Na Lusako Mwang’onda, Mahakama
Kuu – Iringa
Jumla ya mashauri thelathini
na moja (31) yanatarajiwa kusikilizwa katika vikao maalum vya Mahakama ya
Rufani ‘Court of Appeal session’ vinavyofanyika Mahakama Kuu, Kanda ya Iringa
kuanzia Aprili 29, 2019 hadi Mei, 15 mwaka huu.
Akizungumza katika
mahojiano maalum, mapema Aprili 29, 2019 Naibu Msajili wa Mahakama ya Rufani,
Mhe. Amir Msumi alisema jumla ya mashauri ishirini na mbili (22) kati ya hayo
ni mashauri ya muda mrefu na mashauri tisa (9) ni mashauri yenye umri wa kati
na mapya.
“Mkakati uliopo ni
kuhakikisha hali ya kuzalisha mlundikano hasa kwa mashauri yenye umri mkubwa
inadhibitibiwa” alisema Mhe. Msumi huku akiongeza kuwa sambamba na kikao hiki vikao
vingine vinafanyika Dar es Salaam na Bukoba.
Naibu Msajili huo
aliongeza kuwa kikao hicho ni muendelezo wa utekelezaji wa Mpango Maalumu wa
kumaliza mlundikano wa mashauri yenye umri mkubwa mahakamani ‘backlogs’ ambacho
pia hushughulikia mashauri yenye umri wa kati na mapya ‘back-stopping’.
Ufunguzi rasmi wa hivyo
katika Kanda hiyo ulifanyika katika viwanja vya Mahakama Kuu Kanda ya Iringa na
umeongozwa na Mwenyekiti wa kikao hicho ambaye ni Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe.
Kipenka M. Mussa.
Mbali na Mhe. Jaji
Kipenka ambaye ndiye Mwenyekiti wa jopo kikao hicho kitaendeshwa na Majaji wengine
wa Mahakama ya Rufani ambao ni Mhe. Jaji Shaaban Lila, Mhe. Jaji Ferdinand
Wambali na Mhe. Jaji Winifrida Korosso.
Mwenyekiti
wa jopo la Majaji wanne wa Mahakama ya Rufani (T) waliopo katika kikao cha
Mahakama hiyo mkoani Iringa, Mhe. Jaji Kipenka Mussa (mwenye joho jekundu) akikagua gwaride maalum
kuashiria ufunguzi rasmi ya kikao cha Mahakama ya Rufani kitakachofanyika
Mahakama Kuu Kanda ya Iringa kuanzia Aprili 29, 2019 hadi Mei 15, 2019.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni