Mtendaji wa Mahakama
Kuu ya Tanzania kanda ya Musoma, Bibi Zilliper Achieng’ Geke amestaafu rasmi kazi
leo baada ya kutimiza umri wa kustaafu kwa hiari kwa mujibu wa sheria za
utumishi wa Umma.
Akizungumza na baadhi
ya watumishi wa Mahakama Kuu kanda ya Musoma Musoma kabla ya kustaafu, Mtendaji
huyo aliwaasa watumishi kuhakikisha wanakuwa na umoja na mshikamano katika
kutekeleza majukumu yao ya kila siku.
“Hakuna jambo
linaloshindikana katika umoja, kila mtu akitambua nafasi yake lakini pia akijua
kuwa peke yake hawezi bila ya mwenzake hakuna litakaloshindikana”, alisisitiza
Mtendaji huyo.
Aidha, bibi Geke pia
aliwataka watumishi hao kupendana, kuheshimiana na kushirikiana katika kazi zao
hatua itakayowawezesha kutekeleza Mpango Mkakati wa Miaka Mitano (2015/16 hadi 2019/2020) wa Mahakama ya Tanzania vizuri na kufikia lengo kuu la
kutoa haki sawa kwa wote na kwa wakati.
Aliwashauri maafisa Tawala
na Utumishi wa kanda hiyo kuhakikisha wanaendelea na ukarabati mdogo mdogo wa majengo
ya Mahakama hasa zile za Mwanzo licha ya ufinyu wa bajeti. Alisema kwa kufanya
hivyo itasaidia kuboresha miundo mbinu hiyo na kuongeza ari ya kazi kwa
watumishi lakini pia usalama wao.
Mtendaji huyo ambaye
amefanya kazi katika Mahakama Mkoa wa Mara tangu mwezi Octoba 2013 atakumbukwa
kwa mengi ikiwemo kuhamasisha ushirikiano baina ya watumishi, usimamizi mzuri wa
ofisi, ukarabati wa Mahakama za Mwanzo na wilaya, ujenzi wa vyoo, pamoja na ushirikiano
mzuri na wadau.
Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Musoma Bibi Zilliper Achieng’ Geke akifafanua jambo ofisini kwake wakati akiwaaga watumishi wa Mahakama hiyo. Bibi Geke amestaafu rasmi Utumishi wa Umma kwa mujibu wa Sheria.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni