Jumanne, 2 Julai 2019

JAJI MKUU MSTAAFU: KIONGOZI ALIYELETA MABADILIKO NDANI YA MAHAKAMA




Na Lydia Churi-Mahakama
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amemuelezea Jaji Mkuu Mstaafu Mhe. Mohamed Chande Othman kuwa ni Kiongozi aliyeleta mageuzi makubwa ndani ya Mahakama hasa katika kuongeza uwajibikaji kwa watumishi.

Akizungumza kwenye hafla maalum ya kumuaga kitaalum Mhe. Chande iliyofanyika mapema Julai 02, 2019  jijini Dar es salaam, Jaji Mkuu alisema, miongoni mwa mageuzi makubwa aliyoyaanzisha Jaji Chande ni pamoja na kuweka mkakati wa kuhakikisha kesi zinamalizika kwa wakati Mahakamani. 

Kwa mujibu wa Jaji Mkuu, mkakati huo ni pamoja na kupanga idadi ya mashauri yanayotakiwa kusikilizwa na kumalizwa na Wahe. Majaji na Mahakimu pamoja na muda wa mashauri hayo kukaa kwenye Mahakama mbalimbali. Alisema kupitia mkakati huo, Majaji wanatakiwa kumaliza jumla ya mashauri 220 na Mahakimu mashauri 250 katika kipindi cha mwaka moja.

Kuhusu muda wa mashauri kukaa Mahakamani, mashauri katika Mahakama ya Rufani na Mahakama Kuu yanapaswa kumalizika ndani ya miaka miwili na katika Mahakama za Hakimu Mkazi na Mahakama za wilaya yanatakiwa kumalizika  ndani ya miezi 12 wakati kwenye Mahakama za Mwanzo shauri linapaswa kumalizika ndani ya miezi sita.

Mhe. Prof. Juma pia alisema Jaji Mhe. Chande ndiye aliyeanzisha mabadiliko ndani ya Mahakama kwa kusimamia kuandaliwa kwa Mpango Mkakati wa Miaka mitano wa Mahakama ya Tanzania (2015/16 hadi 2019/20), mpango utakaotatua changamoto mbalimbali zinazoukabili Mhimili wa Mahakama ikiwemo uhaba na uchakavu wa majengo ya Mahakama nchini.

Alisema kuwa Mpango Mkakati wa Mahakama ya Tanzania unatoa mwelekeo wa nini cha kufanya ili kufikia upatikanaji wa haki kwa wakati. Aliongeza kuwa mpango huo pia umewezesha Mahakama kuwa karibu zaidi na wadau wake na kusaidia mashauri kumalizika kwa wakati. 

Kwa upande wake, Jaji Mkuu Mstaafu amesema vitendo vya rushwa ndani ya Mhimili wa Mahakama huweza kuhatarisha uhuru wa Mahakama na hivyo kuwataka watumishi kujiepusha na vitendo hivyo ili kujenga taswira nzuri kwa Mhimili huo.

Mhe Chande alisema katika kipindi cha uongozi wake, Mahakama iliweza kufanya mabadiliko makubwa ikiwemo kuanzishwa kwa miradi mingi ya ujenzi wa majengo ya Mahakama, na kuanzishwa kwa mfumo wa kuratibu malalamiko.

Hafla ya kumuaga rasmi kitaaluma Jaji Mkuu Mstaafu wa Tanzania ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Mahakama na Serikali wakiwemo Majaji wa Mahakama ya Rufani, Majaji wa Mahakama Kuu, Majaji wastaafu, Mkurugenzi wa Mashitaka, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Katibu Mkuu Kiongozi, Mawaziri Wakuu wastaafu  Mawaziri, Manaibu Wasajili na Watendaji wa Mahakama.  

Mhe. Mohamed Chande Othman aliteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania tarehe 16 Agosti 2004 na tarehe 6 Februari 2008 alipandishwa kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani. Aidha, tarehe 2 Disemba 2010 aliteuliwa kuwa Jaji Mkuu wa Tanzania, nafasi aliyoishika hadi alipofikia umri wa kustaafu kwa mujibu wa Katiba  tarehe 17 Januari 2017.
Bendi kutoka Jeshi la Magereza Tanzania ikiongoza maandamano wakati wa sherehe za kumuuaga Jaji Mkuu Mstaafu wa Tanzania Mhe. Mohamed Chande Othman.
 Jaji Mkuu Mstaafu Mhe. Mohamed Chande Othman pamoja na Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe.Profesa Ibrahim Hamis Juma wakiwa katika maandamano ya sherehe za kumuaga Jaji Mstaafu huyo wakielekea ukumbi namba moja wa Mahakama Kuu ya Tanzania nyuma yao ni Majaji wa Mahakama ya Rufani.
 Jaji Mkuu Mstaafu Mhe.Profesa Ibrahim Hamis Juma, akihutubia wakati wa hafla ya kumuaga Jaji Mstaafu  huyo.
 Jaji Mkuu Mstaafu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Mohamed Chande Othman (wa tatu kushoto) akitoa hotuba yake wakati wa sherehe ya kumuaga kitaaluma iliyofanyika leo katika ukumbi namba moja uliopo katika Mahakama Kuu ya Tanzania, kulia kwakwe ni Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe, Profesa. Ibrahim Hamis Juma akifutilia kwa makini hotuba hiyo.
 Naibu Wakili Mkuu wa Serikali Dkt. Ally Possi akisoma hotuba kwa niaba ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali wakati wa hafla fupi ya kumuaga kitaaluma Jaji Mkuu mstaafu Mhe Mohamed Chande Othman.
 Msajili Mkuu wa Mhakama ya Tanzania Mhe. Katarina Revocati akitoa maelezo mafupi kuhusiana na hafla ya kumuuaga Jaji Mkuu mstaafu wa Tanzania Mhe. Mohamed Othman Chande.
 Jaji Mkuu Mstaafu wa Tanzania, Mhe.Mohamed Chande Othman (wanne kushoto walioketi)  pamoja na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Profesa Ibrahim Juma(wa tano kulia walioketi), wakiwa katika picha ya pamoja na Majaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania mara baada ya hafla ya kumuuaga kitaaluma Jaji Mkuu Mstaafu  Mhe. Othman. Hafla hiyo imefanyika leo katika ukumbi namba moja wa Mahakama Kuu ya Tanzania
 Jaji Mkuu Mstaafu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Mohamed Chande Othman (wa tatu kushoto) na mkewe (wa pili kushoto) pamoja na Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe.Profesa Ibrahim Hamis Juma wakiwa katika picha ya pamoja na mawakili mara baada ya hafla ya kumuuaga Jaji Mstaaafu huyo, wa kwanza kulia ni Waziri Mkuu Mstaafu Mhe.  Mizengo Pinda, na wa kwanza kushoto ni Rais wa Chama cha  wanasheria wa Tanganyika Dkt. Rugemeleza Nshalla
 Jaji Mkuu Mstaafu wa Tanzania Mhe. Mohamed Chande Othman, akifurahia jambo na Katibu Mkuu Kiongozi Dkt. John Kijazi mara baada ya hafla hiyo.

Jaji Mkuu Mstaafu wa Tanzania Mhe. Mohamed Chande Othman (wa nne kushoto) pamoja na Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Profesa.Ibrahim Hamis Juma (wa tano),  wakiwa katika picha ya pamoja na Majaji wa Mahakama ya Rufani (walioketi) pamoja na  Majaji Wastaafu (walio simama).

(Picha na Mary Gwera na Dennis Buyekwa).

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni