Na Dennis Buyekwa-Mahakama
Mahakama
ya Tanzania imeunganisha mfumo wake wa
kusajili na kuratibu mashauri (JSDS ll) na mfumo wa serikali wa ukusanyaji wa
Mapato (GePG) ili kurahisisha ukusanyaji wa mapato na kuondokana na changamoto
zinazotokana na ukusanyaji na utunzanji wa mapato ya serikali.
Katika
hatua za kuhakikisha mfumo huu unafanya kazi yake ipasavyo, Mahakama ya
Tanzania imeandaa mafunzo ya siku mbili kwa Wahasibu na Makarani wake
yaliyoanza jana katika kituo cha Mafunzo
na Habari kilichopo ndani ya viwanja vya
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es salaam.
Akifungua
mafunzo hayo kwa niaba ya Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mkurugenzi wa
Mipango na Ufuatiliaji Bw. Mathias Mwangu alisema mafunzo hayo yanawahusisha
Wahasibu na Makarani wa Mahakama wenye uelewa wa namna mfumo wa JSDS ll
unavyofanya kazi na yanaendeshwa na Mahakama kwa kutumia maafisa Tehama wake
ambao ndio waratibu na wasimamizi wa Mfumo huo.
Alisema
lengo la mafunzo hayo ni kuwaandaa Wahasibu na Makarani kufanya kazi ya
kuratibu vyema makusanyo yote yanayokusanywa baina ya Mahakama ya Tanzania na
Serikali.
Mkurugenzi
wa Mipango na Ufuatiliaji alisema mfumo huo pia utaongeza ufanisi wa utoaji wa
huduma za Mahakama kwa kuwa sasa utawapunguzia mzigo Makarani wa kukutana na
wadaawa moja kwa moja na badala yake Shughuli zote zitafanyika kupitia mfumo
huo na watumishi sasa wataweza kufuatilia malipo yote kupitia mfumo huo wa
kielektroniki.
Alizitaja
faida za kutumia mfumo huo katika ukusanyaji wa maduhuli kuwa ni , pamoja na
kusaidia kukusanya mapato yanayotokana na huduma zinazotolewa na Mahakama ili
kusaidia Serikali kuboresha huduma mbalimbali kwa wananchi wake.
“Mfumo huu
umekuja kama muarobaini wa kuzuia upotevu wa mapato ya serikali kiholela",
alisema Bwn. Mwangu na kuongeza kuwa ukusanyaji mzuri wa mapato utaisaidia
Serikali kutekeleza mipango yake ya maendeleo.
Kuhusu
utaratibu wa kutoa mafunzo hayo, Mkurugenzi wa Mipango na Ufuatiliaji alisema
Mahakama imeyagawa mafunzo hayo katika kanda kuu nne (4) ambapo kutakuwa na
vituo vya Dar es Salaam ambacho kina jumuisha washiriki kutoka katika mikoa ya
Morogoro, Pwani, Tanga, Lindi na Mtwara.
Vituo
vingine ni Mbeya, Mwanza na Dodoma ambapo pia wanatarajia kuendesha mafunzo
kama hayo katika siku za usoni kulingana na namna ratiba za uendeshaji wa
mafunzo hayo.
Naye
mwezeshaji wa mafunzo hayo kutoka katika kitengo cha Tehama cha Mahakama Bwn.
Athumani Juma ameeleza kuwa kupitia mfumo huu wa kielektroniki Mawakili pamoja
na wadaawa wataweza kufanya malipo kwa wakati kitendo kitakachowasaidia
kusajili kesi zao kwa urahisi na haraka Zaidi.
Alisema
mfumo huo utarahisisha ukusanyaji wa mapato ndani ya Mahakama, utaokoa muda na
gharama na pia utasaidia kufanya malipo mahakamani ikiwa ni pamoja na
kuimarisha ulinzi katika kutunza taarifa za kimahakama.
Mfumo wa
kielekitroniki wa kusajili na kuratibu mashauri (JSDS ll) ulianzishwa kwa lengo
la kurahisisha zoezi zima la usajili wa kesi mbalimbali, lakini kutokana na
uhitaji wa kuboresha huduma za kimahakama, Mahakama imeona ni vyema kuboresha
huduma kwa kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa mapato hatua itakayosaidia
kutoa huduma bora na haki sawa kwa wote.
Watumishi
wa Mahakama wakiwemo Wahasibu na Makarani wakiwa kwenye mafunzo kuhusu
ukusanyaji wa mapato baada ya kuunganishwa kwa mfumo wa kusajili na kuratibu mashauri (JSDS ll) wa
Mahakama ya Tanzania na mfumo wa serikali wa ukusanyaji wa Mapato (GePG) yanayofanyika
katika kituo cha Mafunzo na Habari
kilichopo ndani ya viwanja vya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini
Dar es salaam.
Mhasibu wa Mahakama ya Tanzania Bibi Annastela Natai akizungumza wakati wa mafunzo ya Wahasibu na Makarani wa Mahakama kuhusu ukusanyaji wa mapato baada ya kuunganishwa kwa mfumo wa kusajili na kuratibu mashauri (JSDS ll) wa Mahakama ya Tanzania na mfumo wa serikali wa ukusanyaji wa Mapato (GePG) yanayofanyika katika kituo cha Mafunzo na Habari kilichopo ndani ya viwanja vya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es salaam.
Afisa Tehama wa Mahakama, Samwel Mshote akitoa mada wakati wa mafunzo ya Wahasibu na Makarani wa Mahakama kuhusu ukusanyaji wa mapato baada ya kuunganishwa kwa mfumo wa kusajili na kuratibu mashauri (JSDS ll) wa Mahakama ya Tanzania na mfumo wa serikali wa ukusanyaji wa Mapato (GePG) yanayofanyika katika kituo cha Mafunzo na Habari kilichopo ndani ya viwanja vya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es salaam.
Afisa Tehama wa Mahakama, Athuman Juma akitoa mada wakati wa mafunzo ya Wahasibu na Makarani wa Mahakama kuhusu ukusanyaji wa mapato baada ya kuunganishwa kwa mfumo wa kusajili na kuratibu mashauri (JSDS ll) wa Mahakama ya Tanzania na mfumo wa serikali wa ukusanyaji wa Mapato (GePG) yanayofanyika katika kituo cha Mafunzo na Habari kilichopo ndani ya viwanja vya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es salaam.
Mmoja wa Watumishi wa Mahakama wanaohudhuria mafunzo akichangia mada wakati wa mafunzo hayo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni