Mahakama ya Afrika ya
Mashariki imetupilia mbali maombi ya dharura katika Shauri namba 2 la mwaka 2019
lililofunguliwa na Viongozi waandamizi wa vyama vya siasa vya upinzani nchini katika
Mahakama hiyo iliyopo jijini Arusha.
Mahakama imechukua uamuzi huo baada ya upande
wa walalamikaji kumuomba Jaji anayesikiliza kesi hiyo Mhe. Monica Mungenyi
kusikiliza upande mmoja wa walalamikaji kitendo kilichopingwa na mawakili wa
Serikali.
Baada ya kusikiliza
shauri hilo kwa kuzingatia ushahidi uliotolewa na upande wa waleta maombi, Jopo
la waheshimiwa Majaji liliamua kutupilia mbali shauri hilo kwa kile
walichokieleza kuwa upande wa waleta maombi wameshindwa kuthibitisha kwa
Mahakama hiyo umuhimu wa kusikiliza shauri upande mmoja kwani masuala yaliyopo
katika shauri hilo ni muhimu hivyo ili haki itendeke ni vyema upande wa pili
usikilizwe ndipo Mahakama itoe maamuzi.
Kesi hiyo
iliyosikilizwa na Majaji watano wa Mahakama hiyo ambao ni Mhe. Jaji Monica
Mugenyi, Mhe Jaji Faustine Ntezyilyayo, Mhe Jaji Fakihi Jundu, Mhe. Jaji Audace
Ngiye, na Mhe. Jaji Charles Nyachae, ilifunguliwa na viongozi wa vyama vya
siasa wakiongozwa na Mhe. Freeman Mbowe, Mhe. Zitto Zuberi Kabwe, Mhe.Hashimu
Rungwe, Mhe.Seif Sharif Hamad na Mhe.Salum Mwalim kupinga utekelezaji wa sheria
ya vyama vya siasa ya mwaka 2019.
Kufuatia hatua hiyo
waheshimiwa Majaji wameutaka upande wa waleta maombi kuipatia nakala ya maombi
hayo Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali ili kujibu, na tarehe ya kusikiliza
maombi hayo itapangwa hapo baadae.
Katika shauri hilo
upande wa Serikali uliwakilishwa na Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali kupitia
Mawakili wa Serikali Ndg. Evarist M. Mashiba, na Bw. Kombe wakati upande wa
Mashtaka uliwakilishwa na Bi. Fatma Karume, Bw. Jebra Kambole na Ndg, John
Malya.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni