Na
Lydia Churi- Mahakama Njombe
Jaji Mkuu wa Tanzania
Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma leo ameanza ziara ya kikazi katika mikoa ya
Iringa na Njombe na kutaka kuwepo kwa matumizi ya vipimo vya vinasaba (DNA) katika
kesi za mauaji, ubakaji na unajisi kwa watoto ili kurahisisha uendeshaji wa
kesi hizo na kusaidia haki kupatikana kwa wakati.
Akizungumza na Mkuu wa
Mkoa wa Njombe Mhe. Christopher Ole Sendeka alipomtembelea ofisini kwake, Jaji
Mkuu amesema matumizi ya vipimo vya DNA katika kesi yatasaidia haki kupatikana ambapo
aliyetenda kosa atatiwa hatiani na asiyetenda kosa ataachiwa mapema.
“Kipimo cha DNA husaidia kuthibitisha
kosa lililofanyika lakini bahati mbaya, kwa uzoefu wetu hatuoni matumizi ya kipimo
hicho”, alisema Jaji Mkuu.
Alisema kutokutumika kwa kipimo
cha DNA Mahakamani, mshtakiwa huweza kuachiwa huru kutokana na kukosekana kwa
ushahidi.
“Eneo hili tumeona huweza
kusababisha mtuhumiwa kuachiwa huru kwa sababu sisi tunaangallia zaidi ushahidi”
alisisitiza Jaji Mkuu.
Alisema wakati mwingine Jaji
au Hakimu huweza kuona wazi kuwa mshtakiwa alistahili kutiwa hatiani lakini
ushahidi unapokosa uzito mtuhumiwa huachiwa huru.
Akifafanua, Jaji Mkuu Alisema
kesi kama hizi huchukua muda mrefu na kusababisha wakati mwingine ushahidi muhimu
kufifia kiasi kwamba kesi inapofika mahakamani lile joto la ushahidi
lililoonekana wakati wa tukio huweza kupotea.
Alisema kutokana na kukua
kwa sayansi na Teknolojia hivi sasa hatua kubwa imefikiwa katika matumizi ya kipimo
cha DNA na kurahisisha sana. Akitolea mfano wa kesi ya ubakaji au unajisi kwa
watoto wadogo alisema badala ya kumuhoji mtoto mdogo mahakamani, kipimo hiki huweza
kutumika ili kuthibitisha kosa lililofanyika.
Alisema Serikali kwa
kushirikiana na Mahakama hawana budi kuifanyia kazi changamoto hii ili kila
raia anayetenda kosa atiwe hatiani na asiye na kosa aachiwe huru mapema hata
katika hatua ya upelelezi wa kesi husika.
Wakati huo huo, Jaji Mkuu alisema suala la
ujazaji wa fomu za taarifa ya Daktari yaani PF 3 halizingatiwi kwa kuwa fomu hizo
hazijazwi kwa ufasaha na hivyo huweza kusababisha mtuhumiwa kuachiwa huru
wakati mwingine.
“Fomu hii inayo maeneo
muhimu ya kujazwa na hasa yanayohitaji vipimo na endapo itajazwa kwa ufasaha itasaidia
sana katika kuhakikisha mtu anayetenda kosa anatiwa hatiani”, alisema.
Kuhusu kesi za Mirathi,
Jaji Mkuu alisema eneo hili lina changamoto kwa kuwa kesi hizi pia huchukua muda
mrefu zaidi hivyo elimu haina budi kutolewa hasa kwa wananchi wanaoishi maeneo
ya vijijini. Alisema wananchi wanatakiwa kufahamu kuwa kila mtu anapaswa kujitahidi
kutafuta chake badala ya kutegemea cha marehemu.
Naye Mkuu wa Mkoa wa
Njombe alimpongeza Jaji Mkuu wa Tanzania kwa kujitoa kwake katika kuhakikisha
Mahakama inatoa mchango mkubwa kwenye maendeleo ya nchi na pia alimpongeza kwa
kuendeleza ushirikiano na Mihimili ya Serikali na Bunge.
Aidha, Mhe. Ole Sendeka ameahidi
kushirikiana kwa karibu zaidi na Mahakama ya Tanzania inapotekeleza majukumu
yake ya msingi ya utoaji wa haki kwa wakati.
Katika ziara iliyoanza
leo, Jaji Mkuu ametembelea Mahakama ya wilaya ya Makete na kuzungumza na watumishi
wa Mahakama hiyo lakini pia alipata nafasi ya kukagua ujenzi wa jengo la
Mahakama ya Mwanzo Makete.
Mkuu wa Mkoa wa Njombe Mhe. Chistopher Ole Sendeka akiangalia kitabu cha Mpango wa miaka mitano wa ujenzi wa Majengo ya Mahakama baada ya kukabidhiwa na Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma.
Jaji
Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akisalimianana Kamati ya Ulinzi
na Usalama ya Mkoa wa Njombe alipowasili mkoani humo kuanza ziara ya kukagua
shughuli za Mahakama.
Mkuu wa Mkoa wa Njombe Mhe. Chistopher Ole Sendeka akiangalia kitabu cha Mpango wa miaka mitano wa ujenzi wa Majengo ya Mahakama baada ya kukabidhiwa na Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma.
Jaji
Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Njombe Mhe. Christopher Ole Sendeka wakipata maelezo ya maendeleo ya mradi wa ujenzi wa jengo la Mahakama ya Mwanzo Makete Jaji Mkuu alipoenda kukagua akiwa katika ziara yake wilayani Makete.
Jengo la Mahakama ya Mwanzo Makete likiwa katika hatua za ukamilishwaji wake.
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (wa pili kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Njombe. Katikati ni Mkuu
wa Mkoa Mhe. Chistopher Ole Sendeka na wa kwanza kushoto ni Jaji Mfawidhi wa Mhakama Kuu ya Tanzania kanda ya Iringa Mhe. Kente.
Jaji
Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akiwa
katika picha ya pamoja na watumishi wa Mahakama ya wilaya ya Makete.
Watumishi wa Mahakama ya wilaya ya Makete wakimsikiliza Jaji Mkuu akizungumza nao.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni