Ijumaa, 30 Agosti 2019

MAHAKAMA KUTUNZA KUMBUKUMBU ZA KESI KIELEKITRONIKI


Lydia Churi- Mahakama-Iringa
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amesema wakati umefika wa Mahakama kuanza kutunza kumbukumbu za mashauri kwa njia ya kielekitroniki ili kuepuka kupotea kwa kumbukumbu muhimu.

Akihitimisha ziara yake ya kikazi katika mikoa ya Njombe na Iringa leo, Jaji Mkuu amesema Mahakama itakapoanza kutunza kumbukumbu za mashauri kielekitroniki itasaidia kupunguza tatizo la kupotea kwa kumbukumbu na rekodi mbalimbali za mashauri zitakuwa katika hali nzuri.

Alisema vitabu vinavyotunza kumbukumbu za mashauri kuanzia Mahakama za ngazi za chini mpaka Mahakama ya Rufani kurasa zake huwa zimefifia na hazisomeki vizuri kutokana na kutolewa nakala (photocopy) mara nyingi na wakati mwingine kurasa nyingine hupotea.

“Kurasa zilizotolewa photocopy mara nyingi hufikia kiwango cha kutosomeka kabisa hivyo kuna haja ya kuanza kutunza kumbukumbu hizi kwa njia ya kielekitroniki ili kurasa hizo zisomeke kwa ufasaha zaidi”, alisema Jaji Mkuu.

Hali ya Usikilizwaji wa Mashauri kanda ya Iringa

Jaji Mkuu amesema ameridhishwa na kasi ya usikilizaji wa mashauri kwenye  kanda hiyo hasa katika Mahakama za mikoa na amewataka Mahakimu kuendeleza kasi hiyo ili watimize vigezo vya idadi ya mashauri vilivyowekwa. Mahakama iliweka kigezo kuwa kila Hakimu amalize mashauri 250 kwa mwaka.  

Aidha, Mahakama Kuu kanda ya Iringa hadi kufikia Disemba 2018 ilibakiwa na mashauri 2063. Kuanzia Januari hadi Julai 2019 ilisajili mashauri 4566 na kufanikiwa kumaliza mashauri 4530 sawa na asilimia 68.3 ya mashauri yote. Hadi Julai, 2019 yamebaki mashauri 1834 sawa na asilimia 31.7.

Kuhusu kuboresha uandishi wa hukumu zinazotolewa, Jaji Mkuu amesema upo mpango wa mafunzo ya uandishi wa hukumu na lugha utakaotekelezwa ili kuwezesha hukumu zinazotolewa kuwa zinazoeleweka, fupi na zenye lugha fasaha.

Ushirikiano kati ya Mahakama na Mihimili mingine 

Akizungumzia ushirikiano na mihimili ya Serikali na Bunge, Jaji Mkuu amesema mihimili yote ni watumishi wa wananchi hivyo inapaswa kushirikiana bila kuathiri uhuru wao.

Alitoa wito kwa Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na Taasisi ya kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kuchambua malalamiko wanayopokea ili kujua yale yanayotokana na wananchi kutoelewa taratibu. Amezitaka taasisi hizo kuwa na rejista na Mahakama kuwa na utaratibu wa kuyachukua malalamiko hayo na kuyafanyia kazi ikiwa ni pamoja na kuwaelimisha wananchi. 

Mafanikio ya ziara

Kuhusu ziara yake, Jaji Mkuu amesema ameridhishwa na kazi iliyofanyika hasa katika maeneo ya kasi ya usikilizwaji wa mashauri, uelimishaji na utoaji wa elimu kwa wananchi, upunguzaji wa msongamano wa mahabusu magereza na maendeleo mazuri ya miradi ya ujenzi wa majengo ya Mahakama.

Jaji Mkuu amemaliza ziara ya siku tano katika mikoa ya Iringa na Njombe iliyokuwa na lengo la kubainisha kwa wadau changamoto zilizoibuliwa wakati wa kikao cha Mahakama ya Rufani, kukagua shughuli za mahakama, kukaagua miradi ya ujenzi wa majengo ya mahakama, kuhimiza uzingatiaji wa maadili na kuhimiza ushirikiano baina ya Mahakama na wadau.  

 Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akimkabidhi Mkuu wa Wilaya ya Mufindi Mhe. January William kitabu cha Mpango wa miaka mitano wa ujenzi wa majengo ya Mahakama ya Tanzania wakati alipomtembelea Mkuu huyo wa Wilaya leo akiwa katika ziara ya kikazi katika mkoa wa Iringa.





 Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akizungumza na watumishi wa Mahakama ya wilaya ya Mufindi (hawapo pichani) alipotembelea Mahakama hiyo leo. Kushoto ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Iringa Mhe. Panterine Kente na kulia ni Mkurugenzi wa Ukaguzi wa huduma za Kimahakama Mhe. Happiness Ndesamburo.
 
 Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (mbele katikati) akiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa Mahakama ya wilaya ya Mufindi mara baada ya kuzungumza nao.
 Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (wa pili kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Mufindi alipomtembelea Mkuu wa wilaya hiyo Bwn. January William  (wa pili kulia) ofisini kwake.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni