Alhamisi, 22 Agosti 2019

JAJI KIONGOZI AWATAKA WATUMISHI WA MAHAKAMA-KIGOMA KUWA MAHIRI


Na Festo Sanga, Mahakama ya Hakimu Mkazi-Kigoma

Jaji Kiongozi -Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi amewaasa Watumishi wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma kujenga umahiri na maarifa kwa kuwa ni silaha katika utendaji kazi wa utumishi wa umma. 

Mhe. Jaji Dkt. Feleshi  alisema  hayo  hivi karibuni alipofanya ziara  iliyoanza Agosti 19, mwaka 2019 hadi Agosti 20, mwaka 2019  katika  Mahakama  Kuu Kanda ya Kigoma kwa ajili ya kukagua jengo la Mahakama  Kuu  Kanda ya Kigoma  na ujenzi wa  nyumba za Majaji, ikiwemo kuzungumza  na watumishi.

“Jengeni umahiri, uadilifu na maarifa kwani ndivyo vitakavyowanyanyua popote mlipo kwenda ngazi nyingine”.  alisema Jaji Kiongozi. Aliongeza kwa kuwaeleza watumishi hao kuwa kila mmoja ni muhimu na ana mchango katika utendaji kazi wa shughuli za Mahakama.

Hata hivyo Jaji Kiongozi alifarijika kuona muungano mzuri wa watumishi wa Mahakama Kanda ya Kigoma kwa jinsi wanavyofanya kazi baada ya kupokea taarifa ya utendaji kazi iliyotolewa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Mhe Ilvin Mugeta.

Aliwasisitiza watumishi  hao,  kutoa huduma bora ili kuongeza kiwango cha kuridhisha cha wateja, ikiwa ni utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Miaka Mitano(2015/2016-2019/2020)  wa Mahakama ya Tanzania hususani  nguzo ya tatu inayolenga kurejesha Imani kwa Jamii na Ushirikishwaji wa Wadau katika shughuli za Mahakama.

Aidha katika ziara yake, Mhe. Jaji Kiongozi alipongeza jitihada na kasi inayofanywa katika ujenzi wa jengo la Mahakama Kuu pamoja na nyumba za makazi za Wahe. Majaji ambazo zinajengwa na  Mkandarasi wa Masasi Construction Co Ltd.
 Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt.Eliezer  Feleshi akisalimiana na  baadhi ya watumishi wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma mara baada ya kuwasili  katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kigoma.
 Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe.Dkt. Eliezer Feleshi (katikati) akipitia kwa umakini taarifa ya utekelezaji wa shughuli za Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma iliyowasilishwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma, Mhe. Ilvin Mugeta (aliyesimama).
 Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi (katikati) akipata ufafanuzi unaohusu jengo la   Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma kutoka kwa Mkandarasi wa Masasi Construction Co Ltd Mhandisi  Slyvester Mbawala, wakati alipotembelea jengo hilo.
 Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi, (wa pili kulia) akikagua  nyumba za makazi za Wahe. Majaji wa Mahakama Kuu, Kanda ya Kigoma.

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi (wa tatu kushoto) akiwa katika picha ya pamoja  na baadhi ya viongozi wa Mahakama,wakiwemo wakandarasi wa Masasi Construction.








Hakuna maoni:

Chapisha Maoni