Jumanne, 12 Novemba 2019

JAJI MKUU AISHAURI SERIKALI KUWATATHMINI WAPELELEZI NA WAENDESHA MASHITAKA


Na Lydia Churi-Mahakama Sumbawanga
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma ameishauri Serikali kufanya tathmini ya kazi inayofanywa na wapelelezi pamoja na waendesha mashitaka katika kesi iwapo wanatekeleza wajibu wao ipasavyo.  

Akizungumza na Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mhe. Joachim Wangabo alipomtembelea ofisini kwake akiwa katika ziara ya kikazi mkoani humo, Jaji Mkuu alisema Mahakama ya Tanzania inakabiliwa na changamoto ya kesi kutomalizika kwa wakati na wakati mwingine haki kutotendeka kutokana na wapelelezi pamoja na waendesha mashitaka kutotekeleza wajibu wao ipasavyo.

Aidha Jaji Mkuu ameishauri Serikali kuwabana wapelelezi na waendesha mashitaka ili wawe wanajiandaa vizuri katika kesi mbalimbali.

Alisema endapo maandalizi ya hati ya mashitaka katika kesi ni hafifu huweza kusababisha upelelezi wa kesi hiyo kutofanyika inavyotakiwa na hivyo kupelekea wakati mwingine haki kutotendeka na kusababisha mfumo wa sheria kutoaminiwa na wananchi. 

Alisema matumizi ya Tehama katika kesi yatarahisha na kusaidia haki kutendeka na kesi kumalizika kwa wakati huku akitolea mfano wa matumizi ya kipimo cha DNA kwenye kesi kubwa kama vile za mauaji na ubakaji. Alisisitiza umuhimu wa hivyo kuchukuliwa mapema kabla ya ushahidi haujapoa.

Akitolea mfano wa kesi kwenye Mahakama ya Rufani, Jaji Mkuu alisema wakati mwingine Majaji hukutana na changamoto ya maandalizi hafifu ya hati ya mashitaka kwa kuwa inakuwa haiendani na tukio lenyewe. 

Alisema kutokana na kukua kwa sayansi na Teknolojia, hivi sasa wapelelezi hawana budi kuchukua maungamo ya kesi kwa njia ya picha video. “Upelelezi bado uko karne ya 16 wakati wahalifu wako karne ya 21”, alisema Jaji Mkuu.  

Kuhusu Mahakama kuanza kutoa hukumu kwa lugha ya Kiswahili, Jaji Mkuu amesema suala hilo ni muhimu na Mahakama italifanyia kazi. Aliongeza kuwa hivi sasa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto kinatoa mafunzo kwa Mahakimu ya uandishi wa hukumu kwa lugha nyepesi na inayoeleweka zaidi.   

Awali akizungumza, Mkuu wa Mkoa wa Rukwa aliiomba Mahakama kushirikiana na Serikali ili kuhakikisha kesi  zinamalizika kwa wakati hususani zile zinazohusiana na mimba za utotoni kwa wananfunzi wa shule za msingi pamoja na Sekondari zilizopo kwenye mkoa wake.

Alisema tayari kesi 40 za makossa hayo zimefikishwa mahakamani lakini kati ya hizo ni kesi tatu tu ambazo zimesikilizwa na kutolewa maamuzi. Alisema katika kipindi cha mwaka moja kanzia Julai 2018 mpaka Oktoba 2019 katika mkoa wake kuna jumla ya wanafunzi 294 waliopata mimba wakiwemo 209 wa shule za sekondari na 85 wa shule za msingi.   

Naye Mkuu wa wilaya ya Sumbawanga Mhe. Halfan Haule aliiomba Mahakama kuangalia uwezekano wa kuanza kutoa hukumu kwa lugha ya kishwahili hasa kwenye ngazi ya Mahakama za wilaya ili kuwawezesha wananchi kuzielewa kwa urahisi.

Alisema hivi sasa wananchi walio wengi hutumia muda mwingi kuzunguka kwenye ofisi mbalimbali za wanansheria ili kupewa tafsiri za hukumu zao hatua inayowafanya kuchelewa kupata haki ikiwemo kuchelewa muda wa kukata rufaa endapo wanakuwa hawajaridhishwa na hukumu zilizotolewa.    

Jaji Mkuu ameanza ziara ya kikazi Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Sumbawanga ambapo awali alikagua miradi ya ujenzi katika mkoa wa Songwe pamoja na kupokea taarifa ya utekelezaji ya Mahakama kuu kanda ya Sumbawanga. Jaji Mkuu anaendelea na ziara kukagua shughuli za Mahakama katika wilaya za Nkasi na Kalambo.
 Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (kulia) akizungumza jambo mara baada ya kukagua jengo la Mahakama ya Mwanzo Mlowo lililomazika kufanyiwa ukarabati mkubwa hivi karibuni. Katikati mwenye miwani) ni Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brig. Jen. Nicodemus Mwangela na wa kwanza kushoto ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Mbeya Mhe. John Utamwa


 Jengo la Mahakama ya Mwanzo Mlowo kama linavyoonekana pichani baada ya kufanyiwa ukarabati mkubwa na Mahakama ya Tanzania kufuatia kuunguzwa moto wakati wa kipindi cha Uchaguzi Mkuu mwaka 2015. 


 Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wengine pamoja na watumishi wa Mahakama ya Mwanzo Mlowo mara baada ya kukagua jengo hilo lililomalizika hivi karibuni.

 Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akisaini kitabu cha wageni mara baada ya kuwasili kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoa wa songwe.             
                                                                                                                                                                     

 Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma(katikati) akiwa katika picha ya pamoja na wenyeji wake mkoani Rukwa, Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mhe. Joachim Wangabo (wa pili kushoto) na Mkuu wa wilaya ya Sumbawanga Mhe. Halfan Haule (wa kwanza kulia) mara baada ya kumtembelea Mkuu huyo wa Mkoa ofisini kwake.  Wa pili kulia ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Sumbawanga Mhe. David Mrango na wa kwanza kushoto ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Sumbawanga  Mhe. Willbard Mashauri.
 Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brig. Jen. Nicodemus Mwangela akimuelezea jambo Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma wakati Jaji Mkuu alipotembelea kiwanja kitakapojengwa jengo la Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoa wa Songwe. Jaji Mkuu ameanza ziara ya kikazo katika Mkoa wa Rukwa.


Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brig. Jen. Nicodemus Mwangela akiwa ameshika kitabu kinachoonyesha mpango wa ujenzi wa majengo ya Mahakama ya Tanzania nchini mara baada ya kukabidhiwa na Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma.
Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Momba Mhe. Zabibu Abeid Mpangule akimueleze jambo Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma mara baada ya kukagua Mahakama hiyo akiwa njiani kuelekea mkoano Rukwa kuanza ziara ya kikazi. Kulia kwake ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Mbeya Mhe. John Utamwa.
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akisalimiana na Watumishi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Sumbawanga alipowasili Mahakamani hapo kukagua shughuli za Mahakama akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Rukwa. 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni