Na Waandishi, Mahakama
Jaji Mkuu wa Tanzania,
Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma leo amewaapisha Wasaidizi wa Sheria wa Majaji
kuwa Mahakimu Wakazi na kuwataka kutoa maamuzi yatakayoielimisha jamii.
Akizungumza baada ya
kuwaapisha Mahakimu Wakazi 53 Juni 18 mwaka huu Jaji Mkuu pia amewataka Mahakimu hao kuandika hukumu
zinazoeleweka, zinazosomeka, zenye lugha nyepesi, pamoja na kutoa hukumu hizo
kwa wakati.
“Uamuzi wowote mtakaoutoa
kuanzia siku ya kwanza Mahakamani utagusa Uhai, Mali na Hali ya wanadamu
wengine, hivyo kosa lolote la kimaamuzi mtakalotoa litakuwa na gharama pamoja
na gharama ya muda kwa nchi, kwa watu, na kwa familia kwa ujumla”, alisema.
Aidha, Jaji Mkuu
amewataka Mahakimu wapya kufanya kazi kwa kuzingatia maadili, umakini na
unyenyekevu kwa kuwa kazi hiyo inahitaji uangalizi wa hali ya juu. Aliwataka
Mahakimu hao pia kuwasaidia watanzania kuhusu masuala ya kisheria hususan
wanawake na watoto.
Akizungumzia vitendo
vya rushwa Mahakamani, Prof. Juma alisema bado Mahakama haizungumziwi vizuri
katika suala hilo hivyo aliwataka Mahakimu hao kutoogopa kulizungumzia tatizo
hilo, na kupanga mikakati ya kukabiliana nayo.
“Rushwa ni kitu kinachojificha, pangeni
mikakati ya kupambana nayo. Someni ripoti ya Jaji Warioba ya mwaka 1996 ili
muelewe ni wapi rushwa imejificha”, alisema.
Aidha, Jaji Mkuu
alivitaja viashiria vya rushwa ndani ya Mahakama kuwa ni katika maeneo ya
kufungua mashauri, kupanga tarehe za mashauri, utafutahji wa majalada, na
utoaji wa nakala za hukumu. Aliwataka Mahakimu hao kuhakikisha wanatoa nakala
za hukumu kwa wakati ili wasihusishwe na dhana ya rushwa.
Alisema Mahakimu ni nyara
ya Mahakama hivyo hawana budi kujenga taswira nzuri ya Mahakama kwani kwa
kutofanya hivyo nchi nzima itachafuka. Aliongeza kuwa ni muhimu kwa Mahakimu
kuheshimiana na kuheshimu kada nyingine kwa kuwa hakuna kada muhimu zaidi ya
nyingine.
“Sauti yako ni sauti ya
umma lazima itoke kwa juu, usimfokee mtu Mahakamani,” alisisitiza.
Nao Mahakimu
walioapishwa kwa ujumla wao wameonyesha kufurahishwa na hatua hiyo na kuahidi
kufanya kazi kwa uadilifu na kuahidi kutoa huduma bora kwa wananchi.
Kabla ya kuapishwa
rasmi, Mahakimu hawa walikuwa wakihudumu katika ngazi ya Mahakama ya Rufani na
Mahakama Kuu kama Wasaidizi wa Sheria wa Majaji kwa takribani miaka tisa (9).
Mahakimu hawa ambao
tayari wameshapangwa katika vituo mbalimbali wataongeza nguvu kazi ya kupunguza
mlundikano wa mashauri.
Jaji Mkuu wa Tanzania,
Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (aliyesimama) akiwaapisha rasmi waliokuwa
Wasaidizi wa Sheria wa Wahe. Majaji kuwa Mahakimu Wakazi mara ya kubadilishwa
Kada. Hafla ya uapisho imefanyika mapema Juni 18, 2019 katika Ukumbi namba moja
(1) wa Mahakama Kuu- Dar es Salaam. Kushoto ni Jaji Kiongozi-Mahakama Kuu ya
Tanzania, Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi na kulia ni Jaji Mfawidhi, Mahakama
Kuu-Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Beatrice Mutungi.
Pichani ni Wahe.
Mahakimu wakila kiapo mbele ya Mhe. Jaji Mkuu (hayupo pichani).
Utiaji saini ukiendelea
mara baada ya kiapo.
Mhe. Jaji Mkuu
(katikati) akimzungumza na Wahe. Mahakimu wapya mara baada ya kuwaapisha rasmi.
Wahe. Mahakimu
walioapishwa wakimsikiliza Mhe. Jaji Mkuu alipokuwa akizungumza nao mara baada
ya kuwaapisha rasmi.
Baadhi ya Watendaji,
Wasajili, Watumishi pamoja wageni waliohudhuria katika hafla hiyo iliyofanyika
mapema Juni 18, 2019.
Jaji Mkuu wa Tanzania,
Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (aliyeketi katikati) akiwa katika picha ya
pamoja na Wahe. Mahakimu wapya walioapishwa, kushoto waliokaa ni Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi, na kulia ni
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam na wa kwanza kushoto ni
mmoja wa Mahakimu wapya walioapishwa, Mhe. Amos Rweikiza.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni