Jumanne, 27 Agosti 2019

WANANCHI WAPATIWA ELIMU JUU YA MAHAKAMA INAYOTEMBEA


Na Aziza Muhali, SJMC

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu-Dar es Salaam imetoa elimu juu ya Mahakama Inayotembea kwa wananchi ili waweze kuifahamau na kupata huduma zinazotolewa na Mahakama hiyo.

Akizungumza na wananchi waliofika katika Mahakama hiyo kupata huduma mbalimbali  mapema Agosti 27, 2019, Mfawidhi huyo ambaye pia ni Naibu Msajili wa Mahakama aliwataka wananchi kufikisha ujumbe wa Mahakama Inayotembea 'mobile court', kwa wananchi wengine ili waweze kufahamu jinsi Mahakama hiyo inavyofanya kazi. 

“Mahakama hii ni Mahakama inayotembea na iliyokamilika inayowafikia wananchi katika makazi yao lengo likiwa ni kuboresha na kusogeza huduma za Mahakama karibu na wananchi, “alisema Mhe.Mhina.

Aliongeza kuwa maeneo yatakayohudumiwa na mahakama hiyo ni wakazi wa Bunju A ambapo Mahakama hiyo itatoa huduma katika viwanja vya Ofisi ya Serikali za Mitaa, Kibamba, Viwanja vya Ofisi ya Wilaya ya Kinondoni, Chanika, pembeni ya Kituo kipya cha Polisi Chanika, Buza, eneo la kituo cha Mabasi Buza.

Kwa upande wake Karani Mkuu Kitengo cha Jinai, Immaculate  Konala ambaye pia ni Msaidizi Mkuu wa Kumbukumbu kutoka Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, amewataka wananchi hao kuepuka kupewa huduma na watu wasiojulikana kisheria ,bali wawatumie watumishi wa Mahakama ambao huvaa vitambulisho vya kazi.

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Mhe. Kelvin Mhina akitoa elimu juu ya Mahakama Inayotembea kwa wananchi waliofika Mahakamani hapo kupatiwa huduma mbalimbali.
Baadhi ya wananchi waliofika kupatiwa huduma za kimahakama katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakisikiliza maelezo juu ya utendaji kazi wa Mahakama  Inayotembea. 

                                                           (Picha na Aziza Muhali)



Hakuna maoni:

Chapisha Maoni