Na
Emmanuel Oguda, Mahakama Kuu-Shinyanga
Chama cha Majaji
Wanawake Tanzania (TAWJA) kimepongezwa kwa kuwa mstari wa mbele kupiga vita
vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto.
Pongezi hizo zimetolewa
na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Shinyanga, Mhe. Jaji Richard Malima
Kibella Mei 23 wakati akifungua rasmi mafunzo ya siku tatu juu ya Haki za
Binadamu na Unyanyasaji wa Kijinsia kwa wasimamizi wa Sheria (Law Enforcers)
Kanda ya Shinyanga yanayoendelea kufanyika katika Ukumbi wa Mikutano Karena
Hoteli, Shinyanga.
Mhe. Jaji Kibella
amewaomba TAWJA kuendelea kutoa Mafunzo na kuwajengea uwezo Mahakimu pamoja na
Taasisi zinazosimamia moja kwa moja kupinga ukatili wa kijinsia dhidi ya
wanawake na watoto ili jamii iweze kutambua mchango wa wanawake katika ujenzi
wa Taifa.
“Kumuelimisha mwanamke
ni sawa na kuelimisha Jamii nzima, hivyo ninawaomba TAWJA muendelee kutoa elimu
juu ya madhara yatokanayo na vitendo vya ukatili wa jinsia kwa wanawake na
watoto ili jamii yetu itambue madhara hayo na kuweza kuwalinda wanawake dhidi
ya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia” alieleza Mhe. Jaji Mfawidhi.
Mafunzo hayo ya siku
tatu (3) yanayotarajiwa kumalizika Mei 25 yameandaliwa na Chama cha Majaji Wanawake
Tanzania (TAWJA) yanatarajiwa kumalizika tarehe Mei 25, 2019 na yamejumuisha
Mahakimu wa Kanda ya Shinyanga, Maafisa Ustawi wa Jamii na Huduma kwa Jamii,
Dawati la Jinsia Polisi, Magereza.
Washiriki wengine ni pamoja
na viongozi wa dini huku wawezeshaji wakiwa ni baadhi ya Waheshimiwa Majaji
wastaafu, Mhe. Jaji Salum Massati,Jaji Mstaafu Mahakama ya Rufani Tanzania,
Mhe, Jaji Cresensia Makuru , Jaji Mstaafu wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Mhe.
Jaji Rose Teemba, Jaji Mstaafu wa Mahakama Kuu ya Tanzania.
Mhe. Jaji Richard Malima Kibella, Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu Kanda ya Shinyanga akizungumza wakati alikuwa akifungua rasmi mafunzo ya Haki za
Binadamu na Unyanyasaji wa Kijinsia kwa wasimamizi wa Sheria (Law Enforcers)
Kanda ya Shinyanga.
Washiriki wakijadili katika makundi.
Picha ya pamoja ya Washiriki wa Mafunzo ya Haki za
Binadamu na Unyanyasaji wa Kijinsia kwa wasimamizi wa Sheria (Law Enforcers)
Kanda ya Shinyanga. Katikati ni Jaji Mfawidhi, Mahakama Kuu, Kanda ya Shinyanga, Mhe. Richard Kibella na baadhi ya Majaji wastaafu walioketi nae.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni