Lydia
Churi-Mahakama Iringa
Mahakimu wametakiwa
kusimamia uendeshaji wa mashauri na kuzuia maahirisho ya mara kwa mara ya kesi
bila ya sababu za msingi kwa lengo la kuhakikisha kesi zinamalizika kwa wakati
Mahakamani.
Jaji Mkuu wa Tanzania
Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amesema hayo wakati wa kikao cha majumuisho mara
baada ya kumaliza ziara ya kikazi ya siku tano katika mikoa ya Iringa na Njombe
aliyoifanya kwa lengo la kukagua shughuli za Mahakama pamoja na kubainisha kwa
wadau changamoto zilizoibuliwa wakati wa kikao cha Mahakama ya Rufani
kilichomalizika leo mjini Iringa.
Jaji Mkuu amewata Mahakimu
kutokubali kuahirisha mashauri kwa muda mrefu kwa ajili ya kuandaa maamuzi
madogo yanayotokana na pingamizi ambazo nyingi hutumiwa vibaya kwa lengo la
kuchelewesha mashauri.
“Maafisa wote wa Mahakama
ni jukumu lenu pia kuzipa nguvu za kimahakama vifungu vya sheria zinazolinda
haki ya Mwananchi aliye mahabusu kwa kuhakikisha hakuna mwananchi atashikiliwa bila
kufikishwa mahakamani ndani ya siku zilizowekwa na sheria”, alisema.
Alitoa rai kwa Mahakimu
kutokuwa wepesi kukubali hoja za waendesha mashitaka za kusema kuwa upelelezi
bado unaendelea bila ya kufafanua ni kitu gani katika upelelezi bado
kinatafutwa na ni kwa muda gani.
“Ni umakini wa Mahakama
ndiyo utahakikisha kuwa shughuli za upelelezi haziwanyimi wananchi haki yao ya
kikatiba ya kutochelewesha haki yao ya kusikilizwa kesi dhidi yao bila sababu
za kimsingi,” alisisitiza Jaji Mkuu.
Akizungumzia dhamana,
Jaji Mkuu amesema ni wajibu wa Mahakama kutoa dhamana kwa makosa yenye dhamana
kwa kuwa Mahakama ni msimamizi wa haki ya kila mtu kuwa huru na kuishi kama mtu
huru.
Alivitaja vigezo vya
kutumiwa katika kutoa dhamana kuwa ni pamoja na vitambulisho vya Taifa, na
vitambulisho vinavyokubalika. Aliongeza kuwa Mahakama pia ziwaruhusu washtakiwa
kujidhamini wenyewe pale Hakimu anapojiridhisha na utambulisho wao kuwa
watahudhuria mahakamani.
“Mashauri ambayo
washtakiwa wamekosa dhamana yasikilizwe mfululizo, kwa yale makosa yasiyo na
dhamana na yako ndani ya mamlaka ya Mahakama, matumizi ya sheria yatumike ili
kuyaondosha”, alisema.
Katika kupunguza
msongamano magerezani, Jaji Mkuu amesema Maafisa wa Mahakama hawana budi kutumia
adhabu mbadala kwa makosa madogo madogo kwa kuzingatia sheria zilizopo.
Jaji
Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis akimsikiliza Mkuu wa wilaya ya Mufindi Bwn. Jamhury William akimuelezea jambo wakati alipokwenda kukagua kiwanja itakapojengwa Mahakama ya Mwanzo mjini Mafinga.
Watumishi wa Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Iringa wakimsikiliza Jaji
Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis akizungumza nao. Wa kwanza kushoto ni Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Iringa Mhe. Agatha Chugulu.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni