Na
Lydia Churi-Mahakama Rukwa
Jaji Mkuu wa Tanzania
Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewataka Mahakimu nchini kuanza kuzipitia Sheria
na kanuni zinazohusu uchaguzi.
Akizungumza na Watumishi
wa Mahakama ya Wilaya ya Nkasi wakiwemo Mahakimu, Jaji Mkuu amewataka Mahakimu
kuanza kujiandaa kusikiliza kesi za uchaguzi kwa kuanza kuzipitia sheria hizo
kwa kuwa mwaka huu nchi itafanya uchaguzi wa Serikali za mitaa na baadaye
mwakani uchaguzi mkuu.
Aidha, Jaji Mkuu pia amewaagiza
Mahakimu kutochelewesha kesi za uchaguzi ili wasije kuiingiza Mahakama kwenye
migogoro. Aliongeza kuwa endapo kesi hizo zitasikilizwa kwa mujibu wa sheria na
kumalizika kwa wakati zitasaidia kuifanya Mahakama kuendelea kuaminiwa zaidi na
wananchi.
Alisema endapo Mahakimu
watazipitia sheria na kujiandaa vema kusilikilza kesi hizo ni wazi kuwa
hawatababaishwa mahakamani. “Hakimu anayefahamu sheria na taratibu hawezi
kubabaishwa awapo Mahakamani”, alisema Jaji Mkuu.
Jaji Mkuu pia amewataka
Mahakimu kutojihusisha na masuala ya siasa ili waweze kuwa huru katika kusikiliza
kesi hizo. Alifafanua kuwa Sheria inamkataza Jaji, Msajili, na Hakimu kujiunga
na chama chochote cha siasa ili waweze kutatua migogoro inayoletwa kwao.
Awali akizungumza na Mkuu
wa wilaya ya Nkasi, Said Mohamed Mtanda, Jaji Mkuu amesema Mahakama ya Tanzania
inao mpango wa kujenga majengo ya mahakama za Mwanzo za kisasa kwenye kwenye
kila tarafa kwa nchi nzima ili kusogeza huduma zake karibu zaidi na wananchi.
“Tutahakikisha tunajenga
Majengo ya kisasa ili endapo kutatokea mabadiliko ya kiserikali kwa tarafa
husika kuwa wilaya basi majengo hayo hayo yatatumika kuwa Mahakama za wilaya”,
alisema Jaji Mkuu. Alisema Mahakama itaiomba Serikali Kuu kupeleka fedha za
ujenzi wa majengo hayo kwenye halmashauri ili halmashauri zijenge.
“Sisi tutatoa ramani za majengo, tutatafuta na
fedha ili halmashauri zijenge kwa kuwa tayari zinao uzoefu katika kujenga vituo
vya afya hivyo na jukumu la kujenga Mahakama za Mwanzo mlibebe.”
Awali akizungumza na Mkuu
wa wilaya ya Nkasi, Said Mohamed Mtanda alipomtembelea ofisini kwake, Prof.
Juma alihimiza ushirikiano wa Mahakama na mihimili mingine kwa kuwa Katiba ya
nchi pia inatambua na imegawa majukumu kwa kila mhimili ambapo alisema mihimili
yote haina budi kushirikiana kwa kuwa yote yanalo jukumu la humtumikia
mwananchi.
Mkuu huyo wa wilaya alisema
Serikali wilayani humo itashirikiana na Mahakama ya Tanzania kwa karibu ili
kuhakikisha wananchi wa wilaya hiyo wanapata huduma zote muhimu zikiwezo huduma
za mahakama.
Jaji Mkuu anaendelea na
ziara yake ya kikazi katika mkoa wa Rukwa ambapo leo alitembelea Mahakama za
wilaya ya Nkasi na Kalambo ili kukagua shughuli za Mahakama.
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim
Hamis Juma akiwa katika picha ya pamoja na kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya ya Nkasi alipomtembelea Mkuu wa wilaya hiyo ofisini kwake akiwa katika ziara ya
kikazi mkoa wa Rukwa.Viongozi mbalimbali wa Mahakama ya Tanzania walioambatana na Jaji Mkuu kwenye ziara yake wakimsikiliza alipokuwa akizungumza na watumishi wa Mahakama ya wilaya ya Nkasi.
Watumishi wa Mahakama ya wilaya ya Nkasi wakimsikiliza Jaji Mkuu.
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akiwa katika picha ya pamoja na wananchi wa wilaya ya Nkasi waliofika Mahakamani kupata huduma za kimahakama |
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni