Na
Mary Gwera, Mahakama
Tanzania imetajwa kuwa
nchi ya kwanza Barani Afrika kuanzisha huduma ya Mahakama inayotembea ‘Mobile Court’
lengo likiwa ni kusogeza huduma za Mahakama karibu zaidi na wananchi.
Mtaalam Mwelekezi
kutoka Benki ya Dunia, Bw. Waleed Malik alibainisha hayo Septemba 02, 2019 katika
Kituo cha Mafunzo na Habari kilichopo eneo la Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu-Dar
es Salaam wakati akitoa Mada katika Mafunzo kwa vitendo kwa baadhi ya Watumishi
wa Mahakama wa jijini Dar es Salaam wanaohudumu katika Mahakama hiyo.
“Kwa kuwa Tanzania ni
nchi ya kwanza katika Bara la Afrika kuanzisha huduma hii ni vyema mkatoa
huduma bora zenye viwango ili nchi nyingine zivutiwe na kuja kujifunza kutoka
kwenu,” alieleza Bw. Malik.
Aidha; Mwezeshaji huyo wa
Mafunzo hayo kutoka Benki ya Dunia, aliwasisitiza Watumishi hao kufanya kazi
kwa ushirikiano ‘team work’ kwa kuwa ndio nguzo kuu ya mafanikio.
“Nawaomba kufanya kazi
kwa pamoja ili kuleta matokeo chanya ya huduma hii,” alisema Bw. Malik.
Aidha; Mtaalam huyo pia
alisisitiza juu ya utoaji elimu kwa umma kuhusu Mahakama hiyo ili jamii iwe na
uelewa wa jinsi inavyofanya kazi na huduma inazotoa.
Akifungua rasmi Mafunzo
hayo, naye Msajili Mkuu, Mahakama ya Tanzania, Mhe. Katarina Revocati amewaasa
Watumishi wanaofanya kazi katika Mahakama hiyo kutojihusisha na vitendo vya
rushwa pindi wanapotekeleza majukumu yao.
“Mahakama imewaamini ninyi, na mpo katika historia
ya kuwa sehemu ya Watumishi wa kwanza kutoa huduma katika aina hii ya Mahakama,
hivyo ni rai yangu kwenu kutojihusisha na vitendo hivyo kwakuwa vitaidhoofisha Mahakama
kwa ujumla,” alisisitiza Mhe. Revocati.
Mbali na vitendo vya
rushwa, Mhe. Msajili Mkuu vilevile alisisitiza juu ya kutoa huduma nzuri kwa
wateja ‘customer care’ ili lengo kuu linalokusudiwa na Mahakama ya Tanzania la
utoaji huduma bora kwa wananchi liweze kufikiwa.
Jumla ya Washiriki 50
ambao ni Mahakimu, Dereva, Washauri wa Mahakama, Makarani wa Mahakama, Maafisa
Utumishi na Utawala, Maafisa Habari, Makatibu Muhtasi pamoja na baadhi ya
Wajumbe wa Menejimenti ya Mahakama ya Tanzania wameshiriki katika mafunzo kwa
vitendo kuhusiana na utoaji huduma ya Mahakama inayotembea ikiwa ni kuwawezesha
kutoa huduma kwa ufanisi zaidi.
Kwa sasa Mahakama zinazotembea zipo mbili na zinatoa huduma katika mikoa miwili ya Dar es Salaam na Mwanza, hata hivyo; Mahakama ya Tanzania ina mpango wa kutanua wigo wa utoaji huduma hii kwa kuanzisha vituo vingine katika mikoa iliyosalia kwa awamu tofauti kulingana na upatikanaji wa fedha.
Kwa sasa Mahakama zinazotembea zipo mbili na zinatoa huduma katika mikoa miwili ya Dar es Salaam na Mwanza, hata hivyo; Mahakama ya Tanzania ina mpango wa kutanua wigo wa utoaji huduma hii kwa kuanzisha vituo vingine katika mikoa iliyosalia kwa awamu tofauti kulingana na upatikanaji wa fedha.
Baadhi ya nchi nyingine
zinazotoa huduma ya Mahakama inayotembea ni pamoja na Guatemala, Brazil na
Pakistan.
Mtaalam kutoka
Benki ya Dunia ambaye pia alikuwa Mwezeshaji wa Mafunzo kwa vitendo juu ya ufanyaji kazi katika Mahakama inayotembea 'mobile court' , Bw. Waleed Malik (wa kwanza kulia) akitoa maelezo kwa sehemu ya Wajumbe wa Menejimenti ya Mahakama ya Tanzania. (Wa pili kulia) ni
Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe Katarina Revocati, (wa kwanza
kushoto) ni Naibu Msajili Mwandamizi, Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Messeka Chaba, (wa pili kushoto) ni Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Bw. Leonard Magacha, (wa tatu
kushoto) ni Naibu Msajili Mfawidhi, Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Joachim Tiganga, (wa nne
kushoto) ni Mkurugenzi wa Usimamizi wa Mashauri, Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Nkya na (wa tano kushoto) ni Katibu wa Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Upendo Ngitiri.
Mkurugenzi wa Teknolojia
ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), Bw. Kalege Enock (aliyenyoosha kidole)
akiwaonyesha baadhi ya viongozi wa Mahakama ya Tanzania na watumishi wanaofanya
kazi katika Mahakama inayotembea moja ya vifaa kilichopo ndani ya gari la
Mahakama hiyo, wakati wa mafunzo kwa vitendo yaliyofanyika leo katika Kituo cha
Mafunzo na Habari kilichopo katika Mahakama Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es
Salaam.
Meza kuu katika picha ya pamoja
na baadhi ya watumishi wa Mahakama ya Tanzania wanaofanya kazi katika Mahakama
Inayotembea-Kinondoni.
(Picha na Magreth Kinabo, Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni