Jumatano, 3 Julai 2019

TANZANIA YAWA MWENYEJI WA MKUTANO WA SHIRIKA LA HAKI MILIKI DUNIANI (WIPO)


Na Mary Gwera, Mahakama

Jumla ya Washiriki 35 kutoka Mataifa mbalimbali duniani ikiwemo Tanzania wanashiriki katika Mkutano na Mafunzo ya Miliki Bunifu/Haki Miliki yanayoratibiwa na Shirika la Miliki Bunifu Duniani (WIPO) na Serikali ya Tanzania.

Akizungumzia Mafunzo hayo Julai 03, 2019, Mwakilishi kutoka Mahakama ya Tanzania, ambaye ni Hakimu Mkazi na Msaidizi wa Msajili Mkuu, Mahakama ya Tanzania, Mhe. Upendo Ngitiri alisema kuwa Mkutano huo unalenga kupata maendeleo ya Miradi mbalimbali inayoendelea inayohusiana na masuala ya Haki Miliki ambayo imeanzishwa na Washiriki walioteuliwa na WIPO.

“Moja ya malengo ya Mkutano huu ambao umeshirikisha Maafisa Waandamizi kutoka nchi zilizoshiriki ni pamoja kupata taarifa za maendeleo pamoja na uzoefu wa kila nchi juu ya masuala ya Haki Miliki,” alisema Mhe. Ngitiri.

Akiwasilisha mada katika  Mkutano huo; Mhe. Ngitiri aliwaeleza Washiriki kuwa kwa upande wake yeye kama Mratibu wa masuala ya Haki miliki ameanzisha Mradi unaolenga kutoa Mafunzo na kujenga uelewa kwa Mahakimu kuhusiana na masuala ya Haki Miliki  kwa kuwa uelewa juu ya suala hili ni mdogo.

Aliongeza kuwa , Mahakama ya Tanzania kwa kushirikiana na WIPO kwa mara ya kwanza imewapatia Mafunzo ya Haki miliki jumla ya Mahakimu 30 ambayo yatawawezesha kuamua bora zaidi mashauri yanayohusiana na haki miliki yaliyofanyika Juni 27 na 28, 2019.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Shirika la Haki Miliki Duniani (WIPO), Bi. Alexandra Bhattacharya amepongeza jitihada za Mratibu wa Tanzania, Mhe. Upendo Ngitiri kuwezesha Tanzania kushirikiana na Shirika hilo katika utoaji elimu ya haki miliki.

Mkutano huo wa siku saba (7) unaofanyika katika Hoteli ya Hyatt Regency jijini Dar es Salaam umeshirikisha Washiriki kutoka Sweden, Switzerland, Nepal, Cambodia, Rwanda, Uganda, Mozambique, Zambia, Malawi, Burtan, Ethiopia n.k.

Washiriki wa Mkutano watapata fursa ya kubadilishana uzoefu kutoka katika maeneo wanayotoka kwa manufaa ya kila mshiriki kupata elimu na kujifunza namna bora zaidi ya ushughulikiaji wa masuala ya Haki Miliki.
 Mratibu wa Mradi wa Uhamasishaji na Utoaji Elimu ya Haki Miliki ambaye pia ni Hakimu Mkazi na Msaidizi wa Msajili Mkuu-Mahakama ya Tanzania, Mhe. Upendo Ngitiri akiwasilisha Mada katika Mkutano na Mafunzo ya Miliki Bunifu/Haki Miliki yanayoratibiwa na Shirika la Miliki Bunifu Duniani (WIPO) na Serikali ya Tanzania.
 Mkurugenzi wa Shirika la Haki Miliki (WIPO) Kanda ya Nchi zinazoendelea, Bw. Kifle Shenkoru pamoja na Mwakilishi wa Shirika la WIPO, Bi. Alexandra Bhattacharya wakifuatilia mada katika Mkutano huo.

Washiriki kutoka nchi mbalimbali wakiwa katika Mkutano huo.

Prof. Bed Mani kutoka Nepal akiwasilisha Mada katika Mkutano/mafunzo.
 
 



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni