Na Magreth Kinabo-
Mahakama
Jaji Kiongozi wa
Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi amewashauri viongozi na wanachama wa Chama cha Ushirika
cha Akiba na Mikopo cha Mahakama ya
Tanzania (MAHAKAMA SACCOS) kukinadi chama hicho, ili kiweze kuwa na idadi kubwa
ya wanachama na kuiwezesha Mahakama kuwa Taasisi bora inayoongoza kwa utoaji
wa mikopo kwa riba nafuu kitaifa na kimataifa.
Akizungumza leo
Oktoba 26, mwaka huu wakati akiwa mgeni
rasmi wa kufungua Mkutano Mkuu wa Mwaka wa chama hicho, uliofanyika katika ukumbi namba
moja uliopo Mahakama Kuu ya Tanzania, jijini Dar es Salaam, Jaji Kiongozi alisema ni vema viongozi hao na wanachama kuweka mikakati ya kuweza kuongeza idadi ya
wanachama ili kufikia azima hiyo.
Alisema idadi ya
majaji saba waliojiunga na chama hicho, bado ni ndogo, wakiwemo baadhi ya mahakimu na
wasajili.
“Mnapaswa kuweka
mikakati ya kukinadi chama hiki ili kuweza kuwa na angalau nusu ya idadi ya
watumishi wa Mahakama ya Tanzania, chama hakijafanyiwa uhamasishaji wa kutosha,
hivyo kila mwanachama anao wajibu wa kuhamasisha watu kujiunga,” alisema Jaji
Kiongozi.
Jaji Kiongozi aliongeza
kwamba chama hicho, kinatakiwa kutumia mitandao ya kijamii na tovuti ya
Mahakama ili kiweze kufahamika na kutangaza shughuli za kupitia mitandao hiyo,
ikiwemo kuwa na vijarida na vipeperushi vya chama, kwa kuwa ni nyezo za
kukifanya kiweze kufahamika.
Aidha Jaji
Kiongozi alikishauri chama hicho, kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA)
katika shughuli zake, ikiwa ni hatua ya kuweza kuwafikia watumishi wengi na kupunguza
gharama za uendeshaji.
Dkt. Feleshi alisema
pia chama hicho, kitumike kama sehemu ya kudumisha, amani, upendo, ushirikiano
na mshikamano miongoni kwa watumishi hao ili kiweze kusaidia changamoto za
kiuchumi na kijamii hali itakayosaidia wanachama kuweza kufanya kazi za utoaji
haki kwa hisia.
Awali akizungumza
kabla ya kumkaribisha Jaji Kiongozi, Mwenyekiti wa chama hicho, Bw. Edwin Protas alisema kilianzishwa mwaka 1970 kikiwa na
wanachama 84 na hivi sasa kina wanachama 372, kati ya watumishi zaidi ya 5000 wa
Mahakama.
Protas alisema
kwamba baadhi wanachama wake, ambao si maafisa wanakabiliwa na changamoto ya
kuwa na mishahara midogo, hivyo aliiomba Tume ya Utumishi ya Mahakama ya
Tanzania kuweza kuliangalia suala hilo, ili chama kisiweze kuzorota.
Kwa upande wake,
Afisa Ushirika kutoka Manispaa ya Ilala,Bi. Herodia Kambanga alikitaka chama
hicho kuwa ushirikiano na vyama vingine ili kuweza kubadilishana uzoefu na
kutatua changamoto mbalimbali.
Afisa Ushirika kutoka Manispaa ya Ilala, Bi. Herodia Kambanga
akisisitiza jambo kwa wanachama wa chama hicho.
|
Baadhi ya wanachama wa chama hicho, wakipitia taarifa mbalimbali za
chama.
|
Mwanachama wa MAHAKAMA SACCOS, Bw. William Yohana akichangia jambo
katika mkutano huo.
(Picha na Magreth Kinabo - Mahakama)
|
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni