Na
Lydia Churi- Mahakama Njombe
Jaji Mkuu wa Tanzania
Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma ameagiza kuanzishwa kwa utaratibu wa kusajili
makubaliano ya ukoo ili kupunguza migogoro inayoweza kutokea katika mashauri ya
Mirathi.
Akizungumzia dhana ya
usuluhishi wa migogoro, Jaji Mkuu alisema kuwa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania inahimiza migogoro kutatuliwa nje ya Mahakama hivyo ameshauri mashauri
ya Mirathi nchini yapatiwe suluhu nje ya Mahakama.
Akizungumza wakati wa
ziara yake ya kikazi mkoni Njombe, Mhe. Prof. Juma alisema kuwepo kwa utaratibu
wa kusajili makubaliano ya ukoo kutasaidia kumaliza migogoro ya mirathi ambayo
imekuwa ikichukua muda mrefu Mahakamani wakati wasimamizi wa mirathi wakiendelea
kufaidika na mali za marehemu.
Alisema utaratibu
mwingine ulioanzishwa na Mahakama jijini Dar es salaam ni ule wa kufanya malipo
ya mirathi kupitia benki na hivyo ameshauri mahakama nyingine kuiga utaratibu
huo.
“Ni vizuri malipo hayo
yakapitia benki na si kugawana ofisini kwa hakimu kwani siku zote hicho huwa ni
chanzo cha migogoro” alisema Jaji Mkuu.
Alisema changamoto hii
pamoja na nyingine zinazoikabili Mahakama ya Tanzania wameziona kwenye vikao
vya Mahakama ya Rufani vinavyoendelea katika Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya
Iringa.
Alisema mikoa ya Njombe
na Iringa ina jumla ya mashauri ya mirathi 577 yaliyodumu Mahakamani kwa zaidi
ya miaka miwili tangu kusajiliwa ambapo kati ya hayo, mashauri 183 ni ya mkoa
wa Njombe na mashauri 394 ni ya mkoa wa Iringa.
“Mashauri ya mirathi
kukaa Mahakamani kwa kipindi cha zaidi ya miaka miwili ni muda mrefu sana kwa
kuwa ukizungumzia mirathi maana yake ni mali inayoshikiliwa hadi mgogoro
utakapoisha”, alifafanua.
Jaji Mkuu anaendelea na
ziara ya kikazi katika mkoa wa Iringa baada ya kukamilisha ziara katika mkoa wa
Njombe ambapo alitembelea mahakama zilizopo katika wilaya za Makete, Ludewa na
Njombe mjini.
Jaji Mkuu wa Tanzania
Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akisikiliza hoja za Watumishi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoa wa Njombe (hawapo pichani) alipofika kukagua shughuli za Mahakama akiwa kwenye ziara ya kikazi katika mikoa ya Njombe na Iringa. Kushoto ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Iringa Mhe. Panteine Kente na kulia ni Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Huduma za Kimahakama wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Happiness Ndesamburo.
Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Huduma za Kimahakama wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Happiness Ndesamburo akifafanua jambo kwa Watumishi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe walipokuwa wakizungumza na Jaji Mkuu.
Watumishi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe walipokuwa wakizungumza na Jaji Mkuu.
Afisa Utumishi wa Mahakama ya Tanzania Bibi. Rose Tengu akitoa ufafanuzi juu ya masuala mbalimbali yanayohusu Utumishi kwa Watumishi wa Mahakama ya
Hakimu Mkazi Njombe walipokuwa wakizungumza na Jaji Mkuu.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni