Na
Mary Gwera & Denis Buyekwa, Mahakama
Jaji Kiongozi wa
Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi, amesema Mahakama ya
Tanzania inatambua umuhimu wa wadau wake katika kufanikisha huduma ya utoaji
Haki nchini.
Mhe. Jaji Kiongozi
aliyasema hayo Juni 10 alipokuwa akifungua rasmi warsha ya siku tatu (3) ya Wadau
kuhusu uhamasishaji wa sheria, kanuni, taratibu na utendaji wa Mahakama Kuu Divisheni
ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, inayofanyika katika ukumbi wa mafunzo wa
Mahakama uliopo katika viwanja vya
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu-Dar es
Salaam.
“Kwa kuzingatia umuhimu
wa Wadau Mahakama ya Tanzania kupitia Mpango Mkakati wake wa miaka mitano (5)
2015/2016-2019/2020 chini ya nguzo namba tatu ambayo inasema Kurejesha
imani ya jamii na ushirikishwaji wa wadau inalenga katika kuweka mfumo wa utoaji haki
sawa kwa wote wenye kuaminiwa na jamii,” alisema Mhe. Jaji Kiongozi.
Akizungumzia mafunzo
hayo Mhe. Jaji Kiongozi amewataka wadau hao kutoa mawazo yatakayosaidia
Mahakama Kuu Kitengo cha Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi kujua namna bora
zaidi ya kuendesha mashauri yanayohusiana na vitendo vya makosa ya rushwa na
uhujumu uchumi ili iweze kuwasaidia kutoa haki kwa wakati.
Aidha; Mhe Jaji Dkt.
Feleshi aliongeza kwa kuwataka wadau hao kuibua changamoto mbalimbali
zinazopelekea ucheleweshaji wa kesi Mahakamani na kuja na mbinu ya namna ya
kukabiliana na changamoto hizo zitakazosaidia uendeshaji na umalizwaji wa
mashauri kwa wakati.
Katika hatua nyingine;
naye Mkuu wa Chuo Cha Uongozi wa Mahakama (IJA)-Lushoto, Mhe. Jaji Dkt. Paul
Kihwelo amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwapa uelewa wadau kuhusiana na suala
zima la utendaji wa Mahakama ikiwa ni pamoja na kujadili changamoto
zinazowakabili ili waweze kuzitafutia ufumbuzi hasa zile zinazohusiana na
masuala ya upelelezi.
“Mafunzo haya ni mwendelezo wa mafunzo mengine
yaliyokwishafanyika huko nyuma yakiwa na lengo la kutafuta namna bora ya
uendeshaji wa Mashauri yanayohusu makosa
ya Rushwa na uhujumu uchumi, taratibu za
kutoa hukumu na jinsi ya kusimamia utekelezaji wa maadili kwa maafisa wa
Mahakama” Alisema Mhe. Jaji Dkt. Kihwelo.
Mkuu huyo wa Chuo cha (IJA)
aliongeza kuwa mafunzo hayo yatasaidia kuleta uelewa wa pamoja kati ya Mahakama
na wadau wake hatua itakayopelekea kuongeza tija ya utendaji kazi baina ya
pande zote mbili.
Mafunzo hayo yameandaliwa
na Mahakama ya Tanzania kwa kushirikiana Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA) chini
ya udhamini wa Programu ya kitaifa ya kuzijengea uwezo Taasisi za Umma
zinazohusika kuzuia na kupambana na
Rushwa (BSAAT).
Washiriki wa Mafunzo
hayo ni Waheshimiwa Majaji kutoka Mahakama Kuu, Divisheni ya Makosa ya Rushwa
na Uhujumu Uchumi, Wadau kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya
Mwendesha Mashtaka wa Serikali (DPP), TAKUKURU, TCRA, Ofisi ya Wakili wa
Serikali, na Wizara ya Katiba na Sheria.
Jaji Kiongozi, Mahakama Kuu
ya Tanzania, Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi akifungua rasmi Warsha ya siku
tatu (3) ya Wadau kuhusu uhamasishaji wa Sheria, Kanuni, taratibu na utendaji wa
Mahakama Kuu, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi yanayofanyika
katika Ukumbi wa Mafunzo wa Mahakama uliopo katika Viwanja vya Mahakama ya
Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam.
Jaji Mfawidhi, Mahakama
Kuu-Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, Mhe. Dkt. Lilian Mashaka
(aliyesimama kulia) akitoa neno la utangulizi kabla ya kumkaribisha Mhe. Jaji
Kiongozi kufungua rasmi warsha hiyo. Walioketi kushoto ni Jaji Kiongozi,
Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi na katikati ni Mkuu
wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA) Lushoto, Mhe. Jaji Dkt. Paul Kihwelo.
Sehemu ya Washiriki wa
Warsha wakimsikiliza Mhe. Jaji Kiongozi alipokuwa akitoa nasaha za ufunguzi wa
warsha.
Washiriki wakimsikiliza
mgeni rasmi.
Mhe. Jaji Kiongozi
akitoa mada kwa washiriki.
Mmoja wa wadau wa kutoka Wizara ya Katiba na Sheria (aliyesimama)
akichangia jambo.
Mhe. Jaji Kiongozi
(katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Washiriki wa Mafunzo, kushoto ni
Jaji Mfawidhi- Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi,
Mhe. Dkt. Lilian Mashaka na kulia ni Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa
Mahakama (IJA) Lushoto, Mhe. Jaji Dkt. Paul Kihwelo.
Washiriki wa Warsha hiyo
wametoka Mahakama ya Tanzania, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa
Serikali, Ofisi ya Mwendesha Mashtaka wa Serikali (DPP), TAKUKURU, TCRA, Ofisi
ya Wakili wa Serikali, na Wizara ya Katiba na Sheria.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni