Na
Mary Gwera, Mahakama
JAJI Mkuu wa Tanzania,
Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewataka Manaibu Wasajili wa Mahakama Kuu nchini na wote
wanaoshughulika na uandaaji wa kumbukumbu za rufaa kuzingatia sheria na kanuni muhimu katika uandaaji wa nyaraka hizo ili kuondoa mapungufu yanayoweza kusababisha usikilizaji wa
rufaa kukwama.
Akizungumza wakati wa
kufunga rasmi kikao cha siku mbili (2) cha Majaji wa Mahakama ya Rufani nchini
kilichofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Mwalimu Nyerere
(JNICC) Aprili 24, 2019, Mhe. Jaji Mkuu alisema kwa kufanya hivyo kutapunguza
makosa yanayojitokeza ambayo kwa wakati mwingine hupelekea ucheleweshaji wa
usikilizwaji wa rufaa hizo kwa kufanya marekebisho mara kadhaa.
“Ni vyema Manaibu
Wasajili na Watumishi wanaohusika katika utayarishaji wa nyaraka hizo, kuandaa vyema kumbukumbu za rufaa ‘records of
appeal’ kwa kuibua makosa mbalimbali yanayoonekana pindi wanapoandaa kumbukumbu
za rufaa ili kuzuia kesi kuchukua muda mrefu Mahakamani,” alieleza Mhe. Jaji
Mkuu.
Awali, akitoa taarifa
ya Utendaji wa Mahakama ya Rufani kwa mwaka 2018, Naibu Msajili Mwandamizi wa
Mahakama ya Rufani (T), Mhe. Elizabeth Mkwizu alisema kwa mwaka huo Mahakama ya
Rufani iliweza kushughulikia jumla ya mashauri 1230 katika jumla ya vikao 38
vilivyofanyika katika Kanda 11 kote nchini.
Mhe. Mkwizu alisema
kuwa jumla ya Mashauri 1108 kati ya 1230 yaliyopangwa katika vikao hivyo
yalimalizika ikiwa ni asilimia tisini (90%) ya mashauri yote yaliyopangwa
kusikilizwa.
“Hiki ni kiwango kizuri
pamoja na kuwa lengo la kumaliza mashauri kwa asilimia mia moja (100%)
halikutimia, hata hivyo tunatoa pongezi kwa wote waliochangia mafanikio hayo,”
alieleza Mhe. Mkwizu.
Akizungumzia muda wa
mashauri kukaa Mahakamani, Mhe. Mkwizu alisema kuwa takwimu za mashauri zinaonyesha
kushuka kwa wastani wa muda wa rufaa za jinai kukaa Mahakamani kutoka siku 5240 mnamo Februari, 2017 hadi siku 898 kufikia mwishoni mwa Desemba 2018
na kusema hii ni hatua kubwa.
Kwa upande mwingine, kwa
mwaka huu 2019 Mahakama ya Rufani imejiwekea malengo ya kuendelea kusikiliza
mashauri na kuimarisha masjala.
Kwa mujibu wa taarifa
ya Mpango kazi wa Mahakama ya Rufani ya mwaka 2019 Mahakama ya Rufani tayari
imepitia Rejista na kukusanya takwimu za mashauri, kufanya ‘stock taking’ ya
mashauri yaliyopo katika masjala, kuainisha idadi ya mashauri yaliyopo kwa
kanda na kwa umri lengo likiwa ni kuweka mkakati wa uondoshaji wa mashauri ya
zamani kulingana na mzigo uliopo kwa kila kanda.
Mkutano wa mwaka huu wa
Wahe. Majaji wa Mahakama ya Rufani pia uliwashirikisha Manaibu Wasajili,
wasaidizi wa kisheria wa Majaji, Makarani na watunza kumbukumbu ambao walitoa
taarifa za utendaji kazi pamoja na changamoto zinazowakabili ili waweze
kusaidiana kwa pamoja kupanga mikakati ya kumaliza mashauri kwa wakati.
Jaji Mkuu wa Tanzania,
Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (wa kwanza kulia) akiwa katika kikao cha mwaka
cha Majaji wa Mahakama ya Rufani cha kutathmini utendaji wa mwaka 2018 na
kuweka malengo ya mwaka 2019. Kikao hicho kilifanyika kwa siku mbili (2) Aprili
23 na 24, 2019 katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Mwalimu Nyerere
(JNICC) jijini Dar es Salaam. Kikao hicho kimewashirikisha Wahe. Majaji wa
Mahakama ya Rufani, Manaibu Wasajili wa Mahakama ya Rufani na Mahakama Kuu, Wasaidizi
wa Kisheria wa Majaji, Makarani na Watunza kumbukumbu wa Mahakama ya Rufani.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni