Na
Lydia Churi- Mahakama-Njombe
Jaji Mkuu wa Tanzania
Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma ameiomba Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa-Takukuru
kuyafanyia uchunguzi wa kina malalamiko ya rushwa wanayopokea kutoka kwa wananchi.
Akizungumza na Kamati ya
Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Ludewa alipomtembelea Mkuu wa Wilaya hiyo, Bwn. Andrea
Tsere ofisini kwake, Jaji Mkuu ameiomba Takukuru kuyafanyia uchunguzi malalamiko hayo
ili kubaini kama yanatokana na wananchi
kutofahamu taratibu za Mahakama au ni tuhuma kweli za rushwa.
“Takukuru tunawashukuru
kwa kuwa mmetupa ramani ya maeneo yenye viashiria vya rushwa lakini sasa
tunawaomba muende hatua ya pili ya kuyachunguza malalamiko yanayoletwa kwenu
ili kujua kama yanatokana na wananchi kutokujua taratibu au ni malalamiko ya
kweli”, alisema Jaji Mkuu.
Alisema hatua ya Takukuru
kuyachunguza malalamiko hayo itairahisishia Mahakama ya Tanzania kufahamu idadi
ya wananchi wasiofahamu taratibu za Mahakama pamoja na kujua kiwango halisi cha
vitendo vya rushwa ndani ya Mahakama.
Akizungumzia changamoto
za utoaji haki nchini, Jaji Mkuu alisema Mihimili yote mitatu ya dola haina
budi kushirikiana kwa karibu kwa kuwa wote wana lengo moja la kumhudumia
mwananchi. Aliongeza kuwa huduma za mahakama zinatakiwa kusogezwa karibu zaidi
na wananchi kwa ushirikiano wa mihimili yote.
Alisema changamoto katika
kusogeza huduma za mahakama karibu zaidi na wananchi bado ni kubwa na hasa kufikisha
haki katika ngazi za chini zikiwemo Mahakama za Mwanzo na za wilaya.
Kwa mujibu wa Jaji Mkuu, Mahakama
ya Tanzania imeandaa Mpango wa miaka mitano unaotoa picha ya maeneo
yanayohitaji huduma za Mahakama. Alisema, Mpango huo utaisaidia Mahakama kujipima
katika kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi.
“Kuanzia sasa mpaka
ifikapo mwaka 2020 tunataka kila mkoa uwe na Mahakama Kuu pamoja na Mahakama za
Mwanzo katika kila tarafa nchini”, alisema.
Aliongeza kuwa Mahakama
imeshaandaa michoro kwa ajili ya ujenzi wa majengo yake na endapo kutakuwa na
wilaya yenye fedha za ujenzi, Mahakama itashirikiana nayo kujenga.
Akizungumzia utovu wa maadili,
Jaji Mkuu alisema Mahakama haifichi changamoto hiyo na katika kupambana nayo, tayari
imesambaza mabango ya kupambana rushwa nchi nzima ili kuimarisha Imani ya
wananchi kwa mhimili huo. “Bila kuwa na Imani ya wananchi Mahakama hazitakuwa
na maana”, alisema.
Kuhusu uchumi wa viwanda
na kufikia uchumi wa kati, Jaji Mkuu alisema taratibu za Mahakama hazina budi
kuangaliwa upya kwa kuwa baadhi ni ndefu na haziendani na kasi ya ukuaji wa uchumi
huku akitolea mfano wa mashauri ya ardhi na yale ya Mirathi kuwa huchukua muda
mrefu na mwisho wake thamani ya mali husika hupotea.
Aliwataka Majaji na Mahakimu
kuifahamu jamii inayowazunguka na kuhakikisha wanamaliza mashauri mapema ili
kuendana na kasi ya ukuaji wa uchumi.
Jaji Mkuu wa Tanzania
Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akizungumza na watumishi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Njombe alipofika kukagua shughulii za Mahakama akiwa katika ziara yake kwenye mikoa ya Njombe na Iringa.
Watumishi wa Mahakama ya
Hakimu Mkazi Njombe wakimsikiliza Jaji Mkuu alipozungumza nao leo.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni