Na
Waandishi-Mahakama
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe.
Prof. Ibrahim Hamis Juma amekishauri chama cha wanasheria cha Tanganyika Law
Society (TLS) kushirikiana na Mahakama katika kutekeleza majukumu yake.
Akizungumza na Rais wa
TLS pamoja na ujumbe wake walipomtembelea leo ofisini kwake jijini Dar es
salaam, Jaji Mkuu amesema Mahakama pamoja na chama hicho wanayo maeneo mengi ya
kushirikiana pasipo kuingiliana katika majukumu yao.
Aidha, Jaji Mkuu pia amekishauri
chama hicho kuwa na mpango kazi wa muda mrefu ili kuongeza ufanisi ndani ya
chama hicho kwa kuwa kwa mujibu wa Sheria, viongozi wa chama hicho hukaa
madarakani kwa kipindi cha mwaka moja kabla ya uchaguzi kufanyika tena.
Akizungumzia mapambano
dhidi ya rushwa katika utoaji wa haki, Jaji Mkuu amewataka Mawakili nao
kupambana na rushwa kwa kushirikiana na Mahakama ya Tanzania ili waweze
kutekeleza majukumu yao kwa kufuata maadili.
“Zifanyieni kazi changamoto za
rushwa na shirikianeni na Mahakama ya Tanzania kwa kuwa Mahakama ni mfumo wa
kukosoana, alisema Jaji Mkuu.
Kwa upande wake, Rais
wa TLS Mhe. Dkt. Rugemeleza Nshala ameiomba Mahakama ya Tanzania kushughulikia
changamoto mbalimbali wanazokutana nazo Mawakili wanapotekeleza majukumu yao ya
kisheria Mahakamani ikiwemo kuchelewa kuanza kwa kesi mahakamani.
Rais huyo pia
aliishukuru Mahakama kwa ushirikiano inaoutoa kwa chama chake na kuahidi
kufanya kazi zake kwa kushirikiana na Mahakama ya Tanzania.
Naye Jaji Kiongozi wa
Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezar Feleshi amewapongeza viongozi wapya
wa TLS waliochaguliwa hivi karibuni na kuwashauri kufanya kazi kwa kushirikiana
na Mahakama ya Tanzania.
“Mifumo yetu iko wazi
nasi tuko tayari kufanya kazi nanyi kwa kuwa wote tunayo nia moja ya kumtumikia
mwananchi”, alisema Jaji Kiongozi.
Wakati huo huo,
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Bwn. Hussein Kattanga amewashauri
viongozi wa TLS kushirikiana na Mahakama katika kutatua changamoto mbalimbali za
upatikanaji wa haki na kuwataka kuwasilisha hoja na malalamiko kwa kuwa
Mahakama kwa sasa inapokea hoja, maoni na malalamiko ili kuboresha huduma zake.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akizunzumza na viongozi wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) walipomtembelea mapema Mei 16, 2019 ofisini kwake Mahakama ya Rufani jijini Dar es Salaam. Wa kwanza kulia kwake ni Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe.Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi, anaefuata ni Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Hussein Kattanga, kushoto kwake ni Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) Dkt. Rugemeleza Nshala, anaefuata ni Makamu wa Rais wa Chama hicho Bw. Mpale Mpoki , pamoja na wajumbe wengine walioshiriki katika mazungumzo hayo.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. ibrahim Hamis Juma akisisitiza jambo wakati akizungumza na ujumbe kutoka Chama cha Wnasheria Tanganyika, ukiongozwa na Rais wa chama hicho, Dkt. Rugemeleza Nshala.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi akizungumza na ujumbe huo.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Hussein Kattanga akichangia jambo katika mazungumzo hayo.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akiwa katika picha ya pamoja na Rais wa Chama cha Wanasheria nchini (TLS) Dkt. Rugemeleza Nshala (kushoto kwa Jaji Mkuu) pamoja na wajumbe wengine.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni