Mahakama ya Tanzania kwa kushirikiana na Shirika
la Haki Miliki Duniani (WIPO), imeendesha mafunzo yenye lengo la kuwajengea
uwezo Mahakimu kuwa na uelewa wa sheria za haki miliki ili kutatua migogoro
mbalimbali.
Akizungumza
wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo mapema Juni 27, 2019, Jaji wa Mahakama ya
Rufani Tanzania, Mhe. Barke Sahel amesema kuwa mafunzo hayo ni ya kipekee kwani
yanafanyika mara ya kwanza nchini hivyo yatasaidia Mahakimu hao kuendesha
mashauri yanayohusiana na Hakimiliki kwa weledi hatua itakayosaidia kutoa haki kwa
wakati.
Aidha
Mhe Jaji huyo ameongeza kuwa mafunzo hayo pia yatawasadia Mahakimu hao kupata
uelewa wa ujumla katika mambo yote yanayohusiana na Hakimili hasa katika
kipindi hiki ambacho Tanzania inapiga hatua kubwa katika sekta ya viwanda.
“Sasa
hivi tunapoelekea kwenye nchi ya viwanda watu wengi wanakuwa wameendeleza
mawazo yao (Patent Rights) kwa maana hiyo changamoto au migogoro lazima
itajitokeza, hivyo ni vyema waheshimiwa Mahakimu kupatiwa uelewa wa kutosha
utakaowasaidia kushughulikia migogoro hiyo kwa haki na kwa wakati”. Alisema Mhe
Jaji Saleh.
Akizungumzia
uamuzi wa Mahakama ya Tanzania kuendesha mafunzo hayo, Jaji Mstaafu wa Mahakama
Kuu Mhe. Robert Makaramba amesema kuwa mafunzo haya ni muhimu kwa kuzingatia
ukweli kuwa eneo hili la Haki miliki ni eneo ambalo halieleweki kwa watu wengi
sana ikiwa ni pamoja na Mahakimu.
“Sasa
hivi mashauri ya Hakimiliki yanaanza kuongezeka hasa baada ya Tanzania kuanza
kutekeleza sera yake ya kuwa nchi ya viwanda na uchumi wa kati ifikapo mwaka
2025, hatua hii itapelekea kuwepo kwa mashauri ya kugombea Hakimiliki za
uandishi, za viwanda na zile za alama za kufanyia biashara, hivyo kupitia
mafunzo haya Mahakimu wataweza kutatua migogoro hiyo kwa urahisi. Alieleza Jaji
huyo.
Katika
hatua nyingine Mwakilishi wa Shirika la Haki Miliki Duniani (WIPO), Mheshimiwa
Alexandra Bhattacharya, amesema kuwa baada ya mafunzo haya Mahakama itakuwa
kiungo muhimu katika kuhakikisha Haki
Miliki za wananchi zinalindwa kwani itawezesha kutatua migogoro yote kwa usawa na haki pasipo
na upendeleo.
Naye Mratibu wa mafunzo, Hakimu Mkazi ambaye pia ni Msaidizi wa Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Upendo Ngitiri amesema
uwepo wa Haki Miliki ni muhimu kwani utaongeza chachu katika ukuaji wa
tekinolojia hata katika ukuaji wa sekta ya viwanda nchini hatua itakayosaidia
ukuaji wa uchumi kwa ujumla katika Nyanja mbalimbali.
Katika
Mafunzo hayo Washiriki watapata pia fursa ya kubadilishana uzoefu na kujifunza
zaidi juu ya mfumo wa haki miliki Kimataifa, mfumo wa kimataifa wa ulinzi wa
hakimiliki na jukumu la Mahakama katika kulinda na kuimarisha haki miliki na
uzoefu juu ya utatuzi wa haki hizo.
Mafunzo
hayo ya siku mbili yanafanyika katika Kituo cha mafunzo kilichopo katika
viwanja vya Mahakama ya Hakimu Mkazi kisutu na yamewahusisha Mahakimu kutoka
katika vituo vya mikoa ya Dar es Salaam, Pwani pamoja na Morogoro.
Jaji wa Mahakama ya
Rufani ya Tanzania ambaye pia alikuwa Mgeni rasmi, Mhe. Barkel Sahel akifungua
rasmi Mafunzo ya siku mbili ya Haki Miliki yanayofanyika katika Kituo cha
Mafunzo cha Mahakama kilichopo eneo la Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Jijini Dar es Salaam.
Sehemu ya Waheshimiwa
Mahakimu wakifuatilia hotuba ya ufunguzi wa mafunzo hayo.
Msajili Mkuu-Mahakama
ya Tanzania, Mhe. Katarina Revocati
akitoa neno kabla ya kumkaribisha rasmi Mgeni rasmi kufungua Mafunzo hayo.
Mwakilishi wa Shirika
la Haki Miliki Duniani (WIPO), Mheshimiwa Alexandra Bhattacharya akitoa mada ya
haki miliki kwa washiriki wa Mafunzo.
Jaji wa Mahakama ya
Rufani (T) ambaye alikuwa mgeni rasmi, Mhe Barke Sahel (aliyeketi katikati) akiwa katika picha wa pamoja na Washiriki wa Mafunzo ya siku mbili (2) ya Haki Miliki (waliosimama), aliyeketi wa pili kulia ni Jaji Msataafu wa Mahakama Kuu, Mhe. Robert Makaramba, wa pili kushoto ni Msajili Mkuu wa Mahakama ya
Tanzania, Mhe. Katarina Revocati, wa kwanza kulia ni Naibu Msajili kutoka BRELA, Bi. Loy Mhando na wa kwanza kushoto ni Mwakilishi wa Shirika
la Haki Miliki Duniani (WIPO), Bi. Alexandra Bhattacharya.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni