Na
Mary Gwera, Mahakama-Iringa
Jaji Kiongozi, Mahakama
Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi mapema leo Aprili 04, 2019
amewasili Mkoani Iringa kuanza rasmi ziara ya kikazi katika Mahakama Kanda ya
Iringa pamoja na Kanda ya Mbeya.
Katika ziara yake Mhe.
Jaji Kiongozi, anatarajiwa kuongoza hafla ya kumuaga rasmi kitaaluma, Jaji
Mstaafu wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Iringa, Mhe. Jaji Mary Simbo Shangali
itakayofanyika Aprili 05, 2019 katika Ukumbi ya Mahakama Kuu-Iringa.
Aidha; Mhe. Jaji Dkt.
Feleshi atapata wasaa wa kutembelea Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe ambayo pia ni sehemu ya Kanda ya Iringa na vilevile atazungumza na Watumishi pamoja na kukagua miradi mbalimbali
ya ujenzi wa Mahakama inayoendelea katika Kanda hizo mbili.
Lengo la ziara ni kujua
hali ya maendeleo ya utekelezaji wa maboresho
ya huduma mbalimbali za Mahakama na
vilevile kuwakumbusha Watumishi wa Mhimili huu kuendelea kutekeleza jukumu la msingi
la utoaji haki nchini kwa ubora wa hali ya juu kwa manufaa ya wananchi ambao
ndio walengwa wakuu.
Jaji Kiongozi, Mahakama
Kuu ya Tanzania, Mhe. Jaji Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi (kushoto) akisalimiana na
Jaji Mfawidhi, Mahakama Kuu-Kanda ya Iringa, Mhe. Panterine Kente pindi
alipowasili mkoani humo.
Mhe. Jaji Kiongozi (wa
tatu kulia) akifurahia jambo na Wenyeji wake waliofika kumlaki, wa pili kulia
ni Jaji Mfawidhi, Mahakama Kuu-Kanda ya Iringa, Mhe. Panterine Kente na wa
kwanza kulia ni Jaji wa Mahakama Kuu, Kanda ya Iringa, Mhe. Immaculate Kajetan
Banzi, na wa kwanza kushoto ni Hakimu Mkazi Mfawidhi, Mahakama ya Wilaya Iringa.
(Picha na Mary Gwera, Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni