Bwn. Solanus Nyimbi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni