Na
Festo Sanga, Mahakama ya Hakimu Mkazi, Kigoma
Kamati ya Ulinzi na
Usalama Mkoa wa Kigoma ikiongozwa na
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Brigedia Jenerali Mstaafu Emanuel Maganga
imetembelea Jengo la Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma na Nyumba za Makazi za Majaji
na kupongeza upatikanaji wa huduma ya Mahakama Kuu katika mkoa huo.
Ugeni huo ulitembelea
miradi hiyo ya ujenzi mapema Oktoba 08,
2019 na ulipokelewa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma Mhe. Jaji
Ilvin Mugeta.
Katika ziara hiyo, Brigedia
Jenerali Mstaafu Maganga amepongeza jitihada za Mahakama ya Tanzania katika
kusogeza huduma kwa wananchi wa Mkoa wa Kigoma kwani awali walikuwa wakisafiri umbali wa takribani kilomita 858 (kwenda na kurudi) kufuata huduma
za Mahakama Kuu Mkoani Tabora.
Pia amepongeza utendaji
kazi wa Mkandarasi wa ‘Masasi Construction Co Ltd’ anayejenga jengo
la Mahakama Kuu pamoja na nyumba za Makazi za Majaji.
“Wajumbe wenzangu tuone
uwezekano wa kuwatumia wakandarasi hawa katika miradi ya ujenzi kutokana na
kazi waliyoifanya katika jengo hili,” alisema Mkuu wa Mkoa.
Ziara hiyo ni muendelezo
wa utekelezaji wa Mpango ulioandaliwa na Uongozi wa Mahakama Kuu Kigoma kuhakikisha
wadau wa Mahakama Mkoa wa Kigoma wanapata fursa ya kutembelea jengo hilo jipya
na kujionea miundo mbinu iliyopo ikiwa ni pamoja na kupata elimu.
Baadhi ya wadau wakiwemo
wajumbe wa Haki Jinai Mkoa, wajumbe wa vituo vya msaada wa kisheria( paralegal)
Mkoa wa Kigoma, watumishi wa Mahakama Kanda ya Kigoma, wazabuni mbalimbali
waliweza kutembelea jengo hilo ambalo linatarajiwa kuzinduliwa hivi karibuni.
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma,
Brigedia Jenerali Mstaafu Emmanuel Maganga (katikati) akifafanua jambo wakati
yeye pamoja na Kamati ya Ulinzi na Usalama ilipofanya ziara ya kutembelea
miradi ya ujenzi wa Mahakama Kuu Kigoma na nyumba za makazi ya Wahe. Majaji.
Muonekano wa jengo jipya la Mahakama Kuu, Kanda ya Kigoma.
Jaji Mfawidhi wa
Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma Mhe. Jaji Ilvin Mugeta akiongoza msafara wa
wajumbe wa Kamati ya Ulinzi mara walipofika Katika jengo la Mahakama Kuu
Kigoma. Nyuma ya Mhe. Jaji ni Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Brigedia Jenerali Mstaafu Emmanuel Maganga.
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma
Brigedia Jenerali Mstaafu Emanuel Maganga akiteta jambo na Mhe. Jaji Mfawidhi pamoja na Wakandarasi katika UKumbi wa Wazi
wa Jengo la Mahakama Kuu.
Muonekano wa moja
kati ya nyumba za Wahe. Majaji lililopo
mkabala na jengo la Mkuu wa Mkoa Kigoma likiendelea kujengwa.
Picha ya pamoja ya
Kamati ya Ulinzi na Usalama Mkoa wa Kigoma, Viongozi wa Mahakama na Wakandarasi
wa 'Masasi Construction Ltd.'
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni