Jumatano, 30 Oktoba 2019

KATTANGA AHIMIZA UMOJA NA UPENDO KWA WATUMISHI WA MAHAKAMA


 Na Lydia Churi-Mahakama

Aliyekuwa Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Balozi Mteule, Hussein Kattanga amewataka watumishi wa Mahakama kuwa na umoja wanapotekeleza majukumu yao na kumpa ushirikiano Mtendaji Mkuu mpya wa Mahakama. 

Akiagana na wajumbe wa Menejimenti ya Mahakama ya Tanzania na kumtambulisha kwa wajumbe hao Mtendaji Mkuu Mpya wa Mahakama, Mhe. Kattanga amesema kuwepo na umoja kati ya Watumishi wa Mahakama kutarahisisha utekelezaji wa majukumu mbalimbali ndani ya Mhimili huo.

Aidha, amewataka wajumbe hao wa Menejimenti ya Mahakama kuwa na upendo siku zote na kujiepusha na chuki kwani chuki ni kitu kinachoondoa umoja. “Jiepusheni na chuki, ukimchukia mtu unajitesa mwenyewe”, alisisitiza.

Kattanga pia amewataka wajumbe hao wa Menejimenti kutoa ushirikiano wa dhati kwa Mtendaji Mkuu mpya na kuwa na ari ya kufanya kazi ili waweze kufanikiwa zaidi. Aliwaasa wajumbe hao kutokukasirika pindi wanapohimizwa kutekeleza majukumu yao. 

Naye Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Bwn. Mathias Kabunduguru amesema atazifanyia kazi changamoto mbalimbali zinazoikabili Mahakama ya Tanzania ikiwemo upungufu wa Mahakimu pamoja na watumishi wengine.

Alisema Mahakama ya Tanzania ni chombo cha kutoa haki na inayo dhamana kubwa katika jamii hivyo muonekano wake unapaswa kuwa mzuri wakati wote.
Aidha, alimpongeza Mhe. Kattanga kwa kuteuliwa kuwa Balozi na kuondoka salama Mahakama ya Tanzania.

Wakati huo huo, Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Katarina Revocati amempongeza Mhe. Kattanga kwa mabadiliko aliyoyafanya ndani ya Mahakama katika kipindi chote alichokuwa Mtendaji Mkuu.

“Tulifanya kazi na wewe vizuri sana, tunashukuru ulivyokuwa chachu ya mabadiliko ndani ya Mahakama na tumejifunza mengi kutoka kwako”, alisema Msajili Mkuu.

Akimkaribisha Mtendaji Mkuu mpya wa Mahakama, Mhe. Revocati aliahidi kutoa ushirikiano kwa kiongozi huyo mpya. “Tunakukaribisha na tutashirikiana na wewe ipasavyo. Una timu ya watu watiifu katika kazi”, alisema.

Hivi karibuni, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli alifanya mabadiliko ndani ya Mahakama kwa kumteua Bwn. Mathias Kabunduguru kuwa Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania kuchukua nafasi ya Bwn. Hussein Kattanga ambaye ameteuliwa kuwa Balozi. 

Aliyekuwa Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Balozi Mteule Hussein Kattanga akipokea zawadi ya maua kama ishara ya kuagana na Menejimenti ya Mahakama ya Tanzania. Anayempa maua ni Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Katarina Revocati.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Bwn. Mathias Kabundunguru  akipokea zawadi ya maua kama ishara ya kukaribishwa na Menejimenti ya Mahakama ya Tanzania. Anayempa maua ni Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Katarina Revocati. 
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Bwn. Mathias Kabundunguru  akimpongeza aliyekuwa Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Balozi Mteule Hussein Kattanga.  
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Bwn. Mathias Kabundunguru akizungumza na wajumbe wa Menejimenti ya Mahakama ya Tanzania.
 
Baadhi ya Wajumbe wa Menejimenti ya Mahakama ya Tanzania wakisikiliza.
Aliyekuwa Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Balozi Mteule Hussein Kattanga akizungumza na wajumbe wa Menejimenti ya Mahakama ya Tanzania.

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Bwn. Mathias Kabundunguru na
aliyekuwa Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Balozi Mteule Hussein Kattanga wakiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa Menejimenti ya Mahakama ya Tanzania. Kushoto ni Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Katarina Revocati.   
Aliyekuwa Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Balozi Mteule Hussein Kattanga akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Madereva wa Mahakama ya Tanzania.

Aliyekuwa Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Balozi Mteule Hussein Kattanga akiwa katika picha ya pamoja na Watendaji wa Divisheni za Mahakama Kuu ya Tanzania pamoja na Kanda ya Dar es salaam.

Aliyekuwa Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Balozi Mteule Hussein Kattanga akiwa katika picha ya pamoja na Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali watu Bwn. Edward Nkembo ( Wa pili kushoto) pamoja na wakurugenzi wasaidizi wa Idara hiyo.




Hakuna maoni:

Chapisha Maoni