Ijumaa, 28 Juni 2019

MAHAKIMU WAASWA KUJIENDELEZA


NA MAGRETH KINABO NA DENNIS BUYEKWA

JAJI Mstaafu wa Mahakama Kuu, Mhe. Robert Makaramba, amewataka Mahakimu Wakazi   kuwa na tabia ya kujiendeleza kielimu kuhusiana na  masuala ya haki na Haki Miliki ili kuweza kufanya kazi zao kwa uweledi.

Hayo yalisemwa na  Jaji Makaramba  leo  wakati  akifunga  mafunzo ya siku mbili kuhusu Haki Miliki kwa mahakimu hao,  yaliyofanyika  katika kituo cha Mafunzo kilichopo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu iliyopo jijini Dar es Salaam, yaliyotolewa na Mahakama ya Tanzania kwa kushirikiana na Shirika la Haki Miliki Duniani(WIPO).

“Kutokana kuwepo kwa dunia ya utandawazi ni vizuri mkawa na tabia ya kujiendeleza kwa kusoma vitu mbalimbali kuhusiana na masuala ya Haki pamoja na Haki Miliki kwa kutumia simu za mkononi na mitandao ya kijamii hususan wa  Umoja wa Mataifa unaoshughulikia masuala ya Haki Miliki  na masuala ya alama ya biashara  ili kuweza  kutoa haki kulingana na wakati, badala ya kusubiri mafunzo,” alisema  Jaji Makaramba.

 Aliongeza kuwa hivi sasa Tanzania iko katika uchumi wa viwanda, tunategemea na kuwa na migogoro mfano bidhaa feki au kughushi bidhaa, hivyo ni vema Mahakama ikiwa na uelewa mpana kuhusu mambo yanayohusu Haki Miliki  ili kuweza kufanya maamuzi kwa haraka na weledi.

 Jaji  Makaramba  pia aliwataka mahakimu hao kuwa walimu kwa wenzao kwa kuwa mahakimu wenye elimu hiyo ni wachache, huku akisisitiza kwamba  kuna haja mafunzo hayo yakatolewa kwa wadau wengine wanaohusiana  na kesi za  hati miliki, ambao ni mawakili wa Serikali  na  kujitegemea, wakiwemo watunga sera.

Akizungumza wakati wa kutoa neno la shukurani, Hakimu Mkazi, Elimo Massawe kwa niaba ya wenzake alisema wanaishukuru Mahakama ya Tanzania kwa kushirikiana na WIPO kuratibu Mafunzo hayo, ambayo yatawasaidia  katika utatuzi wa kesi zinazohusu Hakii miliki.

Mafunzo hayo yamehuhusisha  jumla ya Mahakimu 30 kutoka katika mikoa ya  Dar es Salaam, Morogoro na Pwani.



 Jaji Mstaafu wa  Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Robert Makaramba akizungumza wakati wa kufunga mafunzo ya siku mbili yanayohusu Hakimiliki. Mafunzo yaliyowashilikisha Mahakimu 30 yalifanyika katika kituo cha mafunzo kilichopo katika viwanja vya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu iliyopo Jijini Dar es Salaam.

Hakimu Mkazi Mhe. Elimo Massawe akitoa neno la shukrani mara baada ya mafunzo hayo kumalizika ambayo yamefanyika katika kituo cha mafunzo kilichopo katika viwanja vya mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

 Hakimu Mkazi Mhe. Samwel Mushumbusi, akimfafanulia jambo  Mwakilishi wa Shirika la Hakimiliki Duniani Mhe. Alexandra Bhattacharya wakati mafunzo hayo yakiendelea.
 Mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo akisoma maazimio yaliyofikiwa wakati wa mafunzo hayo yaliyofanyika katika kituo cha mafunzo kilichopo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Jijini Dar es Salaam.

Jaji Mstaafu wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Robert  Makaramba(katikati), akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa mafunzo hayo ya siku mbili yaliyofanyika katika kituo cha mafunzo kilichopo katika viwanja vya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni