Na
Mary Gwera na Dennis Buyekwa, Mahakama
Mahakama ya Tanzania
kwa kushirikiana na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto imeandaa utaratibu wa
kuwapatia mafunzo maalum Mahakimu wapya wanaojiriwa yatakayowawezesha kutimiza wajibu
wao kwa weledi.
Hayo yamezungumzwa na
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma Aprili 25, 2019 Ofisini
kwake Mahakama ya Rufani-Dar es Salaam mara baada ya kumuapisha rasmi Mhe.
Mfanyeje Omari Banza, kuwa Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo.
“Tofauti na miaka ya
nyuma, kuanzia mwaka huu Mahakimu wote watakaoajiriwa watahudhuria mafunzo
maalumu yatakayokuwa yanaendeshwa na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto ili kuwajengea uwezo utakaowawezesha kutimiza
majukumu yao vyema” alieleza Mhe. Jaji Mkuu.
Kwa upande mwingine, Mhe.
Jaji Mkuu amemuasa Mhe. Banza kutimiza majukumu yake ya utoaji haki kwa
kuzingatia sheria na taratibu zilizopo ikiwa ni pamoja na kutojihusisha na vitendo vya rushwa.
“Mahakama tunatuhumiwa
sana kwa kujihusisha na vitendo vya rushwa, hivyo ni wajibu wa kila mmoja wetu kukemea
vitendo hivyo ili kurejesha taswira nzuri ya Mahakama kwa jamii,” alieleza Mhe.
Jaji Mkuu.
Akizungumza katika mahojiano
maalum mara baada ya kuapishwa, Mhe. Banza ameahidi kutumikia vyema nafasi hiyo
kwa kufuata misingi ya sheria na taratibu zilizopo katika kutekeleza majukumu
yake ya uhakimu.
Akizungumzia safari
yake ya utumishi ndani ya Mahakama Mhe. Banza amesema, alianza kufanya kazi
Mahakama kama Karani wa Mahakama ya Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro mwaka
2004.
Mwaka 2006, Mhe. Banza alihamishiwa
Mahakama ya Rufani, Kitengo cha Masjala ya wazi akihudumu kama Karani wa
Mahakama hiyo. Mnamo mwaka 2008 alihamishiwa Mahakama Kuu ya Tanzania- Dar es
Salaam, Kitengo cha Jinai akihudumu kama Karani wa Mahakama hiyo.
Aidha Mhe. Banza ameendelea na kazi hiyo ya Ukarani hadi
kuapishwa kwake rasmi leo Aprili 25, 2019.
Akizungumzia safari
yake ya masomo, Mhe. Banza amesema alianza kujiendeleza kimasomo mwaka 2007
katika fani ya Sheria mpaka alipohitimu mwaka 2011 katika Chuo Kikuu Huria-Dar
es Salaam. Mwaka 2014 Mhe. Banza alijiunga na Shule ya sheria (Law School) na
kufanikiwa kuhitimu masomo yake ya uanasheria kwa vitendo.
Hafla hiyo fupi
imehudhuriwa na Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Eliezer
Mbuki Feleshi pamoja na Maafisa kadhaa wa Mahakama ya Tanzania.
Jaji Mkuu wa Tanzania,
Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (kulia) akimuapisha Bi. Mfanyeje Omari Banza kuwa
Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo, wanaoshuhudia wa pili kushoto ni Naibu Msajili
Mwandamizi, Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Messeka Chaba, kushoto kwake ni
Mtendaji anayeshughulikia Mahakama za Mwanzo nchini, Bw. Humphrey Paya.
Wakisaini hati za
kiapo.
Mhe. Jaji Mkuu
akimpongeza Mhe. Banza kwa kuwa Hakimu mara baada ya kumuapisha rasmi.
Jaji Mkuu wa Tanzania,
Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akizungumza na Mhe. Banza mara baada ya
kumuapisha, wa kwanza kushoto kwa Mhe. Jaji Mkuu ni Jaji Kiongozi wa Mahakama
Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi pamoja na baadhi ya Maafisa
walioshiriki katika hafla fupi ya kuapishwa.
Pichani ni Mhe.
Mfanyeje Omari Banza, Hakimu mpya aliyeapishwa na Mhe. Jaji Mkuu.
(Picha na Mary Gwera,
Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni