Jumanne, 8 Oktoba 2019

JAJI MKUU: UTOAJI HABARI NI WAJIBU SI FADHILA


Na Mary Gwera, Mahakama

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof.  Ibrahim Hamis Juma ameishauri Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika (MISATAN) pamoja na vyombo vya habari nchini kuitekeleza ipasavyo Sheria  namba 6 ya Upatikanaji wa Habari ya mwaka 2016.

Akizungumza na Mwenyekiti wa MISATAN Tawi la Tanzania, Bi. Salome Kitomari, mapema Oktoba 08, 2019 ofisini kwake jijini Dar es Salaam, Mhe. Jaji Mkuu alisema Sheria hii itumike ipasavyo kudai taarifa.

“Tumieni sheria hii kudai taarifa, sheria inatoa shurti ya kutoa taarifa zinazotakiwa na umma, hivyo suala la kutoa taarifa sio fadhila ni amri kwa hivyo ni vyema kuangalia ni kwa namna gani tunatumia Sheria hii kushurutisha utoaji wa taarifa,” alibainisha Mhe. Jaji Prof. Juma.

Mhe. Jaji Mkuu aliongeza kuwa ili kutekeleza sheria hii ipasavyo ni wajibu wa kila mmoja kutimiza wajibu wake, kwa kufanya hivyo tutakuwa tumetekeleza takwa la kikatiba na kisheria.

Kwa upande mwingine, Mhe. Jaji Mkuu alizungumzia pia suala la Vyombo vya habari nchini kuandika Habari za uchunguzi ‘Investigative Journalism’badala ya kutegemea habari zitokanazo matukio mbalimbali.

“Ni muhimu pia kufanya habari za uchunguzi kwa kuchagua mada maalum ‘agenda setting’ itakayokuongoza kufanya utafiti, kwa kufanya hivi itasaidia kupunguza malalamiko na vilevile itasaidia kuwa na habari zenye usahihi zaidi ‘accurate’, alieleza Mhe. Jaji Mkuu.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa MISATAN-Tanzania, Bi. Salome Kitomari alimueleza Mhe. Jaji Mkuu kuwa Taasisi yake imekuwa na uhusiano mzuri na Mahakama katika maeneo mbalimbali.

“MISATAN kwa kushirikiana na Mahakama tumefanikiwa kutoa mafunzo ya Huduma kwa Mteja ‘Customer Care’ kwa zaidi ya Watumishi 350 wa Mahakama,” alieleza Bi. Kitomari.

Hata hivyo; Mwenyekiti huyo alishauri mafunzo haya ni vizuri kutolewa pia kwa Watumishi wa Mahakama wa ngazi za juu wakiwemo Majaji na Mahakimu.

Aidha; Bi. Salome aliongeza kwa kupendekeza kufanyika kwa Mkutano kati ya Mahakama, MISATAN na Taasisi nyingine za Habari lengo likiwa ni kujenga imani na uwajibikaji kwa taasisi zote.

Ujumbe huo wa MISATAN umemtembelea Mhe. Jaji Mkuu kwa lengo la kuitambulisha rasmi Taasisi hiyo, kuishukuru Mahakama kwa kufanya kazi kwa karibu na MISA Tanzania ikiwa ni pamoja na kujadili maeneo ya uhusiano baina ya Taasisi hizi kwa miaka ijayo.
 Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akizungumza na Mwenyekiti wa MISATAN Tanzania, Bi. Salome Kitomari (hayupo pichani) pindi ujumbe kutoka Taasisi hiyo ulipomtembelea Ofisini kwake, Mahakama ya Rufani jijini Dar es Salaam.
 Mwenyekiti wa MISATAN-Tanzania, Bi. Salome Kitomari akizungumza jambo na Mhe. Jaji Mkuu (hayupo pichani).

Mhe. Jaji Mkuu akisisitiza jambo wakati wa mazungumzo hayo. Wa pili kushoto ni Mkuu wa Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano, Mahakama ya Tanzania, Bw. Nurdin Ndimbe, wa kwanza kushoto ni Katibu wa Mhe. Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Adrian Kilimi, kulia ni Maafisa kutoka MISATAN na Mahakama.

Maafisa kutoka MISATAN-Tanzania, (kushoto), Mwenyekiti, Bi. Salome Kitomari na Afisa Habari na Utafiti kutoka Taasisi hiyo, Bi. Neema Kasabuliro kwa pamoja wakinukuu masuala yaliyokuwa yakitolewa na Mhe. Jaji Mkuu.
 Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe kutoka MISATAN-Tanzania na baadhi ya Watumishi wa Mahakama walioshiriki katika mazungumzo hayo, wa pili kushoto ni Mwenyekiti wa MISATAN Tanzania, Bi. Salome Kitomari, wa pili kulia ni Mkuu wa Kitengo cha Habari, Elimu na Mawasiliano, Mahakama ya Tanzania, Bw. Nurdin Ndimbe, wa kwanza kushoto ni Afisa Habari na Utafiti kutoka Taasisi hiyo, Bi. Neema Kasabuliro na wa kwanza kulia ni Salum Tawan, Mkutubi-Mahakama ya Tanzania.
(Picha na Mary Gwera, Mahakama)





Hakuna maoni:

Chapisha Maoni