Jumatatu, 19 Agosti 2019

MAHAKIMU NA WADAU WA MAHAKAMA KANDA YA MOSHI WAPATIWA MAFUNZO YA KUWAJENGEA UWEZO


Na Paul Mushi – Mahakama Kuu-Moshi
Mahakimu na Wadau wa Mahakama Kanda ya Moshi wameanza mafunzo maalumu ya kuwajengea ujuzi zaidi wa kushughulikia mashauri ya watoto katika Mahakama za Watoto.

Mafunzo hayo yanayoratibiwa na kuendeshwa na Chuo cha Uongozi wa Mahakama-Lushoto (IJA) yameshirikisha jumla ya Washiriki 45 ambao ni Mahakimu na Wadau wa Mahakama wakiwemo Waendesha Mashtaka wa Polisi (PP), Ofisi ya Mashtaka ya Serikali, Maafisa Ustawi wa Jamii.

Akifungua Mafunzo hayo mapema leo (Agosti 19, 2019), Jaji Mfawidhi-Mahakama Kuu Kanda ya Moshi, Mhe. Jaji Dkt. Fauz Twaib amesema, “Najisikia furaha kupatiwa fursa hii, pia natumaini lengo la mafunzo haya ni kuwapatia ujuzi na maarifa zaidi ya kutafsiri na kutekeleza Sheria ya Watoto nambari 21 ya Mwaka 2009 (Law of the Child Act No. 21 of 2009)”.

Sambamba na hayo Mhe. Jaji Mfawidhi amewasisitiza washiriki kupitia Sheria zote zinazohusiana na watoto ili kuongeza ufanisi baada ya kukamilisha mafunzo hayo yatakayotolewa ikiwa ni pamoja na kuweka katika vitendo maarifa watakayoyapata katika mafunzo hayo.

Mafunzo hayo ya siku tano (5) yanayofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Chuo cha Mafunzo na Ufundi Stadi (VETA) Moshi yanatarajiwa kuhitimishwa rasmi Agosti 23, 2019.
 Jaji Mfawidhi-Mahakama Kuu, Kanda ya Moshi, Mhe. Dr Fauz Twaib akifungua mafunzo maalumu ya kuwajengea uwezo Mahakimu na Wadau wa Mahakama Kanda ya Moshi kuhusu Mashauri ya Watoto.

Washiriki wakimsikiliza Mhe. Jaji Mfawidhi (hayupo pichani) wakati akifungua rasmi Mafunzo hayo.

Picha ya pamoja na Wahe. Mahakimu wanaoshiriki katika mafunzo hayo.
 Picha ya pamoja na Wadau.

 
 


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni