Jumanne, 2 Aprili 2019

KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA KATIBA NA SHERIA YAKAGUA JENGO LA MAHAKAMA KUU MUSOMA: YARIDHISHWA NA MAENDELEO YA UJENZI


Na Francisca Swai, Mahakama ya Hakimu Mkazi, Musoma

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria ikiongozwa na Kaimu Mwenyekiti wa kamati hiyo  Bw. Emmanuel Mwakasaka imefanya ukaguzi katika jengo la Mahakama Kuu Musoma lililopo katika hatua za mwisho za ujenzi.

Ukaguzi huo ulifanyika Machi 30, 2019 wakiongozwa na mwenyeji wao Jaji wa Mahakama Kuu, Kanda ya Mwanza, Mhe. Mohamed Gwae pamoja na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Mwanza, Mh. Mary Moyo, pamoja na watumishi mbali mbali wa Mahakama ya Tanzania. 

Katika ziara hiyo kamati hiyo ya Bunge, ilionyesha kuridhishwa kwa namna ujenzi unavoendelea na hatua iliyofikiwa. Ugeni huo ulifanya kaguzi ya jengo zima ikiwa ni pamoja na kukagua vifaa (materials) vya ujenzi vinavyotumika kama vile nondo na ubora wake.

Pamoja na ukaguzi huo, kamati hiyo pia ilitoa mapendekezo mbalimbali, kama vile kushauri kazi ya upakaji rangi iendelee kwa kasi ili kumaliza mapema na jengo lianze shughuli zake, pia walishauri, kwakuwa katika eneo lililojengwa Mahakama hiyo bado kuna eneo kubwa sana, ni vyema kukajengwa Mahakama ya watoto (Juvenille Court) ili kuwatenganisha watoto na watu wazima na pia ili kesi zao zisikilizwe kwa haraka zaidi.

Mwenyeji wa ugeni huo, Mhe. Jaji Gwae, aliiomba kamati hiyo, kuchukua kilio cha upungufu wa watumishi na kukifanyia kazi, ili kupata kibali cha ajira kwakuwa watumishi waliopo hawatoshelezi na bado Mahakama hiyo itakapoanza kazi rasmi itabidi watumishi wake kupunguzwa kutoka katika vituo vya sasa na kuletwa kufanya kazi hapo, jambo ambalo litaongeza uhaba na mzigo mkubwa wa kazi kwa watumishi wa Mahakama.
 Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria wakifanya ukaguzi katika sehemu ya mbele ya jengo la Mahakama Kuu Musoma lililopo katika hatua za mwisho za ujenzi wake.
 Wajumbe wa Kamati ya kudumu ya Katiba na Sheria wakiwa katika ukaguzi wa jengo na vifaa vya ujenzi wa jengo hilo. Anayetoa maelezo (kulia) ni Mkuu wa Kitengo cha Ujenzi, Mahakama ya Tanzania, Mhandisi. Khamadu Kitunzi.






Hakuna maoni:

Chapisha Maoni