Na
Lydia Churi na Magreth Kinabo-Mahakama
Mkutano wa Kamati ya
Uongozi wa Kongamano la Majaji Wakuu wa nchi za Kusini mwa Afrika (Southern
African Chief Justice’s Forum) umefanyika jijini Dar es salaam Tanzania chini
ya Mwenyekiti wa kongamano hilo ambaye ni Jaji Mkuu wa Malawi Mhe. Andrew
Nyirenda.
Mkutano huo pia
umehudhuriwa na Majaji wakuu wanne kutoka nchi za Kusini mwa Afrika ambazo ni pamoja
na Malawi, Zambia, Namibia, Seychelles na Tanzania ambayo ndiyo ilikuwa mwenyeji
wa Mkutano huo.
Akizungumza kuhusu
Kongamano la Majaji Wakuu wa nchi za kusini mwa Afrika, Mwenyekiti wa Kamati ya
Uongozi wa Kongamano hilo, Jaji Mkuu wa Malawi Mhe. Andrew Nyirenda alisema malengo
makuu ya kongamano hilo ni kujadili maendeleo ya Mahakama za kusini mwa Afrika,
kuimarisha na kulinda utawala wa sheria katika
nchi hizo pamoja na kuimarisha ushirikiano kati ya Mahakama za nchi zilizo
wananchama wa kongamano hilo.
Alisema kupitia kongamano
hilo, ajenda maalum huzungumzwa ikiwemo kuimarisha mawasiliano na majadiliano kati
ya Mahakama za nchi zilizo kusini mwa Afrika ili Mahakama hizo ziwe na maendeleo
ya pamoja. Alisema kupitia kongamano hilo wanahamasisha kuwepo kwa utawala wa
sheria kwa kuwa Mahakama ndicho chombo
chenye jukumu la kusimamia utawala wa sheria.
Kwa mujibu wa Mhe. Jaji
Nyirenda, Kongamano hilo pia huboresha ustawi wa watumishi wa Mahakama kazini wakiwemo
Majaji, Mahakimu pamoja na watumishi
wengine wa Mahakama zilizo kwenye nchi za kusini mwa Afrika.
Kuhusu mafanikio
yaliyofikiwa na Kongamano hilo, Mwenyekiti huyo alisema kumekuwa na maendeleo hasa
kwa upande wa Sheria kwani baadhi ya sheria na kanuni zimeweza kufanyiwa mabadiliko
katika baadhi ya nchi zilizo kwenye umoja huo. Aliongeza kuwa mafaniko mengine
yaliyofikiwa kutokana na kuwepo kwa Kongamano hilo ni pamoja na kuwajengea
uwezo watumishi wa Mahakama kwa kuwapatia mafunzo mbalimbali yakiwemo ya
uongozi.
Kuhusu umuhimu wa
Kongamano la Majaji Wakuu wa nchi za kusini mwa Afrika, Jaji Mkuu Mhe. Nyirenda
alisema umuhimu wake umeonekana hasa baada ya kuimarika kwa kazi za kila siku za Mahakama
katika maeneo nchi hizo na pia wameweza kubadilishana uzoefu katika masuala ya
sheria na pia kutatua changamoto mbalimbali zinazozikabili Mahakama zao kwa
pamoja.
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (wa pili kushoto) akionesha kitu kwa Majaji Wakuu wenzake mara baada ya kumaliza Mkutano wao. Wa kwanza kushoto ni Jaji Mkuu wa Zambia Mhe. Irene Mambilima ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Kongamano hilo. Katikati ni Jaji Mkuu wa Malawi Mhe. Andrew Nyirenda akifuatiwa na Jaji Mkuu wa Namibia Mhe. Peter Shivute na wa kwanza kulia ni Jaji Mkuu wa Seychelles Mhe. Mathilda Twomey.
Wajumbe
wa Kamati ya Uongozi wa Kongamano la Majaji Wakuu wa Nchi za Kusini mwa
Afrika (Southern African Chief Justice's Forum) wakiwa katika picha ya pamoja na wasaidizi wao mara baada ya kumaliza Mkutano wao. Nyuma wa Kwanza kushoto ni Mratibu wa Kongamano hilo Mhe. Jaji Evaristo Pengele.
Wajumbe wa Kamati ya Uongozi wa Kongamano la Majaji Wakuu wa Nchi za Kusini mwa Afrika (Southern African Chief Justice's Forum) wakiwa katika picha ya pamoja na wasaidizi wao mara baada ya kumaliza Mkutano wao.
Majaji Wakuu kutoka nchi tano za Kusini mwa
Afrika (Southern African Chief Justice's Forum) wakiwa katika picha ya
pamoja mara baada ya kumaliza Mkutano wao.Waliokaa katikati ni Mwenyekiti wa Kongamano hilo ambaye pia ni Jaji Mkuu wa Malawi Mhe. Andrew Nyirenda. Kulia kwake ni Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma na kushoto ni Jaji Mkuu wa Zambia Mhe. Irene Mambilima. Waliosimama kutoka kulia ni Jaji Mkuu wa Namibia Mhe. Peter Shivute akifuatiwa na Jaji Mkuu wa Seychelles Mhe. Mathilda Twomey na wa kwanza kushoto ni Mratibu wa Kongamano hilo Jaji Mhe. Evaristo Pengele.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni