Waziri wa Katiba na
Sheria Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga amepokea ripoti zenye mapendekezo ya
kurekebisha sheria tatu kutoka Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania.
Ripoti zilizopokelewa
ni pamoja na ile ya Kurekebisha Sheria ya Ufilisi, Sheria ya Ushahidi na Sheria
ya eneo la Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro. Mwenyekiti wa Tume ya
Kurekebisha Sheria Tanzania Jaji Mstaafu Mhe. Januari Msoffe aliwasilisha
ripoti hizo jana katika ofisi za wizara zilizopo kwenye mji wa Serikali, Mtumba
jijini Dodoma.
Aidha, ripoti hizo zimeainisha
maeneo ambayo yanahitaji kufanyiwa marekebisho kuwa ni pamoja na eneo la ulipishwaji
wa faini ndogo, Lugha ngumu isiyoeleweka kwa urahisi, matumizi yasiyo sahihi ya
ardhi ikiwemo usajili wa vijiji kwenye eneo la hifadhi.
Akizungumza baada ya
kupokea ripoti hizo, Waziri Mahiga alisema katika eneo la utoaji ushahidi
mahakamani ni vizuri kwa sasa Tanzania ikaanza kupokea ushahidi kwa njia ya
video ili kurahisisha utoaji wa ushahidi kutoka sehemu mbalimbali pasipo
shahidi kuwepo Mahakamani.
“Suala hili linaweza
kufanikiwa kwa kushirikiana na balozi mbalimbali ambazo zinaonekana kuunga mkono
utawala wa sheria uliopo nchini kwa kuchangia vifaa na kutoa mafunzo kwa
watendaji”, alisema Waziri Mahiga.
Aidha, balozi Mahiga aliipongeza
Tume ya Kurekeisha sheria kwa kazi kubwa na nzuri wanayofanya ya utafiti wa
Sheria kabla ya kutoa mapendekezo ambayo yanawezesha sheria mbalimbali
kurekebishwa na kuendana na wakati.
Waziri Mahiga pia alisifu
utawala wa sheria uliopo nchini ambao Tume ya Kurekebisha Sheria imesaidia
uwepo wa Utawala huo.
“Utawala wa Sheria ili
uwe rahisi ni vizuri kuwa na Tume ambayo inapitia na kufanyia tafiti Sheria
mbalimbali”, alisema Balozi Mahiga.
Naye Mwenyekiti wa Tume
ya Kurebisha Sheria alisema kazi ya utafiti wa sheria nchini ni miongoni mwa
majukumu ya Tume yake na kazi hiyo hufanyika ili kuzifanya sheria ziendane na
wakati.
Alisema taasisi
mbalimbali za Serikali zinazosimamia sheria husika huiomba Tume ya kurekebisha
Sheria kuzipitia na baada ya kuzifanyia utafiti na kubaini mapungufu, hutoa mapendekezo
ambayo huwasilishwa serikalini na baadaye bungeni kwa ajili ya kuzirekebisha.
Waziri wa Katiba na
Sheria Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga akipokea ripoti kutoka kwa Mwenyekiti wa
Tume ya Kurekebisha Sheria Jaji Mstaafu Mhe. Januari Msoffe kuhusu Marekebisho
ya Sheria jana jijini Dodoma.
Mwenyekiti wa Tume ya Kurekebisha Sheria Jaji Mstaafu Mhe. Januari Msoffe akimwelezea jambo Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga wakati wa makabidhiano ya ripoti tatu kuhusu Marekebisho ya Sheria jana jijini Dodoma.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni