Na
Lydia Churi-Mahakama Rukwa
Benki ya Dunia
imeipongeza Mahakama ya Tanzania kwa kutekeleza vizuri mradi wa maboresho ya
huduma za mahakama kupitia Mpango mkakati wake wa miaka mitano (2015/16-2016/2019).
Jaji Mkuu wa Tanzania
Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma aliwasilisha pongezi hizo kutoka Benki ya Dunia kwa
watumishi wa Mahakama ya wilaya ya Kalambo alipokuwa akizungumza nao akiwa
katika ziara ya kikazi kukagua shughuli za Mahakama mkoani Rukwa.
Alisema taarifa ya
ukaguzi iliyoandaliwa na ujumbe wa Benki ya Dunia uliofika nchini Februari 4
hadi 15, 2019 kufanya ukaguzi imetoa pongezi hizo kufuatia Mahakama kuzipitia
sheria na kanuni zaidi ya 50 na kuzifanyia marekebisho ili kurahisisha utoaji
wa haki nchini.
Jaji Mkuu aliyataja
maeneo mengine yaliyopongezwa na Benki ya Dunia kuwa ni hatua iliyochukuliwa na
Mahakama ya kutunga kanuni mpya zinazoongoza Madalali wa pamoja na zile
zinazoongoza Mawakili.
Kwa mujibu wa Jaji Mkuu,
maeneo mengine ni matumizi sahihi ya mfumo wa taarifa za kusajili mashauri
(JSDS II), kwa kuwa katika mfumo huo hakuna taarifa chafu iliyowahi kuingizwa
na kila shauri linalosajiliwa huingizwa kwenye mfumo siku hiyo hiyo
linaposajiliwa.
Aidha, Benki ya Dunia
imeisifu na kuipongeza Mahakama ya Tanzania kwa kujiwekea malengo na kufanya
kazi inayoonyesha matokeo na kujiwekea viwango au mikakati ya kupunguza
mashauri ya mlundikano. Benki hiyo pia imeipongeza Mahakama kwa aina ya ujenzi
wa majengo ya mahakama kwa kuwa yanazingatia kukua kwa matumizi ya teknolojia
ya kisasa.
Maeneo mengine
yaliyoonyesha mafanikio na kupongezwa na Benki ya Dunia ni kitendo cha Mahakama
kujiwajibisha yenyewe katika utendaji kazi wake hasa kwa kujiwekea mifumo ya
kujiwajibisha na kufanyiwa tathmini ya utendaji wake na Taasisi
inayojishughulisha na masuala ya utafiti ya Repoa.
Kufuatia pongezi hizo,
Jaji Mkuu amewataka watumishi wa Mahakama kuendelea kutambua nafasi pekee ya
Mahakama katika jamii kwa kuwa Mahakama hutoa uamuzi kwa kuzingatia taratibu
ilizojiwekea.
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akiwa katika picha ya pamoja na Watumishi wa Mahakama ya wilaya ya Kalambo mara baada ya kuzungumza nao.
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akizungumza na watumishi
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni