Na
Lydia Churi-Mahakama, Bunda
Jaji Kiongozi wa Mahakama
Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi amesema Mahakama inakusudia kupunguza
kuwatumia wazee washauri wa Mahakama katika kuamua mashauri Mahakamani na itabaki
ikiwatumia katika mashauri ambayo yataonekana yana ulazima wa kuwatumia wazee
hao.
Akizungumza wilayani
Bunda ambapo ameanza ziara ya kikazi kukagua shughuli za Mahakama katika Mkoa
wa Mara, Jaji Kiongozi amesema wazee hao watatumiwa na Mahakama kwenye mashauri
ambayo yatakuwa na ulazima wa kuwatumia lakini yale ambayo siyo lazima, wazee
hao wataacha kutumiwa.
Jaji Kiongozi amesema
baadhi ya wazee washauri wa Mahakama hujishirikisha na vitendo vya rushwa na
wakati mwingine huwatisha Mahakimu wanapokuwa wakitekeleza wajibu wao.
Alisema matumizi ya wazee
washauri wa Mahakama wakati mwingine husababisha mashauri kuchelewa kumalizika
kutokana na kuchelewa kwao kufika Mahakamani na kusababisha mashauri
kutokusikilizwa kwa wakati.
Akizungumza kuhusu rushwa,
Mhe. Dkt, Feleshi alisema Mahakama kama Taasisi haijishirikishi na vitendo vya rushwa bali
vitendo hivyo hufanywa na baadhi ya
watumishi wasio waaminifu ndani ya Mahakama.
“Tuachane na maneno
mepesi mepesi kuhusu rushwa kwa kuwa taarifa zipo, pelekeni Takukuru, hakuna
anayemlinda mtu”, alisema Jaji Kiongozi.
Alisema Mahakama
itashirikiana na Serikali katika kupambanana na rushwa na hivvo aliwataka
wananchi wenye taarifa juu ya vitendo hivyo kuwasilisha kwenye Taasisi ya
Kuzuia na Kupambana na Rushwa –Takukuru.
Aidha, Mhe. Dkt. Feleshi
amesema Mahakama na Serikali katika wilaya ya Bunda wanapaswa kushirikiana
katika kutatua changamoto nyingine mbalimbali za wananchi kwa kuwa wote
wanamtumikia mwananchi.
Akizungumza na watumishi
wa Mahakama ya wilaya ya Bunda, Jaji Kiongozi amewataka watumishi hao kufanya
kazi kwa bidii, uadilifu na kubeba matarajio ya Taasisi kwa kutoa huduma bora
kwa wananchi.
Aliwataka Mahakimu kumalizika
mashauri kwa wakati, pamoja na kutoa nakala za hukumu na mienendo ya mashauri ndani
ya muda uliopangwa ambao kwa nakala za hukumu ni siku 21 tangu kumalizika kwa
shauri na mienendo ya shauri hutolewa ndani ya siku 30.
Aidha, aliwataka
watumishi hao kujenga tabia ya kutafuta na kufahamu taarifa mbalimbali za
Mahakama kupitia Tovuti pamoja na Blog ya Mahakama ya Tanzania.
Naye Mkuu wa wilaya ya
Bunda Bibi Lydia Bupilipili amewashauri Watumishi wa Mahakama kujenga mazingira
yatakayowafanya wananchi kuendelea kuiamini Mahakama ya Tanzania kwa kutoa
huduma zilizo bora kwa wananchi.
Alisema Serikali pamoja
na Mahakama wilayani Bunda wanashirikiana katika kutatua baadhi ya changamoto za
Mahakama huku akitoa wito kwa Mahakimu kutumia njia ya usuluhishi katika
kutatua baadhi ya migogoro miongoni mwa wananchi.
Mkuu huyo wa wilaya pia
aliishauri Mahakama ya Tanzania kujikita katika kutoa elimu kwa wananchi hasa
kwenye maeneo yenye changamoto zaidi wakati wa maadhimisho ya wiki ya sheria
ambayo hufanyika kila mwaka nchini.
Alisema wananchi hawana
budi kufahamu taratibu mbalimbali za Mahakma hususan zile za ufunguaji wa
mashauri Mahakamani.
Jaji Kiongozi ameanza
ziara ya kikazi ya siku tano Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Musoma ambapo
atakagua shughuli mbalimbali za Mahakama katika wilaya za Bunda, Serengeti,
Tarime pamoja na Musoma.
Jaji Kiongozi wa Mahakama
Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi (kushoto) akiagana na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Mwanza Mhe. Sam Rumanyika na kupokewa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Musoma Mhe. John Kahyoza (katikati) wakati akiwasili wilayani Bunda kuanza ziara ya kikazi katika mkoa wa Mara.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi (kushoto) akisalimiana na Mkuu wa wilaya ya Bunda Bibi Lydia Bupilipili alipowasili ofisini kwa Mkuu huyo wa wilaya wakati akianza ziara ya kikazi katika mkoa wa Mara.
Jaji
Kiongozi wa Mahakama
Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi akizungumza jambo na Mkuu
wa wilaya ya Bunda Bibi Lydia Bupilipili alipoenda kukagua kiwanja cha ujenzi wa jengo la Mahakama ya wilaya ya Bunda. Katikati ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Musoma
Mhe. John Kahyoza
Watumishi wa Mahakama ya wilaya ya Bunda wakimsikiliza Jaji
Kiongozi wa Mahakama
Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi (hayupo pichani) alipokuwa akizungumza nao.
Jaji
Kiongozi wa Mahakama
Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi akikagua Rejesta za mashauri katika Mahakama ya wilaya ya Bunda.Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi akiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa Mahakama ya wilaya ya Bunda. Kulia ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Musoma Mhe. John Kahyoza na kushoto ni Mkuu wa wilaya ya Bunda Bibi Lydia Bupilipili.
Jaji
Kiongozi wa Mahakama
Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi akiwa katika picha na wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya ya Bunda. Kulia ni Jaji
Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Musoma
Mhe. John Kahyoza na kushoto ni Mkuu wa wilaya ya Bunda Bibi Lydia
Bupilipili.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni