Jaji Mkuu wa Tanzania
Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amesema kuwa Mahakama ya Tanzania imeonyesha nia
ya dhati katika kupiga vita vitendo vya rushwa, ukosefu wa maadili na matumizi
ya lugha zisizozingatia staha.
Akifungua warsha ya
kujadili rasimu ya miongozo ya mafunzo na uendeshaji wa kamati za Maadili ya
watumishi wa Mahakama ya Tanzania iliyofanyika leo Kisutu jijini Dar es salaam,
Jaji Mkuu amesema Mahakama imelipa kipaumbele suala la kuimarisha maadili ya
watumishi wake kwenye ngazi zote kama sehemu ya uwajibikaji kwa kuwa uhuru wa Mahakama
unaimarika kunapokuwa na uwajibikaji na maadili.
Jaji Mkuu amesema lengo
la maboresho ya Mahakama ya Tanzania halitafanikiwa endapo suala la maadili
halitapewa uzito unaostahili kwani rushwa na utovu wa Maadili havina nafasi
katika Mahakama inayofuata misingi ya maboresho.
Aidha, Jaji Mkuu pia
aliwataka wananchi kutoa taarifa za kweli za matukio ya ukiukwaji wa maadili kwenye
kamati za Maadili za Mahakama, “Jitihada dhidi ya vitendo hivi zitafanikiwa tu
endapo wananchi watawasilisha taarifa za kweli za matukio ya ukiukwaji wa
Maadili mbele ya Kamati za Maadili”, alisema Jaji Mkuu.
Amezitaka kamati za
maadili kufanya kazi zake kwa kufuata taratibu na miongozo iliyowekwa.
Alisema dhamira ya
Mahakama katika kupambana na ukiukwaji wa maadili na vitendo vya rushwa pia
inaonekana wazi kwenye mikakati iliyojiwekea ikiwemo kutoa elimu ya mapambano
dhidi ya rushwa kupitia njia mbalimbali hasa kusambaza mabango katika majengo ya mahakama
nchi nzima.
Mabango yaliyosambazwa
nchi nzima yana ujumbe maalum unaowataka wananchi kutoa taarifa za vitendo vya rushwa
na ukiukwaji wa maadili. “Kulalamika
peke yake bila kutoa taarifa hakutoshi katika vita dhidi ya vitendo viovu”,
alisema.
Jaji Mkuu aliwataka
wadau wa Mahakama ya Tanzania na Tume ya Utumishi wa Mahakama wanaohudhuria mkutano
huo kupitia rasimu za miongozo na kutoa maoni yenye lengo la kuiboresha ili iweze
kupunguza ama kumaliza mapungufu
yaliyopo.
Alisema Mkutano wa
wadau ni muendelezo wa kuhakikisha kuwa Sheria ya Uendeshaji wa Mahakama Na. 4
ya mwaka 2011 ambayo imeleta mabadiliko makubwa ndani ya Mahakama inafanya kazi
kwa manufaa ya kujenga imani ya wananchi kwa Mahakama za Tanzania.
Alisema Tume ya
Utumishi wa Mahakama ndiyo mamlaka ya nidhamu kwa watumishi wa Mahakama
wakiwemo Mahakimu katika ngazi zote Majaji, Wasajili na watumishi wengine wa
Mahakama.
Jukumu kubwa la Kamati
za Maadili ni kuchunguza malalamiko yanayofikishwa mbele ya Kamati husika, juu
ya ukiukaji wa maadili dhidi ya watumishi wa Mahakama.
Kamati za maadili ni
jicho la Tume katika kusimamia, kuendeleza na kudumisha maadili ya Utumishi wa
Mahakama ili kuufanya utumishi wa mahakama uwe wenye kutukuka, kuheshimika na
unaojenga Imani ya wananchi kwa Mhimili wa Mahakama. Jicho hili, linatokana na
ukweli kwamba, Kamati zimepewa wajibu wa kisheria, wa kuishauri Tume kuhusu
uzingatiaji wa maadili ya Utumishi ili watoe huduma iliyo bora kwa jamii ya
watanzania.
Jaji Mkuu wa Tanzania
Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akifungua Warsha ya kujadili Rasimu ya Miongozo ya Mafunzo ya Uendeshaji wa Kamati za Maadili ya Watumishi wa Mahakama iliyofanyika leo Kisutu jijini Dar es salaam.
Wadau wa Mahakama wakiwemo Makatibu Tawala wa Mikoa (RAS), Makatibu Tawala wa Wilaya(DAS), Viongozi wa Dini, Watumishi wa Mahakama na wadau wengine wakiwa kwenye Warsha ya kujadili Rasimu ya Miongozo ya Mafunzo ya Uendeshaji wa Kamati za Maadili ya Watumishi wa Mahakama iliyofanyika leo Kisutu jijini Dar es salaam.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Hussein Kattanga ambaye pia ni Katibu wa Tume ya Utumishi wa Mahakama akizungumza kwenye Warsha ya kujadili Rasimu ya Miongozo ya Mafunzo ya Uendeshaji wa Kamati za Maadili ya Watumishi wa Mahakama iliyofanyika Aprili 30, Kisutu jijini Dar es salaam.
Kamishna wa Tume ya Utumishi wa Mahakama Prof. Angelo Mapunda akizungumza kwenye Warsha ya kujadili Rasimu ya Miongozo ya Mafunzo ya Uendeshaji wa Kamati za Maadili ya Watumishi wa Mahakama iliyofanyika leo Kisutu jijini Dar es salaam.
Wadau wa Mahakama wakiwa katika picha ya pamoja na Jaji Mkuu wa Tanzania Prof. Ibnrahim Hamis Juma (waliokaa katikati) mara baada ya kkufunguliwa kwa Warsha ya kujadili Rasimu ya Miongozo ya Mafunzo ya Uendeshaji wa Kamati za Maadili ya Watumishi wa Mahakama iliyofanyika leo Kisutu jijini Dar es salaam.
Jaji Mstaafu Mhe. Eusebia Munuo akizungumza kwenye Warsha ya kujadili Rasimu ya Miongozo ya Mafunzo ya Uendeshaji wa Kamati za Maadili ya Watumishi wa Mahakama iliyofanyika leo Kisutu jijini Dar es Salaam.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni