Na Emmanuel Oguda, Mahakama Kuu-Shinyanga
Jamii
Mkoani Shinyanga imetakiwa kupiga vita vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia
dhidi ya wanawake na watoto.
Hayo
yamebainishwa katika Mkutano maalum uliofanyika katika Kata ya ‘Old’
Shinyanga Manispaa ya Shinyanga Mei 26, 2019 wakati Chama cha Majaji Wanawake
Nchini (TAWJA) kilipokutana na wananchi na kutoa elimu kuhusu haki za watoto na
unyanyasaji wa kijinsia kwa wanawake na watoto.
Akizungumzia
kuhusu vitendo vya ukatili wa kijinsia, Naibu Msajili wa Mahakama Kuu, Kanda ya
Shinyanga, Mhe. Eugenia Rujwahuka, amesisitiza kuwa, watoto wana haki ya kupata
elimu, pia wana haki ya kutonyanyasika na endapo wataona vitendo vyovyote
vinavyoelekea kuvunja haki zao, wachukue hatua mapema ya kutoa taarifa Polisi
ama kwa Serikali za Vijiji na Mitaa ili wahusika wachukuliwe hatu za kisheria.
“Jamii
inapaswa kutoa ushirikiano pindi wanapobainia vitendo vya uvunjwaji haki za
watoto na waondokane na dhana iliyozoeleka Kanda ya ziwa ya ‘Kutulija’ yaani
kumtenga mtu anayetoa ushahidi ama kuripoti juu ya matukio ya uvunjwaji wa haki
za binadamu, wanawake na watoto,” alisema Mhe. Rujwahuka.
Naye
Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni, Mhe. Hanipha Mwingira
amesisitiza juu ya haki ya kurithi kwa wanawake na watoto wanaoachwa baada ya
wapendwa wao kufariki kuwa wana haki ya kusimamia mirathi na kurithi na
waondokane na dhana iliyojengeka kuwa mtoto wa kike hana haki ya kurithi.
Katika
Mkutano huo wananchi wametoa maoni yao kuhusu haki za wanawake na watoto pamoja
na vitendo vya ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto Mkoani humo na
kusisitiza Serikali iendelee kuwachukulia hatua kali za kisheria wale wote
wanaobainika kujihusisha na vitendo vya ukatili.
Aidha
wananchi hao wameomba elimu iendelee kutolewa maeneo ya vijijini zaidi ambako
vitendo hivyo vimeshamiri kwa kiasi kikubwa.
Mada
zilizofundishwa ni pamoja na Mirathi, Haki za Watoto na Ukatili wa kijinsia kwa
wanawake na watoto.
Naibu Msajili Mahakama
Kuu Kanda ya Shinyanga, Mhe. Sekela Mwaiseje akitoa mada kwenye mkutano na
wananchi kuhusu ukatili na unyanyasaji wa kijinsia, Kata ya Old Shinyanga,
Manispaa ya Shinyanga.
Baadhi ya watoto wa
Kata ya Old Shinyanga waliofika kwa ajili ya kupata elimu juu ya haki zao.
Mhe, Janeth Elias Massesa, Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Wilaya Shinyanga akiongea na watoto wa Kata ya Old Shinyanga juu ya haki zao.
Mhe. Hanifa Mwingira, Hakimu Mkazi Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni akisisitiza jambo wakati wa utoaji elimu juu ya haki ya kurithi kwa wanawake na watoto.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni